24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 ya Uhuru| Wizara ya Mambo ya Nje yajivunia mchango wake kwenye kuleta Amani

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

WIZARA ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetaja mafanikio ambayo imeyapata ndani ya miaka 60 ya Uhuru huku ikiweka wazi suala la uraia pacha kwa kudai inaanza na hati maalum.

Pia imesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, ulinzi na usalama Barani Afrika na duniani kwa ujumla, katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Novemba 20, 2021 na Waziri wa Wizara hiyo,Balozi Liberata Mulamula wakati akitaja mafanikio iliyoyapata Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60.

Balozi Mulamula amesema kwa sasa wanaondoka katika uraia pacha na wanaenda kwenye hati maalum ambapo amedai hiyo ndio njia mbadala ya kutambua mchango wa watanzania wanaoishi nje ya Tanzania.

“Bado tunaendelea na sasa hivi tunaendelea sasa tunaondoka kwenye uraia pacha tunaenda kwenye hati maalum ambayo ndio naona itatuvusha maana suala la uraia pacha ni mchakato wa kikatiba lakini hati maalum tukitumia mifano ya Nchi kama India mimi nimesoma nimeielewa na hiyo ndio njia mbadala kuweza kutambua mchango wa Diaspora,”amesema.

AWATAKA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA YA KISWAHILI NJE YA NCHI

Katika hatua nyingine, Waziri Mulamula amewataka Watanzania kuchangamkia fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nje ya Nchi ambapo amedai soko na mahitaji ni makubwa.

“Rai yangu watanzania tuchangamkie fursa tusingoje vya kupewa Nchi jirani wanachangamkia sana,Sasa hivi tupo katika mkakati tunapeleka watu wanaofaa na wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo na mahitaji ni mengi wana Diaspora wanatusaidia,”amesema.

MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA ULINZI WA AMANI NA USALAMA

Waziri Mulamula amesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, ulinzi na usalama Barani Afrika na duniani kwa ujumla, katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

“Katika kipindi hicho, Tanzania imeshiriki katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo kwenye nchi mbalimbali duniani. Ushiriki wa Tanzania katika harakati hizo umekuwa wa moja kwa moja au kupitia jumuiya za kikanda.

“Kwa mfano, mwaka 1999 Tanzania ilishiriki katika kuzipatanisha pande mbili zilizokuwa zikihasimiana nchini Burundi. Mpatanishi Mkuu katika mgogoro huo alikuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kabla ya kifo chake na baadaye juhudi hizo ziliendelezwa na Hayati Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu.

“Usuluhishi wa mgogoro huo ulitamatishwa kwa pande zinazohasimiana kusaini Makubaliano ya Amani na Maridhiano ya Arusha mwaka 2000 na Makubaliano ya Kusitisha Mapigano mwaka 2005, ambayo yamedumisha amani nchini Burundi hadi hivi sasa.

“Mwaka 2015 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilimteua Hayati Benjamin Mkapa kuongoza Majadiliano ya Amani ya Burundi baina ya pande zilizokuwa zikihasimiana nchini humo kufuatia mgogoro wa kikatiba uliombatana na machafuko yaliyotokana na tofauti za kisiasa,”amesema.

MAFANIKIO YA KIUCHUMI

Pia amesema Tanzania imepata mafanikio ya kiuchumi kupitia uhusiano baina yake na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa.

“Uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi nyingine unatokana na uwepo wa mikataba na makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Mathalan, kupitia makubaliano ya ushirikiano katika biashara baina ya Tanzania na nchi za Oman, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia, nchi yetu inauza mbogamboga, nyama na bidhaa za nyama katika masoko ya nchi hizo.

Kadhalika, kupitia makubaliano ya hivi karibuni ya biashara kati ya Tanzania na China, kampuni 72 za kitanzania zimepata ithibati kutoka katika mamlaka za China kuuza maharage ya soya katika soko la nchi hiyo ambapo zaidi ya tani 120 za bidhaa hiyo tayari zimeuzwa nchini humo,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles