26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Umuhimu uzazi wa mpango na fikra za wanawake

Mwanamke akichomwa sindano ya uzazi wa mpango.
Mwanamke akichomwa sindano ya uzazi wa mpango.

Na Hamisa Maganga, aliyekuwa Morogoro

UZAZI wa mpango ni uamuzi wa hiari unaofanywa na mtu binafsi, wanandoa au wenzi walio nje ya ndoa ambao hupanga ni lini wapate watoto, idadi wanayoitaka na baada ya

muda gani. Pia huamua ni njia ipi wangependa kutumia.

Wataalamu wa masuala ya uzazi wanasema matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa wanawake

walioolewa ambao wamefikia umri wa kuzaa yameongezeka, lakini ongezeko hilo ni la taratibu.

Matumizi hayo yaliongezeka kutoka asilimia saba mwaka

1991-92 hadi kufikia asilimia 13 mwaka 1996; asilimia 17 mwaka

1999 na asilimia 20 mwaka 2004 hadi 2005.

Wataalamu hao wanasema kiwango hiki ni cha chini mno

ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki na Kusini

mwa Afrika.

Aidha, tafiti za Hali ya Afya na Uzazi (TDHS), zinaonyesha kuwa asilimia sita tu ya wanawake ndio wanaotumia njia za asili za uzazi wa mpango.

Utafiti huo unasema kuwa wakati mwingine kutopatikana kwa njia hizo wakati wote zinapotakiwa huwavunja moyo watumiaji.

Kwa upande wa watumiaji, wasiwasi juu ya kupata madhara, upinzani wa njia hizo na kupendelea kuzaa watoto wengi ni baadhi ya sababu zinazotajwa za kutotumia njia za uzazi wa mpango.

Utafiti wa TDHS mwaka 2004-2005 pia ulibaini viwango mbalimbali vya matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi.

Ulibainisha kuwa kiwango cha matumizi ni asilimia 30 katika Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na

Manyara. Na asilimia 11 tu katika Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Tabora, Shinyanga na Kigoma.

NJIA ZA UZAZI WA MPANGO

Kuna njia nyingi za kupanga uzazi kwa wanawake na nyingine ni kwa ajili ya wanaume.
Kwa ujumla kuna njia za aina mbili, ambazo ni barrier (vizuizi) na hormonal (dawa).
Tofauti iliyopo ni jinsi zinavyofanya kazi. Vizuizi huzuia yai na mbegu zisikutane kabisa au kuzuia mimba isitunge bila kutumia dawa yoyote. Hapa mhusika anaweza kutumia kondomu, kitanzi kisicho na dawa na njia za asili kama kuhesabu siku.

Njia hizi ni nzuri kwa kuwa hakuna kemikali yoyote inayoingia mwilini wala homoni hazibadilishwi ili kuzuia mimba.
Njia za dawa au hormonies, ni zile zinazobalidisha homoni za mwanamke au mwanamume kwa lengo la kuzuia mimba kutungwa na hivyo kutumia aina fulani ya dawa.

Mara nyingi huwa zinafanya kazi kwa kuudanganya mwili juu ya kinachoendelea au kuzuia mayai yasipevuke au kuzuia mazingira ya mimba kupandikizwa.
Wataalamu wanashauri kuwa iwapo mtu ana mpango wa kuanza kupanga uzazi, ni vema akaonana nao kwa ajili ya kupata ushauri.

Akizungumza katika semina ya ya waandishi wa habari kuhusu masuala ya idadi ya watu, afya na uzazi wa mpango, iliyodhaminiwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya Pathfinder, Mshauri wa masuala ya uzazi kutoka Hospitali ya Marie Stopes, Dk. Dismas Damian, anazitaja njia hizo na faida zake.

Kumwaga manii nje

Dk. Damian anasema kuwa hapa mwanamume humlazimu kutoa uume wake kutoka kwenye uke kabla ya kumwaga manii.
Anasema njia hii ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 72.

“Hii njia haina madhara yoyote bali humsaidia mwanamume kuujua zaidi mwili wake na anakuwa mshiriki mzuri katika kupanga uzazi,” anasema Dk. Damian huku akieleza ubaya wa njia hiyo kuwa ni vigumu kutambua mara zote muda wa kutaka kutoa manii.

Anasema kitendo cha kumwaga manii nje wakati mwingine mbegu hupita taratibu bila mwanamume kutambua.

“Lakini pia mwanamke hana msaada wowote katika kutumia njia hii hivyo humtegemea zaidi mwanamume katika kuzuia mimba,” anasema.

