27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yaja na mfumo wa kuwasilisha ritani kielektroniki

Rachel Mkundai,  Arusha

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha mfumo wa uwasilishaji ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki (e-Filing System) ukiwa na lengo kurahisisha uwasilishaji wa ritani za kodi na kupunguza gharama kwa upande wa mlipakodi.

Akizindua mfumo huo jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa TRA Dk. Edwin Mhede, alisema mfumo huo mpya utaongeza tija katika usimamizi wa kodi na kuboresha uwasilishaji wa ritani ambapo mlipakodi ataweza kuwasilisha ritani za kodi na kupata hati ya madai kwa ajili ya kufanya malipo bila kutembelea ofisi za TRA.

“Hii itapelekea kuondoa adha ya upotevu wa muda na rasilimali, kwa kuwa mfumo unamuwezesha mlipakodi kuwasilisha ritani za kodi wakati wowote hata siku za jumamosi, jumapili au sikukuu,” alisema Dk Mhede.

Alisema mfumo huu pia unamwezesha mlipakodi kujua taarifa za ritani za kodi zinazotakiwa kuwasilishwa kwa kipindi husika na hivyo kuziwasilisha ndani ya muda stahiki na kuepuka faini ya kuchelewa kuwasilisha ritani hizo.

Dk  Mhede alisema mfumo huo umetengenezwa katika namna ambayo unakumbusha mlipakodi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ritani na kulipa kodi zake stahiki na hivyo kupunguza uwezekano wa kutozwa riba na adhabu zinazotokana na kuchelewa kuwasilisha ritani na kulipa kodi stahiki kwa wakati.

Hali kadhalika kwa mujibu wa Dk Mhede mfumo ni kiungo cha kurahisisha mawasiliano baina ya mlipakodi, Mkaguzi wa Hesabu (CAG) na TRA katika majukumu ya kisheria ya kuidhinisha ritani za kodi na kuomba muda wa ziada wa uwasilishaji wa ritani endapo itabidi kufanya hivyo jambo ambalo litapunguza vitendo vya udanganyifu wa kughushi mihuri ya wakaguzi wa mahesabu katika kuidhinisha ritani za walipakodi.

Akizungumza kwa niaba ya washauri wa masuala ya kodi, Mwakilishi wa kampuni ya ushauri wa kodi ya PWC, Pamela Saleh, alisema kuzinduliwa kwa mfumo huu utasaidia kupunguza misongo ya mawazo kwa wawasilishaji wa ritani za kodi kwa kuwa utawawezesha kuwasilisha kwa wakati.

“Mfumo huu wa uwasilishaji ritani za kodi utakuwa mfumo mzuri kwa kuwa utatuondolea stress, yaani msongo wa mawazo kwa kuwa tutawasilisha ritani za kodi wakati wowote na kutuepusha na fani za kuchelewa,” alisema Saleh.

Pamoja na mfumo wa sasa wa uwasilishaji wa ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa njia ya kielektroniki, mfumo huu mpya (e-Filing System) utahusisha ritani za makadirio ya kodi ya mapato kwa watu binafsi, eitani ya makadirio ya kodi ya mapato kwa taasisi, ritani ya kodi ya mapato kwa watu binafsi, ritani ya kodi ya mapato kwa taasisi, ritani ya tozo ya mafunzo na maendeleo ya ufundi stadi (Skills Development Levy – SDL) na ritani ya kodi ya zuio katika Mapato ya Waajiriwa (PAYE).

Alisema wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya uchimbaji wa madini, mafuta na gesi wataendelea kuwasilisha ritani zao za kodi ya mapato kwa njia ya kawaida (manual). Pia ritani nyingine ambazo hazijatajwa, zitaendelea kuwasilishwa kwa njia ya kawaida katika ofisi za TRA.

Mfumo huo wa uwasilishaji wa ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki unaambatana na miongozo na mafunzo kwa walipakodi na wadau mbalimbali ili kujenga uwezo wa namna sahihi ya kutumia mfumo huu.

Mamlaka inawasihi walipakodi na wadau wengine kufuatilia kwa karibu miongozo itakayotolewa kwa njia mbalimbali za mawasiliano pamoja na kushiriki mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles