FRANCIS GODWIN, IRINGA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera ,Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameagiza ujenzi wa vituo 20 vitakavyotoa huduma za ugonjwa Ukimwi kwa wasafiri wa masafa marefu vinavyojengwa chini ya Programu ya Sattf barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda nchi za kusini mwa Tanzania kukamilisha ujenzi huo ndani ya mwezi mmoja.
Alitoa agizo hilo juzi,baada ya kuwekaji wa jiwe la msingi kituo cha afya Ipogolo mjini Iringa kwa niaba ya vituo vingine.
Alisema hajafurahishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa vituo hivyo ambavyo kimsingi ujenzi wake ulipaswa kukamilika tangu Oktoba, mwaka huu.
Alisema ujenzi wa vituo 20 kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma – Momba mpakani wa Tanzania na Zambia,Serikali imekwishatumia Dola za Marekani milioni 3, japo kasi ya ujenzi inasuasua.
Alisema kutokana na kasi ya Serikali uboreshaji wa huduma za afya ujenzi wa vituo hivyo utasaidia kupunguza kasi ya maambukii ya virusi vya ugonjwa huo kwa wasafiri wanaotumia barabara hizo.
Alisema kupitia fedha hizo pamoja na kukamilisha ujenzi wa vituo, pia zitawezesha kununua vifaa vya kisasa na kuweka mazingira wezeshi ya kufundisha wataalamu 10 kila kituo watapata mafunzo.
Alisema lengo la kuwafundisha wataalamu hao, ni kuondoa usumbufu wa uhaba wa wahudumu katika vituo ili wateja watakapofika wapate huduma kwa wakati.
Alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuthibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS ) kuangalia uwezekano wa kuanzisha mpango wa ujenzi wa vituo kama hivyo maeneo ya mipakani.
Alisema ili vituo lazima viweze endelevu na kutoa huduma zake kwa kipindi kirefu zaidi ni vizuri suala la utunzaji na usimamiazi wa miundombinu.
Katika hatua nyingine,Waziri Mhagama aliahidi kuanzisha ujenzi wa chumba cha upasuaji na chumba cha uzazi kituo cha afya Ipogolo na yeye atachangia mifuko 100 ya saruji na bati 100 kama sehemu ya kuunga mkono.
” Ninalazimika kuchangia bati na saruji ili kuanza ujenzi wa chumba cha upasuaji na chumba cha uzazi, nimefurahi kukutana na Rosemary Mwenda ambae leo amepata mtoto katika kituo hiki tena mtoto wa kike ambae nimempa jina la Jenista,mimi ni mama yake wa hiari baada ya mzazi wake kufikisha ombi la kujengewa vyumba,”alisema.
Kuhusu kasi ya mambukizi ya virusi wa vya Ukimwi (VVU) mikoa ya Njombe , Iringa na Mbeya, Mhagama alisema inatisha na kuna haja ya mikoa hiyo kuweka mkakati wa kupunguza kasi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema mkoa huo umepatiwa vituo vinne Wilaya ya Kilolo,kimoja na Iringa vituo vitatu ambavyo vitasaidia kupunguza kasi ya maambukizi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS,Dk. Leonard Maboko alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinakabiliwa na kiwango kikubwa na tatizo la ugonjwa huo,huku takwimu zikionyesha watu takribani milioni 37.9 wanaishi na maambukizi ya VVU mwishoni mwaka 2018 duniani , kati ya hao asilimia 53 wapo nchi za mashariki na kusini mwa Afrika .