Utamu fainali Kilimanjaro Queens Vs Kenya uko hapa

0
1230

MOHAMED KASSARA – DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Wanawake Bara, Kilimanjaro Queens,  leo kitashuka dimbani kusaka taji la tatu la michuano ya Chalenji ya Baraza la Soka Ukanda wa Afrika Mashariki (Cecafa) dhidi ya Kenya, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kilimanjaro itakuwa ikisaka ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo, baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2016 na 2018.

Timu hiyo ilifika  hatua ya fainali, baada ya kuichapa Uganda bao 1-0, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa juzi kwenye uwanja huo.

Kenya ilitinga hatua hiyo baada ya kuifumua Burundi mabao 5-0, katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyochezwa kwenye uwanja huo.

Fainali hiyo itazikutanisha timu zilizomaliza hatua ya makundi, zikiwa vinara wa makundi yao, ambapo Kilimanjaro iliyokuwa kundi A, ilimaliza na pointi zake tisa, baada ya kuzifunga Sudan Kusini mabao 9-0, Zanzibar mabao 7-0 na Burundi mabao 4-0.

Kenya kwa upande wake ilikuwa kundi B, ambapo ilichomoza kinara wa kundi hilo, baada ya kuzichapa Djibout mabao 12-0, Uganda mabao 3-0 na Ethiopia mabao 2-0.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani kwa pande zote mbili, kulingana na historia ya timu hizo zinazokutana.

Mbali na ubora wa timu hizo, zifuatazo ni rekodi zitakazochagiza utamu wa mchezo huo wa kukata na shoka.

Fainali ya kisasi

Licha ya mchezo huo kuzikutanisha timu ambazo zinafahamiana vizuri kutokana na ukaribu uliopo baina yao, lakini Kenya itaingia uwanjani ikihitaji kushinda ili kulipa kisasi dhidi ya Kilimanjaro.

Huo utakuwa mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo katika hatua hiyo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 na Kenya kulambishwa mabao 2-1, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Ufundi jijini Jinja Uganda.

Kenya itakuwa na kazi mbili katika mchezo huo, kwanza kulipa kisasi  cha kupoteza fainali ya Uganda, lakini kuandika historia ya kutwaa taji hilo kwa mara kwanza.

Hata hivyo, kazi hiyo haitakuwa nyepesi kwani Kilimanjaro chini ya Kocha wake mkuu, Bakari Shime imedhamiria kubakisha taji hilo Tanzania, ikijivunia kucheza nyuma ya mashabiki wake.

Shime anakibarua kizito cha kutwaa taji hilo, ilikuendeleza rekodi nzuri alizoweka mtangulizi wake, Sebastian Nkoma aliyetwaa taji hilo mara mbili katika nchi mbili tofauti, akifanya hivyo Uganda mwaka 2016 na Rwanda mwaka jana.

Safu za ushambuliaji moto

Mechi hiyo kweli ina hadhi ya fainali kutokana na viwango vilivyooneshwa na timu hizo mbili,  kuanzia hatua ya makundi hadi fainali.

Ukizubaa katika mchezo huo, basi usishangae ukapigwa kipigo cha aibu kwa kuwa timu zote zina safu kali za ushambuliaji.

Kilimanjaro imefunga mabao 22 hadi hatua hiyo, huku Kenya ikicheka na nyavu mara 22.

Timu zote hazijaruhusu nyavu zao kuguswa hadi sasa, hivyo utaona ugumu wa mchezo huo uliopo, hivyo mechi hiyo itaamuliwa kutegemeana na umakini wa safu za ulinzi.

Mbinu za nani bora?
Mbali na mpambano wa kitakwimu uliopo baina timu hizo, lakini bado mbinu za makocha wa timu hizo Shime na David Ouma zinategemewa kwa kiasi kikubwa kuamua ubingwa wa michuano hiyo.

Makocha hao, kila mmoja ana kazi nzito ya kuhakikisha anachanga vema karata zake, ili kuipa timu yake mbinu bora za kummaliza mpinzani wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here