23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Miradi ya maji miji 28 kutumia Sh trilioni 1.3

Mwandishi wetu -Kilwa

TATIZO la maji katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi litakuwa historia baada ya kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Mavuji, ambao ni mmoja kati ya miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa Sh trilioni 1.3.

Akizungumza wilayani hapa juzi baada ya kufanya ziara ya siku moja, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, alisema mradi huo ni miongoni mwa mingine inayotekelezwa katika miji 28 nchini.

Profesa Mbarawa alisema miradi hiyo yote inagharimu Sh trilioni 1.38, fedha ambazo ni mkopo kutoka Serikali ya India na kwamba inatarajia kuanza kutekelezwa Desemba.

Alisema kwa Wilaya ya Kilwa mipango ya Serikali ya muda mfupi ni kuchimba kisima kirefu katika Hospitali ya Kinyonga iliyopo mji mdogo wa Kivinje na mpango wa muda mrefu wa kutoa maji kutoka Mto Mavuji.

Akiwa katika mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Kilwa – Kivinje, Profesa Mbarawa aliwaahidi wananchi kuwa tatizo la maji sasa litakuwa limefika mwisho. 

“Sitoi ahadi hii mbele yenu tu, bali natoa ahadi hii mbele ya Mwenyezi Mungu aliyenipa nafasi ya kufika hapa leo kuongea nanyi,” alisema Profesa Mbarawa.

Awali Profesa Mbarawa akiongea na watumishi wa Wilaya ya Kilwa, aliwataka kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu ili kuwaletea wananchi kile wanachotarajia kukipata.

“Niwaombe watumishi wenzangu, Rais Magufuli anataka kuona matokeo ya kile kinachofanyika na si hizi taarifa nzuri mnazotuandikia, anataka kuona mnawaondolea wananchi kero zao, hii si karne ya kutembea na ndoo kichwani kilomita tano kufuata maji.

 “Katika taarifa yenu nimeona upungufu wa watumishi katika Idara wa Maji, lakini naomba waliopo wafanye kazi kwa bidi wakati tukiendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo,” alisema Profesa Mbarawa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, akisoma taarifa ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kilwa yenye ukubwa wa kilometa za mraba 13,290 na wakazi wanaofikia 203,000 alisema hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa si ya kuridhisha.

Ngubiagai alisema ni asilimia 62 tu ya wilaya ndiyo inayopata maji kwa maeneo ya mijini na asilimia 59 kwa vijijini.

Alisema mipango iliyopo ni kutekelezwa kwa mradi mkubwa kutoka Mto Mavuji, huku mpango wa muda mfupi ukiwa ni kuchimba visima saba katika vijiji na vitongoji saba. 

Ngubiagai alisema kwa sasa kuna visima 408 vinavyotumia pampu za mikono, huku vinavyofanya kazi vikiwa 335.

Pia alitaja changamoto zinazokabili Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) katika Wilaya ya Kilwa, kuwa ni pamoja na baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa ankara kwa wakati na uharibifu wa miundombinu ya maji, hasa katika maeneo ya vijijini.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala maarufu kama Bwege, alimshukuru waziri huyo na kuwataka wananchi kuamini yote aliyowaahidi kwani ni mtu mkweli na muugwana.

 “Ndugu zangu wana-Kilwa, huyu bwana (Profesa Mbarawa) ni mtu mkweli na muungwana, tumuombee Mwenyezi Mungu ampe afya njema ili yote aliyotuahidi yakamilike kwa wakati,” alisema Bungara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles