26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mbunge CCM atangaza kupisha vijana 2020

Na BENJAMIN MASESE-RORYA

MBUNGE wa Rorya, Lameck Airo (CCM),  amesema licha ya kuchaguliwa kwa kishindo kwa awamu mbili kuongoza jimbo hilo, hatogombea tena katika Uchaguzi Mkuu ujao badala yake atawaachia vijana.

Alisema ingawa hatogombea tena, atatimiza ahadi zake zote alizoahidi wakati wa kampeni za mwaka 2015 na kwamba kazi aliyofanya kwa miaka tisa, itabaki kuwa historia.

Airo ambaye yupo katika ziara jimboni mwake, alisema  tayari amekijulisha chama chake juu ya kusudio lake na kwamba wamekusudia kuwa mchakato wa uchaguzi utakapoanza, watahakikisha Jimbo la Rorya linaongozwa na vijana shupavu na wenye sifa.

Juzi alitembelea vijiji na vitongoji vya Bukama, Nyarombo, Nyamtinga, Busanga, Siko na Rwang’enyi, na kuzungumza na wananchi.

Katika ziara hiyo, alimkabidhi Diwani wa Kata ya Nyamtinga, Chacha Nyambaki (CCM) mabati 200, mifuko ya saruji 100 na Sh milioni moja kumalizia maboma na kuezeka baadhi vyumba vya madarasa katika shule zilizoezuliwa paa kwa upepo.

“Nimeanza ziara katika Kata ya Nyamtinga kwa kutembelea vijiji na vitongoji, ikiwa lengo ni kuona shughuli za maendeleo na pale panapohitaji msaada tutatatua inapowezekana.

“Lakini kama inahitaji kuja na nguvu ya ziara tunapanga, kata hii ndiyo mara zote nimekuwa nikiitolea mfano kwa namna diwani wake anavyowajibika kwa kushirikiana na wananchi kuleta maendeleo.

“Kama mbunge nitahakikisha kwa kipindi kilichobaki cha mwaka mmoja  kabla ya Uchaguzi Mkuu, ahadi zangu zote zinatekelezwa ili atakayerithi nafasi hii, chama kisipate shida kumnadi ifikapo 2020.

“Najua mwezi ujao nchi itakuwa na uchaguzi mdogo, chama na mimi binafsi tunataka tuone  Rorya tunaikabidhi kwa vijana, hivyo nawataka wajiandae.

“Pia kina mama jitokezeni kugombea nafasi mbalimbali, tumechoka kuona sura zile zile miaka yote.

“Wale mnaosubiri kila muda kupewa nafasi za viti maalumu nanyi nendeni mkagombee, hivi sasa tunawapa wale ambao hawajawahi kupata ili nao wapate uzoefu,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Charles Ochele, amethibitisha mbunge huyo kutoa taarifa ya kutogombea tena 2020, huku akisema haitakuwa jambo la kushangaza endapo atabadili mawazo yake siku za mbeleni.

Ochele alisema Airo ni mbunge wa mfano katika jimbo hilo kutokana na maendeleo aliyofanya.

Alisema mbunge huyo amekuwa mtu anayewaondolea wananchi changamoto zilizowakabili kwa muda mrefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,206FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles