30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

MFUMO WA GESI MAJUMBANI WAZINDULIWA DAR

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amezindua matumizi ya gesi asilia majumbani na kwenye magari.

Mradi huo wa matumizi ya gesi uliogharimu Sh trilioni 1.2, ulizinduliwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuwasha mitambo yake katika kituo cha Ubungo, jijini Dar es Salaam jana.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema gesi hiyo itauzwa kwa gharama nafuu tofauti na ile ya sasa iliyopo kwenye mitungi.

Alisema gharama za gesi hiyo tofauti yake ni asilimia 40 ukilinganisha na gharama ya mtungi wa gesi kutoja nje ambao ni  kati ya Sh 50,000 na 60,000 kwa sasa.

Alisema zaidi ya wananchi 1,000 wa awali tayari wameanza kutumia gesi hiyo baada ya kuunganishiwa.

Alisema tayari wamefungulia gesi kutoka bomba kubwa linalotoka Madimba, mkoani Mtwara kuingia kwenye bomba dogo ambalo litasambaza gesi majumbani jijini Dar es Salaam.

“Maeneo  ya awali ya mradi wa usambazaji wa  gesi asilia majumbani, jijini Dar es Salaam, wanufaika wake ni wakazi wa Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Survey, Makongo juu, Samnujoma, Shekilango , Sinza  , Mikocheni Cocacola na  Mwenge,” alisema Dk. Kalemani.

Kalemani alisema hatua ya pili itahusisha Mwenge, Tegeta  hadi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo usambazaji  umeenda sambamba na usambazaji wa gesi hiyo majumbani katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambako wananchi 850  wameunganishiwa.

Alisema shughuli zote za usambazaji gesi asilia majumbani itafanywa na Kampuni ya Ges Co ambayo itakuwa na dhamana ya kusambaza gesi hiyo kama ilivyo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Majisafi na Majitaka(DAWASA) na  mengineyo.

“ Tumejiwekea mkakati kuhakikisha miundombinu ya usambazaji gesi ya majumbani inawafikia watanzania wote na kwamba kasi ya usambazaji miundombinu hiyo ni kubwa,” alisema

Waziri huyo alisema gesi hiyo ya majumbani ina ujazo wa futi trilioni 57.4 ambapo serikali  imeyagawa katika sehemu tatu ambazo ni uzalishaji, matumizi ya majumbani  na viwandani.

“Katika  uzalishaji umeme tuna mradi wa umeme wa Kinyerezi II ambao  unagharimu  sh. trioni 8.8, Kinyerezi III  utazalisha Megawati 300 na Kinyerezi IV utazalisha Megawati 330,”alisema Kalemani.

Alisema kwa matumizi ya viwanda Petrol Chemicals serikali ilitenga Sh trilioni  4.6  ambapo viwanda 37  kati ya 41 vitanufaika.

“Kwa mradi huu wa usambazaji gesi asilia majumbani   na katika magari  zimetengwa sh.trilioni 1.2,”alisema Kalemani.

Kalemani alisema  kuanza kutumika kwa gesi hiyo majumbani   kutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na matumizi ya mkaa ambapo asilimia 90 ya wananchi  wa Mkoa wa Dares salaam wanatumia mkaa.

Awali akitoa taarifa kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba , alisema wamejipanga kuweka bomba lingine la gesi ambalo litaanzia Mwenge mpaka Tegeta kwenda Bagamoyo ambayo thamani yake ni Sh bilioni nne.

Alisema bomba lingine litasambaza gesi asilia katika  eneo la Keko Gerezani na Mbagala ili wakazi wa maeneo hayo waweze kufaidika na rasilimali yao.

Kimu Mkurugenzi huyo wa TPDC alisema bomba lingine litajengwa Kusini Magharibi ya Ubungo ambalo  litasambaza gesi eneo la Tabata mpaka Kimara.

Alisema kuwashwa kwa mitambo hiyo ya gesi majumbani itaunganishwa pia na viwanda viwili vya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kisare Makori alipongeza hatua hiyo ya serikali kuanza usambazaji wa gesi hiyo majumbani na kusema itasaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa nishati.

Hata hivyo wakati TPDC wakiwasha mitambo hiyo na kuanza matumizi, baadhi ya wananchi walijitokeza katika eneo hilo wakidai fidia ya mali zao pamoja na nyumba kwa madai hawajalipwa chochote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles