NA AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), amefika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kumjulia hali Tundu Lissu aliyelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) tangu Septemba 7, mwaka huu akipatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Nyalandu kupitia akaunti zake, zikiwamo za Facebook na Instagram, jana alisema pamoja na kufika hospitalini hapo mapema, lakini hakuruhusiwa na madaktari kumwona Lissu kwa muda huo.
Nyalandu ambaye ni mbunge wa kwanza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenda kumwona Lissu hospitalini, alisema akiwa bado akisubiri ruhusa ya madaktari ili kumwona pia alifanikiwa kutoa pole kwa mke wa Lissu.
“Nimefika Hospitali ya Nairobi mapema leo (jana) kumjulia hali Lissu. Madaktari wanaendelea kumfanyia matibabu, na bado hatujaruhusiwa kumuona. Kwa niaba ya wana Singida na Watanzania wote, nimetoa salamu za pole kwa mke wake, na bado nasubiri uwezekano wa kuweza kuonana naye usiku wa leo (jana) endapo madaktari wataruhusu,” aliandika Nyalandu.
Katika andiko hilo ambalo Nyalandu aliambatanisha picha aliyopiga akiwa hospitalini hapo na mdogo wake Peter Nyalandu, aliwataka Watanzania kuendelea kumwombea Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki ili Mungu amponye katika nyakati hizi za kujaribiwa kwake.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), aliposti picha katika ukurasa wake wa Facebook akiwa na Nyalandu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari wakiwa nje ya eneo la hospitali hiyo.
Katika picha hiyo, aliandika: “Muelekeo ni muhimu kuliko kasi, wengi hawajui waendako, lakini wanakwenda kwa kasi! Ndiyo maana ni bora nchi moja kwenda kwenye muelekeo sahihi kuliko maili moja kwenda kwenye muelekeo usio sahihi.”