23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mfanyabiashara akata Rufaa kupinga uamuzi wakupokonywa gari

Kulwa Mzee, Dar es Salaam

Mfanyabiashara Hassani Kibona anahofia kupoteza gari aina ya Scania analodai ni mali yake, hivyo amekata rufaa Mahakama ya Rufaa Mbeya akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu unaomtaka kukabidhi gari hilo kwa mjibu rufani akidai gari hilo mali yake lilibadilishwa umiliki bila ridhaa yake.

Kesi hiyo ya madai ilifunguliwa na msimamizi wa mirathi Amanyisye Kamwela dhidi ya Kibona akidai gari aina ya Scania yenye namba T260 BQC ni mali ya marehemu kaka yake Gideon Asumwishe.

Katika uamuzi wa Mahakama Kuu mbele ya Jaji John Utamwa, mahakama iliona Mahakama ya Mwanzo Tunduma, Wilaya ya Momba iliamua sahihi kwamba Kibona akabidhi gari hilo kwa mjibu rufani.

Jaji Utamwa katika hukumu anasema hakukuwa na ushahidi kwamba marehemu alighushi nyaraka akajimilikisha gari hilo japo inaonesha kwamba mmiliki wa kwanza wa gari hilo ni Kibona.

Mahakama hiyo ilisema Mahakama ya Wilaya Momba ilikosea kuamua kwamba gari hilo liuzwe mdai na mdaiwa wagawane fedha nusu kwa nusu.

Katika uamuzi wa Mahakama hiyo ya Wilaya, Hakimu Mkazi D. Magezi alisema mrufani Kibona alikuwa mzembe kufatilia gari hilo tangu mwaka 2015 .

Anasema mrufani na marehemu anayedaiwa aliachiwa gari hilo na Kibona walikuwa marafiki wa karibu na kwamba katika ushahidi inaonesha kuna viashiria vya kughushi.

“Hakuna nyaraka kutoka TRA ya kuonesha kuhamisha umiliki kutoka kwa Kibona kwenda kwa marehemu Gideon.

Mahakama hiyo ya Wilaya Novemba 2018 iliamua gari hilo liuzwe, mdai na mdaiwa wagawane fedha nusu kwa nusu uamuzi ambao Kibona hakukubaliana nao ndipo akakata rufaa Mahakama Kuu ambapo pia alishindwa na kuamuliwa kumwachia gari mjibu rufani.

Kibona amekatia rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Februari 16 mwaka huu mbele ya Jaji John Utamwa.

Kibona anadai alinunua gari hilo Zambia kwa ajili ya kubeba mizigo na Februari 12 mwaka 2011 alilisajili kwa namba T260 BQC akashangaa kuona umiliki umebadilishwa na kumpa mmiliki mwingine ambaye ni marehemu Gideon bila makubaliano.

Machi 11 mwaka huu alimwandikia barua Kamishna wa kodi kulalamikia hilo na Machi 12 TRA ilitoa maelekezo TRA Samora kwa barua AC.317/427/01A/24.

Meneja Mkoa wa Kodi Ilala alielekeza TRA Samora kushughulikia suala hilo kwani umiliki unaonesha ulibadilishwa katika ofisi hiyo na kwamba nyaraka ziwasilishwe kwa Kamishna wa Kodi za Ndani ndani ya siku saba kuanzia Machi 12 mwaka huu.

Aprili 24 mwaka huu TRA ilimwandikia barua Kibona yenye kumbukumbu namba AC.317/427/01A/24 ikieleza kwamba kutokana na kumbukumbu zilizopo umiliki ulihamishwa kutoka kwa Hassan Kibona kwenda kwa Gideon Machi 3 mwaka 2015 katika ofisi ya TRA Samora.

“Tumefanya jitihada kubwa kuzitafuta nyaraka zilizotumika kuhamisha umiliki na bado tunaendelea na jitihada hizo kwa kuzingatia uhamishaji huo ulifanyika muda mrefu, miaka sita iliyopita,”ilisema sehemu ya barua hiyo iliyotoka TRA kwenda kwa Kibona iliyoandikwa na kusainiwa na Matem Edward, Msimamizi wa Kituo cha Kituo Usajili wa Magari, Samora.
Rufaa iliyowasilishwa Mahakama ya Rufaa Mbeya itatajwa Juni mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles