22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 55 YA UHURU NAIONA TANGANYIKA IKING’ARA NDANI YA TANZANIA

120511-national-this-day-black-history-tanaznia-independence

NA HELLEN KIJO BISIMBA,

HONGERA sana Tanganyika kufikia miaka 55 ya uhuru. Yupo aliyeniambia hiyo Tanganyika haipo hivyo niseme hongera Tanzania.  Huenda yuko sahihi lakini bahati nzuri sana mimi nimesoma historia na ninaipenda historia na ninajua uzuri na umuhimu wake.

Hatuwezi kuipindisha historia. Miaka 55 ni ya Tanganyika kwani wakati uhuru ukipatikana Tanzania haikuwepo, ilikuja miaka mitatu baadaye. Kwa vile tumeamua kusherehekea uhuru wa Disemba 9, 1961 basi tuikumbuke tu Tanganyika ambayo ni sehemu ya Tanzania.

Kwa wale wenye kumbukumbu nzuri, miaka miwili iliyopita tulipokuwa tunasherehekea miaka 53 ya uhuru huu, niliandika makala iliyokuwa ikihoji nini tulicho nacho cha kujivunia  katika miaka hiyo 53. Bila kuingia katika mabishano ya Tanganyika na Tanzania  nataka kujihoji tena miaka miwili baadaye hali ikoje?

Katika makala ile ya miaka miwili iliyopita nilikuwa naugua sana kutokana na rushwa na ufisadi uliokuwa umekithiri nchini, hali ya mali zetu za kitaifa na mkwamo wa kila kilichokuwa chetu kama vile Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzaniai ), Shirika la Reli na hata reli ya TAZARA, mbali na  viwanda vyetu mbalimbali hasa vile vya nguo na hata Tanganyika Pakers kilichokuwa kikisindika nyama ya ngo’mbe.

Mwaka jana ikiwa ni miaka 54 ya Uhuru Rais John Magufuli alipoingia madarakani aliona hakuna sababu ya kufanya  sherehe  kwa jinsi tulivyozoea na akaona ni heri tujikite katika kufanya usafi  wa nchi yetu chafu na fedha zote za sherehe akazielekeza kuongezea barabara ya Mwenge/ Moroko. Najua watu walihoji,nikiwa mmoja wao na wengine hawakufurahi kabisa lakini ukweli kabisa nikitafakari zaidi mimi naona maamuzi yale pamoja na kuwa niliuliza maswali ya kiutawala kama vile mamlaka ya Rais katika kubadili kasma kwa mujibu wa sheria na utawala bora, hayakuwa mabaya kivile.

Katika ubinafsi wangu ile barabara ilioongezwa, huwa naitumia nikienda kazini kwa hiyo msongamano kidogo umepungua. Na pia kidogo usafi umeongezeka. Lakini hoja hapa si fedha kutumika vipi na sherehe kutofanyika na aliyeidhinisha nani au nini; suala ni kuwa mambo hayakufanyika kikawaida hiyo niliiona kama dhana ya msingi Rais Magufuli alikuwa akiiweka.

Tangu aingie madarakani Rais Magufuli amejaribu kutaka kufanya mambo tofauti na ilivyozoeleka. Katika kufanya hivyo kuna sehemu amefanya vizuri sana na hata kuvuta kuungwa mkono kusifiwa si hapa tu hata nje ya nchi. Nikitaja machache ni pale aliposhindwa kuvumilia uzembe na hata kuwaachisha wateule wake walioonekana kutotimiza wajibu kama walivyotarajiwa.

Hili ni jipya sana maana tulikuwa tunalalamika pale watendaji wanapoboronga hadi kuitwa majina (mawaziri mizigo) lakini huachwa tu. Pia maamuzi ya kununua ndege za Shirika la Ndege la Tanzania na kuwa sasa ndege hizo zimeanza kupasua anga.

Najua watu walikuwa na mawazo mbadala na tofauti na wengine wakikejeli aina ya ndege zilizonunuliwa. Lakini kama ulisoma makala ile nilioizungumzia hapo juu hiki kilikuwa kilio changu angalau tuwe na sisi na kitu cha kujivunia “the wings of Kilimanjaro”.  Natumaini tukiwa na mawazo chanya hili shirika litakuwa na kutuinua  kama si kwa mali basi kwa hali.

Rais Magufuli pia amesisitiza azma yake ya kuijenga Tanzania ya viwanda. Sisi tunakodoa macho kweli tukivikumbuka viwanda tulivyokuwa navyo na kutamani hali hii itokee sasa, kwani ni heshima kwa nchi yetu. Rais pia amejitanabahisha kuwa ni mchukia rushwa ambayo ndio iliyotufikisha hapa tulipo na Rais wa wanyonge.

Kutokana na haya ambayo yanaonekana mwaka mmoja tu katika utawala wa Rais Magufuli ningependa sana kumpongeza. Lakini wakati huo huo ningetamani sana hata nikutane na Rais ana kwa ana nimpe mkono kwa maono haya, ila sijaribu maana marais waliomtangulia wawili niliwahi kujaribu kukutana nao  hadi leo nasubiri majibu.

Kama ningekutana na Rais ningemsihi sana aongeze kasi katika kupambana na rushwa kwani iko kama ndago pamoja na kauli yake ya kumaanisha bado rushwa za rangi mbalimbali zinaendelea.

Kila mara nakutana bado na watu wanoombwa rushwa kabla ya huduma tena bila hofu wala woga. Pamoja na Rais kuonyesha anavyoichukia rushwa na ufisadi bado kumekuwa na wanafunzi hewa katika elimu bure aliyoianzisha. Pia bado hatujaona jinsi lile sakata la Lugumi lilivyoshughulikiwa kwa ukamilifu wake.

Upande mwingine wa shilingi ambao ningependa kuugeuza Rais aone ni umuhimu wa juhudi zake kupata baraka za kisheria na kufuata misingi ya haki za binadamu. Kuna watu hupenda kupindisha mambo. Lakini ukweli ni kuwa Rais akiendelea kufanya kazi zake kwa juhudi hivi na akakosa misingi ya kisheria itakuwa rahisi sana yote aliyoyajenga kuwa kama  mwanasesere wa theluji jua likichomoza  huyo huyeyuka hata kama alikuwa mzuri kiasi gani.

Haki za binadamu zisipozingatiwa machungu na majeraha hubaki mioyoni mwa watu na hii si afya. Kwa kasi hii ya Rais anayejali wanyonge ajitahidi sana kuyafanya yote kwa mujibu wa sheria , taratibu na haki na hayo yatakuwa yamejengeka katika udongo mgumu na yatakuwa ya kudumu.

Mfano mdogo ni kisa cha wamachinga waliomchagua.  Zipo sheria za halmashauri zinazoonyesha wapi biashara zifanyike na  kwa vipi. Miji hupaswa kupangwa kwa ajili ya usafi na utanashati. Ni kweli kuwa wamachinga wamekuwa na hali ya kubughudhiwa sana na askari wa miji.

Lakini suluhisho la kudumu si kuwaambia waendelee kufanya kazi zao kiholela, pawe na njia ambazo mamlaka za miji kama ambavyo nyingine zimeanza, kutenga maeneo na kuwawezesha wamachinga kufanya kazi zao kwa staha. Vinginevyo watazagaa  kiasi ambacho mji utakuwa haupitiki au kukalika.

Miaka 53 ya uhuru tulikuwa hatuoni mbele, sasa kuna mwanga unaanza kuonekana ila miali hiyo itathibitika na Tanzania ilioibeba Tanganyika itainuka iwapo juhudi za Rais Magufuli zitabebwa katika misingi ya  kisheria na hasa Katiba inayochukua yote hayo.

Ikiwa hivyo naiona Tangayika iking’ara ndani ya Tanzania, viwanda hivyo, wananchi wenye amani na furaha mioyoni mwao wakifanya kazi vizuri sana bila hofu wala tashwishi hao,  mafisadi wakisota magerezani  bila kujali walikuwa na hadhi gani, walipa kodi wakiongezeka tena wakigombania kulipa kodi.  Hii haitakuwa nchi ya kufikirika itakuwa ndio nchi yetu, kwa juhudi ninazoziona  zikiwa zimeelekezwa katika usahihi wake ndani ya katiba yenye kuweka  sheria na heshima ya  haki za binadamu. Mungu ibariki Tanzania.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles