Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa klabu ya Azam FC, umeanza kuupigia hesabu mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba, unaotarajiwa kuchezwa Septemba 17 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Azam imefanikiwa kushinda mchezo mmoja na kupata sare moja ambapo hadi sasa ina pointi nne.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd, alisema timu nyingi huwa zinaikamia Azam hasa inapokutana na Simba au Yanga, hivyo wao wataanza kujipanga mapema ili kupata pointi tatu muhimu.
“Mchezo huo tunauchukulia wa kawaida kama ilivyo kwa timu nyingine, lakini tunahitaji muda mzuri wa kujiandaa ili tuweze kufanya vizuri,” alisema.
Alisema kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya mwisho ya mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons, unaotarajiwa kupigwa Septemba 7 katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, ambapo baada ya hapo watakutana na Mbeya City kwenye uwanja huo.
Jafar aliongeza kuwa wachezaji wao ambao wapo kwenye timu ya Taifa watawasili nchini Septemba 4, huku siku inayofuata watawafuata wenzao kwa ajili ya mchezo huo.
Alisema Erasto Nyoni ataukosa mchezo huo baada ya kuumia kidole, Paschal Wawa pamoja na Agrey Moris, huenda wakaanza kucheza baada ya kurejea kwenye ligi kwani afya zao zimeimarika.