23.6 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Mkutano nchi za SADC utakuwa chachu ya uwekezaji

Anthony Benedictor – MAELEZO

WAKATI Serikali ya awamu ya Tano ikielekea kukamilisha miaka minne tangu iingie madarakani, mambo mengi makubwa yamefanyika na yanaonekana kitaifa na kimataifa.

Katika toleo maalum la Jarida la Forbes la hivi karibuni, Rais Dk. John Magufuli ameelezewa kuwa ni kiongozi ambaye kwa maono yake Taifa la Tanzania litafikia maendeleo ya viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati kutokana na jitihada zake za kuimarisha miundombinu, kusimamia uchumi, lakini pia kupambana na ufisadi.

Wakati huu tunapoelekea katika mkutano wa wakuu wa nchi za SADC, ni dhahiri kwamba Watanzania watapata fursa ya  maendeleo yanayoendelea nchini kujiimarisha kiuchumi.

Mbali na yaliyojiri katika mahojiano na Rais Dk. Magufuli, ni ukweli usiopingika kwamba kwa nchi zinazoendelea Tanzania sasa ni miongoni mwa nchi chache ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ukiendelea kuakisi uboreshwaji wa huduma muhimu na za msingi kwa wananchi.

Mkutano wa viongozi wa nchi za SADC unaotarajiwa kufanyika nchini, utachochea na kusaidia kuimarika kwa biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine katika umoja huo.

Ukiangazia uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam, ni eneo mojawapo ambalo nchi wanachama watahitaji kulijadili kwa kina ili kuona namna ya kushirikiana kuitumia bandari hiyo kwa manufaa si tu ya Watanzania bali ya nchi wanachama kwa ujumla.

Aidha, uimarishaji wa usafiri wa anga ni jambo ambalo litaisaidia nchi kwani wakati wa mkutano huo wa SADC shirika letu la ndege litapata biashara lakini pia itakuwa ni sehemu ya kuzitangaza ndege na shirika ambalo kabla ya maboresho yanayofanywa katika awamu ya tano lilikuwa taabani.

Fursa nyingine ambayo mkutano huo utaweza kuzitangaza ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ambao kukamilika kwake si tu faida kwa Watanzania bali hata kwa majirani ambao hawana bandari.

Tanzania ama kwa hakika ikichangamkia uwapo wa mkutano wa wakuu wa nchi za SADC milango mingi ya biashara na uwekezaji itafunguliwa, mbinu mpya za kuuziana mazao zitaibuliwa na pia kubadilishana utaalam ambao kama ingelazimu kuupata nje ya Afrika ingekuwa ghali.

Kwakuwa sekta ya nishati inaendelea kuimarika nchini na tunatarajia kuwa na umeme wa kutosha kwaajili ya kufanikisha Tanzania ya viwanda, ujio wa wageni hao wa SADC utatumika pia kama fursa ya kuwaeleza jinsi watakavyoweza kufaidika na uwapo wa nishati ya kutosha hasa kwa wale watakaotaka kuwekeza katika viwanda.

Mbali na kuwa na vivutio vingi vya kitalii hapa nchini, mkutano huo pia ni muhimu katika kuiinua sekta hiyo kwani utaimarisha utalii kutokana na wageni wengi watakaohudhuria, lakini itakuwa kama uimarishaji wa utalii wa ndani ya Afrika bila kutegemea tu wageni kutoka katika mataifa ya Ulaya.

Nchi inapokuwa na ugeni mkubwa kama huo unaotarajiwa wa wakuu wa nchi za SADC, ni dhahiri nchi itafaidika na uwapo huo lakini tuone ugeni huo kama fursa maana ni mkubwa utakaoacha mamilioni ya fedha za kigeni hapa nchini, lakini pia utasaidia kufungua milango ya uwekezaji na biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,070FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles