29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WATUHUMIWA KIFO CHA MUUZA MACHUNGWA


Na PENDO FUNDISHA - MBEYA

JESHI la Polisi mkoani Mbeya linatuhumiwa kusababisha kifo cha mfanyabiashara ya machungwa, Allen Mapunda mkazi wa Uwanja wa Ndege, Kata ya Iyela mkoani hapa baada ya kumkamata na baadaye kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa siku ya tukio Mapunda alikuwa katika kibanda cha kuchezea ‘pool table’ na kamari.

Walidai polisi wa doria walifika katika kibanda hicho saa 5:00 usiku na Mapunda alipowaona alikimbilia katika kibanda cha chakula.

Mmoja wa wahusika wa kibanda cha chakula, Vicent Abraham (26), alisema baada ya Mapunda kukimbilia huko, aliwaambia askari wanakuja.

“Nadhani walimsikia wakaja na kutukamata nikiwamo na mimi kwa madai kuwa nilichelewa kufunga,” alisema Abraham.

Mama mdogo wa marehemu, Aris Mapunda, alisema siku ya Jumamosi alipata taarifa kuwa mwanawe amekamatwa kwa kosa la uzururaji na alipokwenda kumwekea dhamana Jumapili, alimkuta akiwa dhaifu, anatetemeka huku akilalamika alipigwa na askari.

Aris alisema baada ya kuachiwa, walimpeleka Hospitali ya Mkoa kwa matibabu na baadaye walimhamishia Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambako alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu.

“Madaktari walituuliza huyu mtu mbona inaonekana kama kapigwa sana, maana kila unapomgusa analalamika.

“Wakatuuliza kama polisi wametupa fomu maalumu ya matibabu (PF3), nikawaambia hawakutupa.

“Lakini awali kabla hatujaondoka kituoni tuliomba hiyo fomu na askari mmoja akatujibu ya nini, kwani amepigwa? Huyo anaumwa ugonjwa wa Mungu tu.

“Wakati tunatoka kituoni, alikuwa anapumua kwa shida na anazungumza kwa tabu, ukimuuliza swali anakuangalia na kudondosha machozi, aliweza kusema ‘wamenipiga na sijafanya kosa lolote’,” alisema Aris.

Hata hivyo, baada ya taarifa za kifo cha kijana huyo kusambaa, kundi la vijana lilifanya uharibifu katika ofisi za kata na kuvamia nyumbani kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Iyela 2, Boazi Kazimoto kwa kile walichodai ndiye aliwaita polisi waliomkamata Mapunda na kusababisha kifo chake.

Kazimoto alisema akiwa nyumbani kwake alipewa taarifa vijana wanamtafuta wakimtuhumu kuwaita polisi ambao walimkamata Mapunda na hatimaye kufariki dunia.

“Jumapili saa mbili usiku kundi la vijana lilivamia nyumbani kwangu na kunitaka nitoke nje, lakini watoto wangu walinizuia, baadaye nikasikia mabomu,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema taarifa za kifo hicho atazitoa leo mara baada ya kuziandaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles