23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

ACACIA YAPUNGUZA WAFANYAKAZI 1,200

Na FREDRICK KATULANDA -MWANZA

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Acacia, imekamilisha hatua za kusitisha shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Bulyanhulu uliopo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kwa kupunguza wafanyakazi wake 1,200, wakandarasi 800 na kubakia na 200 pekee.

Jana jioni uongozi wa mgodi huo uliandaa sherehe kuwaaga wafanyakazi wake waliopunguzwa kazi ikiwa ni hatua ya mwisho ya ufungaji mgodi huo.

Taarifa ya kampuni hiyo iliyotumwa juzi kwa gazeti hili, inaeleza kuwa wamefikia uamuzi wa kufunga mgodi huo kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji mara baada ya zuio la usafirishaji wa mchanga wa madini (Makinikia).

Acacia ilieleza kuwa tangu kuwekwa zuio la usafirishaji wa makinikia nje ya nchi, uzalishaji wa mgodi huo uliathirika kwa asilimia 35 kwa sababu ya kukumbwa na tatizo la ongezeko la hifadhi ya makinikia yenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 265 sawa na Sh bilioni 590.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba mgodi huo utafungwa na kubaki na wafanyakazi wachache ambao watakuwa na jukumu la utunzaji wa mali zote zisizohamishika na mitambo, ili kuwezesha mgodi huo kurejea katika utendaji wa kawaida hapo baadaye pindi zuio la usafirishaji makinikia litakapoondolewa na mazingira ya biashara kutulia.

“Kwa sasa shughuli za uchimbaji wa chini ya ardhi na uchenjuaji wa miamba utasitishwa pamoja na usafishaji wa mashapo ambao umesitishwa kwa muda ili kupisha zoezi la kuhifadhi maji kutokana na hali ya ukame,” ilieleza taarifa ya Acacia.

Ilibainisha kwamba kwa sasa usafishaji wa mashapo uliositishwa unatarajiwa kuendelea Oktoba baada ya mvua za kutosha kunyesha. Watazalisha kwa kiwango cha kati ya wakia 30 hadi 35,000 kwa mwaka huku shughuli za uchimbaji chini ya ardhi zikiendelea kusitishwa.

Ilielezwa kuwa Acacia inaamini kuwa majadiliano kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania yanayoendelea yatakuwa yenye ufumbuzi na kusisitiza kuwa majadiliano hayo ndiyo njia bora zaidi kwa pande zote zinazohusika kumaliza tofauti iliyojitokeza.

 

Wafanyakazi wanena

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini (NUMET), Nicomedes Kajungu, alisema tayari wamekutana na uongozi wa Acacia katika vikao viwili na kukubaliana kupunguzwa kwa wafanyakazi hao kutokana na uongozi wa mgodi huo kuamua kusitisha uzalishaji.

Kajungu alisema kwa sasa wanasubiri kikao kingine kujadiliana namna ya kuwalipa wafanyakazi wake 1,200 ambao watapunguzwa kazi na kuiomba Serikali kumaliza mgogoro wake na Acacia kwa kuwa idadi ya wafanyakazi wanaoathirika ni kubwa na ina athari kwa uchumi na ustawi wa maisha ya kila mmoja.

“Kusitishwa kwa shughuli za mgodi huu, kuna athari kubwa kwani utaathiri mauzo ya saruji ambapo mgodi huo ulikuwa ukilipa Dola za Marekani milioni 40, walikuwa wakilipa dola 25 za gharama za umeme, lakini walikuwa wachangiaji wa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hale kwa asilimia 60 na Halmashauri ya Msalala asilimia 70,”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,226FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles