Radi yaua watu wanne, yajeruhi 10

0
853

Gurian Adolf -Nkasi

WATU wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 10 wamejeruhiwa baada ya kupigwa radi wakiwa kilabuni wakinywa pombe katika Kijiji cha Kate, Wilaya ya Nkasi mkoani Rungwe.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kate, Willbroad Feluzi, alisema lilitokea juzi saa 12:30 jioni.

Alisema wakati watu hao wakiendelea kunywa pombe katika kilabu hicho, ghafla ilipiga radi eneo hilo, iliyosababisha wengi kuanguka na kupoteza fahamu.

Feluzi alisema baada ya kuwafanyia uchunguzi, ilibainika wanne kati yao wamepoteza uhai na wengine kujeruhiwa.

Alisema majeruhi wote walikimbizwa zahanati ya Kanisa Katoliki na wale waliozinduka waliruhusiwa kurudi nyumbani.

Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni John Sumuni (31), Akleo Feluzi (45), Boniphace Fundililwa (38) na Annastazia Njali (48), wote wakazi wa kijiji hicho.

Mganga Mkuu wa Zahanati ya Mission Kate, Elly Joseph, alikiri kupokea majeruhi zaidi ya 10, na baada ya kuwapatia huduma ya kwanza wengi wao waliruhusiwa kurudi nyumbani na wanne walikuwa mahututi wanaendelea na matibabu hadi sasa.

Dk. Joseph alisema kati ya majeruhi hao, waliobaki watatu wanaendelea vizuri, isipokuwa mmoja ambaye alipata kidonda mguuni hali yake si nzuri.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda alikiri kutokea tukio hilo na kuthibitisha vifo hivyo.

Mtanda alisema baada ya kikao na viongozi wenzake, watakwenda kijijini hapo kuwajulia hali majeruhi na kushiriki mazishi.

Alisema baada ya hapo atatoa ripoti zaidi juu ya tukio hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here