32.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

MKUU WA SHULE AJINYONGA HADI KUFA


Na EDITHA KARLO, KIGOMA   |    

MKUU wa Shule ya Sekondari Kakonko katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Peter Rubonya, amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba ofisini kwake jana.

Akielezea tukio hilo, mwalimu wa zamu wa shule hiyo, Isaac Japhet, alisema alifika shuleni hapo saa 12:30 asubuhi kufundisha wanafunzi wa kidato cha nne masomo ya ziada baada ya kufunga shule wiki iliyopita na baadaye aligundua hana chaki na mkuu huyo wa shule alimpatia chaki mlinzi wa shule hiyo ili awape wanafunzi.

Alisema baada ya muda mfupi, mratibu wa elimu kata na mmoja wa wazazi walifika ofisini hapo wakiwa na shida na mkuu wa shule na walielezwa kuwa yupo ndani ofisini.

Hata hivyo, baada ya kugonga mlango hawakujibiwa na ndipo waliamua kuufungua kwa nguvu na kukuta mwili wa marehemu ukining’inia darini.

Mwalim Isaac alisema hawakuwahi kusikia mkuu huyo ambaye alikuwa akifundisha pia masomo ya kemia na fizikia shuleni hapo, ana mgogoro wowote wa familia au jamii na kwamba mkewe ambaye ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alifika nyumbani kwake juzi akitokea Dodoma.

Mlinzi wa shule hiyo, Kajolo Kajabojabo, alisema alikutana na mkuu wa shule mapema asubuhi jana akiingia ofisini na kumwomba chaki ambazo alipewa na kuziwasilisha kwa walimu.

“Nilimuona kabisa tukasalimiana, nikamuuliza kama anaweza kuwa na chaki, akaingia ofisini akanipatia boksi moja la chaki, nikachukua nikampelekea mwalimu aliyekuwa anazihitaji, alikuwa kwenye hali nzuri tu, lakini baada ya muda ndiyo tukio hilo likatokea,” alisema Kajoro.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala, akizungumza baada ya kutembelea shule hiyo na kumfariji mjane, alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kujua sababu za kifo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno, alisema anasubiri taarifa rasmi juu ya tukio hilo ili aweze kulitolea ufafanuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles