27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo ya kisiasa yasiue kabumbu

JAVIUS KAIJAGE

IKIWA imepita takribani miaka 39, nchi yetu kwa mara nyingine mwaka huu imefanikiwa kutinga michuano ya fainali za mataifa ya Afrika ijulikanayo kwa jina maarufu la  (AFCON).

Mafanikio haya hayakuja kama zawaidi ya  mvua ya mawinguni  tunayopewa na Mwenyezi Mungu, bali ni juhudi za wanadamu ambao kimsingi ni wachezaji wetu waliojitolea kufa na kupona ili nchi yetu itambulikane kimataifa na kufuta jina la kichwa cha mwendawazimu.

Ajabu pamoja na jitihada zilizofanywa na wachezaji wakisaidiana na benchi la ufundi, hatimaye kufuzu kuingia AFCON, walipoanza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Senegal na kuchapwa mabao mawili kwa bila,  yameibuka mambo ambayo hayakutarajiwa.

Ni dhahiri wanasiasa wakiwamo wabunge, viongozi wa serikali na hata  wananchi wa kawaida kwa ujumla wamelazimika kuingia katika michuano ya maneno makali  ili hatimaye kumpata mshindi mwenye ulimi mkali.

Wanasiasa kulaumiana na kusutana hadharani kwa ajili ya timu ya Taifa Stars halikuwa jambo la heri kwa kuzingatia kuwa timu hiyo ilikuwa bado inazo mechi takribani mbili ambazo kimsingi kama wangejipanga vizuri kisaikolojia na kibaiolojia, uwezekano wa kuingia katika nafasi ya 16 bora bado ulikuwapo.

Nadiriki kusema hata mchezo uliofuata kati ya Taifa Stars na Harambee Stars kutoka Kenya, wanasiasa kwa namna moja au nyingine huenda ndio wamechangia nchi yetu kubwagwa chini.Nasema wanasiasa wamechangia kwa maana ya kwamba kutokana na mashindano ya maneno yaliyoibuka kati yao yalikuwa na uwezo mkubwa kuvuruga na kuwatoa mchezoni wachezaji, kwani badala ya kutumia akili na nguvu za mwili, huenda wachezaji  walitumia nguvu peke yake ili kuhakikisha wanapata ushindi kwa kulazimisha kama lengo la kukwepa mishale ya maneno kwani  pamoja na kuwa walikuwa mbali huko Misri lakini kutokana na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kila tukio lililokuwa likiendelea nchini walikuwa wanapata taarifa.

Ni mambo ya kusikitisha kwani wachezaji walipofuzu kuingia michuano hii mikubwa barani Afrika tena baada ya  muda mrefu kupita, wananchi wakiwamo wanasiasa kwa umoja wetu tulifurahi huku tukiongea lugha moja, sasa inakuwaje baada ya kuteleza kidogo tuparaganyike?

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Ni kweli kisaikolojia kila binadamu huwa na shauku ya kupata mafanikio kwa kila jambo alilolipanga na inapotokea akashindwa maumivu yake huwa makubwa kwani matarajio yake haikuwa hivyo, lakini kuna kila sababu ya kutafuta njia chanya ili kusonga mbele kwa kusudi la kupata ushindi.

Ikumbukwe kuwa wachezaji wanapokuwa katika mashindano wanakuwa kama askari walioko vitani mstari wa mbele   ili kuipigania nchi yao isitekwe na maadui na ndiyo maana ikitokea hofu hulishwa nyama ya ulimi kutoka kwa makamanda wao kama njia ya kuwahamasisha kusudi wasonge mbele hata kama mashambulizi ni makali mno.

Si hivyo tu bali pia wanajeshi wakitumia silaha fulani zikashindwa kuangamiza maadui huwa hawaachi kupigana bali  ni kutafuta silaha mbadala  huku wakijitathimini upya  katika   mbinu zao  za mapambano  wanazotumia.

Hatua ambayo vijana wetu wachezaji wamefikia katika mashindano ya  mwaka huu si haba kwani  mikakati ikipangwa vizuri mashindano yatakayofuata watafanya vizuri  zaidi ya walipofikia maana  miaka 39 iliyopita wapo  waliokuwa wakithubutu lakini walikuwa  wakiishia njiani hivyo wanasiasa  wasihofu.

           Ni kweli katika nchi inayoheshimu demokrasia na uhuru wa kujieleza suala la kulaumiana, kulumbana, kusutana au kunyosheana vidole wakati mwingine huwa  ni mambo yanayojenga  uwezo wa kufikiri lakini pia  ikumbukwe kuwa,  tunapojenga soka letu  hatuna sababu ya kugombana  na wachezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles