Mbwana Samatta atangulia Nigeria

Mbwana Samatta
Mbwana Samatta
Mbwana Samatta

Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, ametangulia nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho dhidi ya Nigeria ‘The Super Eagles’ utakaochezwa nchini humo Jumamosi hii.

Mchezo huo ni wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2017).

Akizungumza na MTANZANIA jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema mchezaji huyo ameondoka nchini Ubelgiji jana na kwenda moja kwa moja nchini Nigeria.

“Samatta ameshaanza safari ya kuelekea Nigeria na yeye atakuwa wa kwanza kufika kabla ya kikosi cha Stars ambacho kitaondoka mapema kesho (leo),” alisema.

Taifa Stars itavaana na Super Eagles licha ya mchezo huo kuwa wa kukamilisha ratiba baada ya Stars kutolewa na Misri kufuzu kutoka kundi G.

Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Stars, Boniface Mkwasa, amesema  kuwa kikosi chake kipo fiti kutokana na mazoezi waliyoyafanya wakati wakiwa kambini.

Aidha, Mkwasa alisema hadi sasa hajapata taarifa yoyote inayomhusu beki wa timu hiyo, Kelvin Yondani.

“Sina taarifa yoyote kuhusu Yondani na kwakuwa muda wa maandalizi umekamilika, siwezi kumtafuta mbadala wake,” alisema Mkwasa.

Pia amempa pole kipa wake, Deogratius Munishi ‘Dida’, kwa kufiwa na baba yake ambapo nafasi yake imechukuliwa na mlinda mlango wa JKT Ruvu, Said Kipao.

Wachezaji watakaoondoka leo ni Said Kipao, Aishi Manula, Kelvin Yondani, Vicent Andrew, Mwinyi Haji, Mohamed Hussein, Shomari Kapombe, David Mwantika, Himid Mao, Shiza Kichuya,
Ibrahim Jeba na Jonas Mkude.

Wengine ni Mzamiru Yassin, Juma Mahadhi, Farid Mussa, Simon Msuva, Ibrahim Ajib na John Bocco.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here