Aidha, inasemekana kuwa kati ya wanawake 100 ambao wenza wao hutumia njia hii, 27 wanapata mimba kila mwaka kama hawatumii kwa usahihi.

Kuhesabu siku

Dk. Damian anasema kuwa njia ya kutumia kalenda au kuhesabu siku ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 76.

Anasema katika njia hii, wahusika huamua kufanya mapenzi kutegemea siku za mzunguko wa hedhi ‘ovulation’ wa mwanamke kwa kutokutana siku za hatari.

“Yai la mwanamke linapevuka (ovulate) kuanzia siku ya 10-18 tangu kuanza kwa hedhi yake.
“Hesabu yake si ngumu kwa mtu mwenye siku zinazoeleweka, labda kama mzunguko wa mwanamke ni siku 32 kila mwezi na haibadiliki, basi ni rahisi kuifuata njia hii.

“Kama siku zako hazibadiliki badiliki, unatakiwa uzigawe kwa tatu kuanzia siku ya kwanza ya hedhi. Tukitumia mfano wa siku 32 gawanya kwa tatu ni siku 10 kasoro mbili.

“Kwa hiyo, toka siku ya kwanza ya hedhi hadi ya 10 ni salama. Siku ya 11 hadi ya 22 ni hatari,” anaelezea na kuongeza kuwa siku ya 23 hadi 32 ni salama pia.

Anasema kama siku zinabadilika badilika, mwanamke anatakiwa kuhesabu siku ya kwanza ya hedhi hadi ya 10 ni salama, halafu siku 10 zinazofuata ni hatari, huku siku zilizobaki hadi hedhi inayofuata zinakuwa salama.

Kondomu

Akizungumzia njia hii ambayo ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 86, anasema pia huzuia

maambukizi ya magonjwa ya ngono ikiwamo Ukimwi.
Vidonge

“Vidonge huwa na dawa ambazo zina vichocheo vinavyozuia yai kutoka kwenye ‘ovary’ (ogani inayozalisha mayai ya mwanamke).

“Kwa kutumia njia hii, mwanamke anakuwa na uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 95,” anasema.

Anasema moja ya faida ya vidonge ni kufanya mzunguko wa hedhi kuwa unaoeleweka na kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya ‘ovary’ pamoja na maradhi ya shingo ya kizazi.

Anataja faida nyingine kuwa ni kupunguza maumivu ya tumbo na wingi wa damu ya hedhi na hata kupunguza chunusi.

Sindano

Dk. Damian anabainisha kuwa njia hii ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99.

Anasema sindano huwa na dawa ambazo zina vichocheo vinavyozuia yai kutoka kwenye ogani inayozalisha mayai ya mwanamke.

“Wanawake wengi hupenda kutumia sindano katika kupanga uzazi ukilinganisha na njia nyingine.

“Katika wanawake 100 wanaochoma sindano kwa ajili ya kujikinga na mimba, mmoja tu ndio anaweza asifanikiwe,” anasema Dk. Damian.

Anasema kuwa njia hii haina madhara bali inaweza kugandisha damu kama ilivyo kwa dawa nyingine za kuzuia mimba au kwa wajawazito.

“Huweza kusababisha kichefuchefu, kupata hamu ya kula, kunenepa au kukonda na kichwa kuuma.

“Wakati mwingine inaweza kusababisha kuvurugika kwa hedhi au kupotea kabisa katika kipindi cha miezi ya mwanzo,” anasema.

Vijiti (vipandikizi)

Hivi ni vijiti vyembamba vidogo vinavyowekwa kwenye sehemu ya juu ya mkono wa mwanamke kwa njia ya upasuaji mdogo, ambapo vina kichocheo kinachozuia kupevuka kwa yai.
Dk. Damian anasema kuwa kama ilivyo kwa sindano, kijiti pia kina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99.

Anasema husaidia kuzuia mimba kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano tangu kupandikizwa.

“Kwa kutumia njia hii katika kupanga uzazi, mwanamke anaweza kuharibu mzunguko wake wa hedhi na kunyonyoka nywele,” anasema.

Kitanzi

Hiki ni kitu kidogo kilichotengenezwa kwa aina maalumu ya plastiki ambacho huwekwa kwa utaalamu ndani ya mfuko wa uzazi. Kinaweza kufanya kazi hadi miaka 10.

“Kitanzi kina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99, lakini ubaya wake ni kwamba kinasababisha ongezeko la damu ya hedhi na kuumwa tumbo.

“Wenza ni lazima wawe wametulia pindi wanapoamua kutumia njia hii kwa kuwa kina tabia ya kudaka maradhi,” anasema na kuwashauri wahusika kutoitumia kama wanadhani bado wanajihusisha na ngono zembe.

Kufunga kizazi

Ni upasuaji wa kuziba mirija ya kupitisha mayai (kwa mwanamke) au kupita mbegu (kwa mwanamume).

Dk. Damian anasema kuwa wahusika wanapaswa kuwa na uhakika na uamuzi wao kwa sababu ukishafanya hakuna kurudi nyuma.

Vidonge vya dharura

Vidonge hivi kitaalamu huitwa The morning after pill. Mara nyingi hutumiwa pale mwanamke anapofanya tendo la ndoa katika siku za hatari bila kutumia kinga yoyote dhidi ya mimba.

Husaidia kuzuia mimba iwapo vikinywewa ndani ya saa 72 baada ya kufanya ngono zembe. Dk. Damian anasema kuwa unavyozidi kuchelewa kuvinywa ndio uwezekano wa kufanya kazi unapopungua kwa kuwa havitatoa mimba iliyokwishatungwa.
Anasema vidonge hivi mara nyingi hutumiwa na watu waliobakwa. 

JE, KIJANA CHINI YA MIAKA 18 ANAWEZA KUTUMIA?

Dk. Damian anasema kuwa vijana chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kupata bidhaa za uzazi wa mpango bila ruhusa kutoka kwa wazazi wao.

Anasema uzazi wa mpango na huduma zingine za afya ya uzazi ni siri hivyo wafanyakazi wa vituo vya afya hawatakiwi kutoa taarifa za mgonjwa kwa mtu yeyote bila ruhusa ya mgonjwa mwenyewe.

Anasema pamoja na kupewa huduma ya kinga dhidi ya mimba, pia wanaweza kupimwa ujauzito, magonjwa ya zinaa na ukaguzi wa ukeni.

“Lakini hata kama ni siri ni vizuri waongee na wazazi wao au walezi ili kupata ushauri na kuwasaidia kufanya uamuzi bora wa kuanza kufanya mapenzi na njia za kinga watakazotumia dhidi ya mimba na magonjwa ya zinaa,” anasema.

Anasema kwa kawaida wanawake kuanzia miaka 15 hadi 49 wanao uwezo wa kushika ujauzito. Hivyo, hata vijana walio chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kutumia njia za uzazi wa mpango bila kificho.

Anasema ni muhimu kwa vijana wa umri huo kutumia njia za uzazi wa mpango kwa kuwa wengi hubeba ujauzito pasipo kutarajia.

Anasema utafiti uliofanywa mwaka huu unaonyesha kuwa asilimia 25 ya vijana chini ya umri wa miaka 18 waliopo vijijini tayari wanaitwa mama ikilinganishwa na mjini ambapo ni asilimia 14.

“Asilimia 6.4 waliopo vijijini tayari wana ujauzito wakati mjini ni asilimia 4.5. Asilimia 31.5 ya watoto wa vijijini tayari wamewahi kulea ikilinganishwa na mjini ambako ni asilimia 18.6,” anasema Dk. Damian na kuongeza kuwa utafiti umebaini kuwa robo ya watoto kuanzia miaka 15 hadi 19 walikuwa wanalea.

WANAWAKE WANAVYOZUNGUMZIA NJIA HIZI

Takwimu za mwaka 2015/2016 zinaonyesha kuwa asilimia 25.7 wanawake hawakuhitaji kutumia dawa za uzazi wa mpango.

Dk. Damian anasema kuwa asilimia 22.1 wanahitaji kutumia njia hizo; asilimia 42.2 wangependa kusubiri zaidi ya miaka miwili ili kuweza kupata watoto wengine wakati asilimia nne hawaelewi hitaji lao.

Anasema kuwa wengi wao wanapenda kuwapa nafasi watoto wao zaidi ya miaka miwili lakini wanaogopa kutumia uzazi wa mpango.

Hata hivyo, uelewa kwa wanawake unaonekana bado ni mdogo ambapo wengi wao wamekuwa hawajui ni muda gani wanapaswa kusubiri baada ya kuacha kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ili waweze kupata ujauzito mwingine.

Suala hili limekuwa likimsumbua Pili Said, ambaye alikuwa akitumia dawa za uzazi wa mpango lakini sasa hivi amekuwa na wakati mgumu katika kubeba ujauzito.

Pili anasema kuwa aliacha kutumia vidonge vya kupanga uzazi tangu mwaka jana ambapo aliamua kubeba mimba nyingine bila ya mafanikio.

“Nilishaacha kutumia hivyo vidonge, hapa unavyoniona nina watoto wawili, mume wangu anahitaji kuongeza mtoto lakini inashindikana, kila siku nahangaika kwa madaktari bingwa lakini hamna kitu,” anasema Pili.

Naye Lightness Mkinga anasema huwa anaogopa kutumia njia za uzazi wa mpango kwa kuhofia kupata madhara hapo baadaye.

“Kuna watu wanatumia vijiti lakini wanasema kuwa wakati mwingine huwa vinatembea mwilini na baadaye husababisha maradhi kama saratani.

“Wale wanaotumia kitanzi nao wananiambia kuwa kwanza hukaa muda mrefu takribani miaka 10 na kwamba katika miaka yote hiyo unapofanya mapenzi ni lazima utumie mtindo mmoja wa kulala chali (kifo cha mende),” anasema Lighteness na kuongeza kuwa ukibadilisha ‘style’ kinafyatuka.

Anasema kwa sababu hiyo, amekuwa akiogopa kutumia njia za uzazi wa mpango kwa hofu ya kupata madhara.

Lighteness hajatofautiana na Mashunda Hassan, ambaye anadhani kuwa unapotumia vidonge kupanga uzazi, ikatokea siku umesahau na ukakutana na mwenza wako, ni lazima mimba itungwe.

Mashunda anathibitisha kuwa wapo wanawake ambao waliwahi kupata ujauzito huku wakitumia vidonge.

Akizungumzia njia ya kondomu anasema kuwa ni nzuri lakini wanaume wengi huwa hawaipendi wakidai inapoteza ladha ya mapenzi.

“Mwanzoni mnaweza kutumia kondomu lakini mpaka lini? Wanaume wengi utawasikia yaani mke wangu mwenyewe nimvalie kondomu? Hapo ndipo mtihani unapoanzia,” anasema Mashunda na kuongeza kuwa wanaume wengine ni walevi hivyo huwawia vigumu kukumbuka kinga pindi wanapolewa.

Kwa upande wake Agness Mandwa, anasema kuwa huwa anatumia njia ya kalenda (kuhesabu siku), ambayo ni salama na nzuri kiafya.

“Mimi kwa kweli huwa natumia  kalenda na kondomu, hizi ni njia ambazo hazina madhara yoyote kwangu, huwa ninafuatilia kwa makini na sijawahi kupata mimba kwa kufuata njia hii,” anasema. Agness anasema kuwa dawa za vidonge, sindano na vijiti ni nzuri lakini zina madhara makubwa japokuwa madaktari wanasema kuwa ni madogo.

Anasema kuwa sasa hivi wanawake kwa kutumia dawa hizi wengi wananenepeana bila mpango na hivyo kujikuta wakipata madhara kiafya.

“Sasa hivi wanawake wengi wanaongoza kuwa na vitambi kuliko wanaume, wengine wamefunga hedhi.

“Hebu jiulize hiyo damu inatakiwa kutoka lakini haitoki, kwa kweli wataalamu wanasema hakuna madhara lakini mimi binafsi nadhani yapo,” anasema Agness.

Naye Sikujua Hamis anasema kuwa yeye anatumia njia ya kijiti lakini inamtesa maana anatokwa na damu ya hedhi kwa muda wa miezi miwili sasa.

Sikujua ambaye ana mtoto mmoja anasema njia ya kalenda ilimshinda kwa kuwa baada ya kijifungua mzunguko wake wa hedhi ulivurugika kabisa.

Anasema kuwa mume wake hataki kusikia habari ya kutumia kondomu. “Sielewi nifanyeje ili hii hedhi ikome… nimechoka,” anasema Sikujua.

Asumptha Zuberi anasema kuwa yeye anatumia kitanzi mwaka wa nne sasa na hajawahi kupata madhara yoyote.

Anasema siku zake za hedhi anazipata kama kawaida na mwili wake uko vizuri haujawahi kuharibika.

“Mwanzoni kilikuwa kinamgasi mume wangu, nikaenda hospitali kuuliza wakasema ni kawaida huwa inafika wakati kinalainika. “Na kweli, sasa hivi hakimsumbui na tunafanya tendo la ndoa kwa mtindo wowote ule. “Pengine madhara ya hizi njia za uzazi wa mpango yanategemea na mtu mwenyewe, wengine zinawakubali na wengine zinawakataa,” anasema.

Mwanamke mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alihoji kwanini washauri wa masuala ya uzazi na madaktari hawawi wa kweli?

Anasema yeye ana mwaka mmoja tangu alipotoa kijiti na hajawahi kupata hedhi huku akikabiliwa na maumivu ya tumbo ya mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles