24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Meneja Barclays adai Aveva alikuwa mteja wake

KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MENEJA wa Benki ya Barclays tawi la Mikocheni, Prisca Daudi (39) amedai aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva alikuwa mteja wake na aliwahi kuingiziwa Dola za Marekani 300,000 na Klabu ya Simba wakionyesha kwamba walikuwa wakilipa deni.

Daudi alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakiongozwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai.

Shahidi amedai Aveva alifungua akaunti mwaka 2014 alipeleka barua na picha kutoka kwa mwajiri wake Klabu ya Simba.

Anadai Machi 16 mwaka 2016 katika akaunti ya Aveva ziliingia Dola za Marekani 300,000 ikionyesha ni malipo ya deni, yalikuwa yakilipwa na Klabu ya Simba, fedha hizo zilitoka benki ya CRDB.

Shahidi anadai Aprili 14 mwaka 2016, Aveva alihamisha Dola za Marekani 62,183 kutoka kwenye akaunti yake kwenda kwenye akaunti ya Kampuni ya China kwa ajili ya kulipia nyasi bandia.

“Deni la nyasi bandia lilikuwa Dola za Marekani 109,499 , walilipa Dola za Marekani 32,316 , deni lililobakia lilikuwa Dola za Marekani 77,183 ambapo Aveva alilipa Dola za Marekani 62,183,” alidai.

Shahidi alidai hajui kwanini hakulipa deni lote lililobakia sababu benki hawawezi kuhoji hilo.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 jijini Dar es Salaam, Aveva na Kaburu walifanya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuandaa hati ya kuhamisha Dola za Marekani 300,000 kutoka akaunti ya Klabu ya Simba benki ya CRDB tawi la Azikiwe kwenda akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays tawi la Uhio.

Shtaka la tatu, Machi 15, mwaka 2016 Aveva na Kaburu, wote kwa pamoja walighushi fomu ya kuhamisha fedha ya tarehe hiyo wakionyesha kwamba Klabu ya Simba inalipa deni la Dola za Marekani 300,000 kwa Rais wake Aveva.

Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa Machi 15, mwaka 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe lililopo Ilala, jijini Dar es Salaam, Aveva aliwasilisha fomu ya kuhamisha fedha zilizoghushiwa ya terehe hiyo akinyesha kwamba Klabu ya Simba imeomba kuhamisha Dola za Marekani 300,000 huku akijua sio kweli.

Katika shtaka la tano, ilidaiwa kuwa kati ya Machi 10, 2016 jijini Dar es Salaam, Aveva alijilipa na kutakatisha Dola za Marekani 187,817 kutoka benki ya Barclays tawi la Uhio, huku akijua zimetokana na kughushi.

Shtaka la sita, kati ya Machi 10 na 16, 2016 Kaburu alitakatisha fedha baada mshtakiwa huyo wa pili kumsaidia Aveva kupata Dola za Marekani 187,817.

Katika shtaka la saba, kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016, jijini Dar es Salaam, Aveva, Kaburu na Poppe walighushi hati ya malipo wakidai wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua si kweli.

Ilidaiwa katika shtaka la nane kuwa, kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016 kwa makusudi alionnyesha nyaraka za kughushi kwa Levison Kasulwa akionyesha kuwa klabu hiyo imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited huku akijua si kweli.

Katika shtaka la tisa, inadaiwa kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 jijini Dar Es Salaam, Aveva, Kaburu na Poppe, walitoa maelezo ya uongo na kuwasilisha nyaraka za kughushi wakionyesha kuwa Klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua si kweli.

Poppe anayekabiliwa na mashtaka ya kughushi yuko nje kwa dhamana wakati Aveva na Kaburu wako mahabusu baada ya kukabiliwa na mashtaka ya kutakatisha fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles