Moi, Kibaki wapishana hospitali Nairobi

0
662

NAIROBI, KENYA

KATIBU binafsi wa Rais wa zamani wa Kenya, Mwai Kibaki amekanusha taarifa kwamba kiongozi huyo amelazwa katika Hospitali ya Nairobi.

Katibu huyo, Ngari Gituku amesema kuwa Kibaki mwenye miaka 88 alifika katika hospitali ya Nairobi Jumatatu kwa ajili ya utaratibu wa kawaida wa  kuangalia afya yake.

 “Ilikuwa ni safari ya kawaida na hakuna kitu kipya,” aliliambia gazeti la Daily Nation la nchini Kenya kwa njia ya simu.

Wakati ikielezwa kuwa Kibaki anasumbuliwa na tatizo la goti baada ya kupata ajali ya barabarani huko Machakos  mwaka 2002,  Gituku kwa upande wake hakuthibitisha kama ni sababu ya sasa ya yeye kwenda hospitalini.

“Kwa umri wake, wanaweza kumchunguza kitu chochote, kama macho, kibofu cha mkojo na vitu vingine,”  alisema.

Chanzo kimoja cha habari ambacho kimekataa kutajwa jina kwa sababu yeye si msemaji wa familia kilisema kuwa rais huyo mstaafu hali yake inaendelea kuimarika na kwamba alikuwa katika hali ya tahadhari.

Hatua ya Kibaki kufika katika hospitali ya Nairobi kulikuja katika siku ambayo Rais wa Mstaafu wa Kenya na ambaye ametawala nchi hiyo kwa muda mrefu, Daniel Arap Moi naye akirejea hospitalini hapo kutokana na kile ambacho msemaji wake Lee Njiru kusema kuwa ni “uangalizi wa kawaida”.

Ingawa chanzo cha habari kutoka katika familia ya Moi kilisema kuwa kiongozi huyo ambaye ana miaka 95 alikimbizwa hospitalini hapo Oktoba 18 mwaka huu baada ya kupata tatizo la kupumua.

Kwa upande wake Kibaki, ambaye ni kiongozi wa zamani wa chama cha Narc, anajiandaa kusheherekea miaka 89 ya kuzaliwa Novemba 15 mwaka huu.

Mara ya kwanza alifikishwa hospitali ya Nairobi Januari 20, 2004.

Timu ya wataalamu waliokuwa wakimtibu walisema kuwa walibaini kuganda kwa damu katika mguu wake wa kulia.

Mwezi Agosti 2016,  kiongozi huyo wa zamani alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya  Netcare Sunninghill iliyoko nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuondoa kuganda huko kwa damu katika mshipa wa kwenye shingo yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here