Takukuru yafikisha watatu kortini

  0
  419

  ANDREW MSECHU –dar es salaam

  TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafikisha mahakamani wafanyabiashara watatu wa mafuta kwa kughushi na kufanya kazi Tanzania bila kuwa na kibali.

  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru, Ali Mfuru, aliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni raia wa China, Yu Hattao na Zhang Zhi Xin ambao ni wamiliki wa Kampuni ya Shin Up Limited iliyopo Visiga, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na John Mnyele, ambaye ni mfanyabiashara Mtanzania.

  Alisema taasisi kwa kushirikiana na polisi wamewafikisha mahakamani watu hao kwa makosa tofauti, ambayo yanahusiana na kughushi na kukiuka taratibu za ujenzi.

  “Mshtakiwa wa kwanza, Yu Hattao anakabiliwa na makosa mawili, la kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335 (a) na 337 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 (marejeo ya 2002), huku akikabiliwa na kosa la kufanya kazi nchini bila kibali kinyume na kifungu cha 9 (1) (a) (b) na 20 (d) cha kanuni za ajira na 1 ya mwaka 2015,” alisema Mfuru.

  Alisema makosa mengine yanayowahusu watuhumiwa wote ni kuendesha shughuli za ujenzi bila kupata kibali cha ukaguzi wa mazingira kinyume na kifungu cha 81 cha sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005 na kifungu cha 60 (1) vikisomwa kwa pamoja na kifungu namba 191 cha sheria ya mazingira.

  “Kosa jingine ni kujenga mtambo wa kusafisha mafuta ya dizeli bila kibali cha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kinyume na kifungu cha 127 (1) na (2) cha sheria ya Petroli Na 21 ya mwaka 2015,” alisema Mfuru.

  Alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, inawashukuru Watanzania wazalendo ambao wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana nao kuwafichua wote wanaolihujumu taifa kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu na rushwa.

  LEAVE A REPLY

  Please enter your comment!
  Please enter your name here