27.8 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Membe achukua fomu aja na mambo matatu

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

MSHAURI wa Chama cha ACT Wazalendo, Benard Membe naye amechukua fomu ya kugombea kugombea  urais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo huku akiwa na mgombea mwenza  Dk.Omary Fakhi Mohammed.

Membe ambaye alifukuzwa uanachama na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kukiuka maadili ya chama hicho alijiunga na chama cha ACT Wazalendo ambapo chama hicho kimempitisha kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mgombea huyo alifika katika ofisi za NEC jana, Dodoma saa 4.47 asubuhi akiwa na Mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho Visiwani Zanzibar, Maalim  Seif Sharif Hamad pamoja na baadhi ya wanachama wa chama hicho.

Wakati Membe na timu yake wakifika katika Ofisi za NEC, Chama cha UPDP ndicho kilichokuwa kikichukua fomu na kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na NEC chama ACT Wazalendo  hakikuwepo katika ratiba ya kuchukua fomu jana.

Kutokana na ACT Wazalendo  kutokuwepo katika ratiba ya siku ya jana ambapo ilionesha kwamba chama hicho kitachukua fomu leo, ilibidi viongozi wa chama hicho  na wale wa Tume kukaa kikao kwa  saa kadhaa ili kujadiliana ambapo baadae NEC ilitoa nafasi kwa chama hicho kuchukua fomu saa 6.30 mchana.

MEMBE NA MAMBO MATATU

Ilipofika saa 6.30 Membe na timu yake waliruhusiwa kuingia  ofisi za NEC  kuchukua fomu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuchukua fomu Membe alitaja mambo matatu yaliyomsukuma kugombea urais.

“Tunashukuru sana kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya kazi yake vyema na hivi sasa ninavyozungumza nina begi kubwa la fomu ambazo tunaenda kuzijaza,”alisema.

Alisema baada ya zoezi la kuchukua fomu kukamilika jambo la kwanza linalofuata ni kutafuta wadhamini na alisema hana shaka hata kidogo kwamba atawapata katika mikoa 10 nchini kama inavyoelekezwa.

“Jambo linalofuata sasa ni mchakato wa kuwapata wadhamini kwa mikoa 10 kama tulivyoelekezwa,” alisema.

NIPO ‘FITI’ KIAFYA

Alisema jambo la pili ni kwamba anawahakikishia watanzania kwamba kiafya yupo vizuri na kwamba ana uhakika atawafikia watanzania wote.

“Nataka niwahakikishie nina afya nzuri na ‘nitatimba’ nchi nzima  mikoa yote kwa ajili ya kutafuta wadhamini na wapo wengi lakini pili kivumbi chenyewe kitakapoanza kuanzia tarehe 26 mwezi huu nina afya nzuri na niwahakikishie watanzania nitawafikia wote,”alisema.

UCHAGUZI WA KISTAARABU

Aidha, Membe alisema kwamba alimsikiliza mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli akisema kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kistaarabu ambapo alidai kwamba na ACT Wazalendo nao watafanya kampeni za kistaarabu katika uchaguzi huo.

“Nimemsika mgombea mwenzetu jana (juzi) akisema kwamba uchaguzi huu utakuwa wa kistaarabu ACT Wazalendo tunasema hivyo hivyo.Uchaguzi huu tutauendesha kwa ustaarabu mzuri sana,tutakuwa wastaarabu sana,”alisema.

Alisema wao watashindana kwa hoja ili kuwashawishi watanzania kuichagua ACT Wazalendo kuchukua awamu hii ya uongozi.

Alisema kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu chama chake kitashindana kwa hoja na kutatua kero za wananchi.

“Tutakuwa tunaenda na hoja za kuwashawishi Watanzania kuchagua ACT Wazalendo kuchukua awamu hii ya uongozi kutoka kwa Mzee wetu, Magufuli na kuileta kwa Membe ili tuyaweke mambo sawa.

“Kwa ustaarabu mkubwa sana tatakuwa tukipambana kwa hoja tutakuwa tunapambana kwa kero za wananchi na namna za kuzitatua,”alisema.

MATATIZO YA WANANCHI YAMSUKUMA KUGOMBEA URAIS

Vilevile Membe alisema sababu zilizomfanya agombee urais ni kutokana na kukerwa na dhamira yake ya kutaka kutatua matatizo ya watanzania.

“La tatu  ningependa kusema jambo moja kwamba uchaguzi huu ni uchaguzi wa kipee sana Watanzania wanasubiri kwa hamu kupata Rais ambaye ataelekeza na kutatua matatizo.

“Na mimi ni miongoni mwa watu ambacho nataka kusema waziwazi kilichonisukuma kugombea urais ni kukereketwa na dhamira yangu ya kutaka kutatua matatizo ya wananchi.

“Mimi sitakuwa Rais wa wanyonge tu nitakuwa Rais wa watanzania wote na kwa bahati mbaya sasa hivi wameishakuwa mashetani sio matajiri tena nitakuwa Rais wa watanzania wote ili tuweze kuisaidia nchi yetu kiuchumi iendelee na ifaidi kama wanavyofaidi wenzatu,”alisema Membe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,679FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles