24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE: WANAOHAMA CHADEMA WAHAME TU

Na WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAKATI kukiwa na wimbi la madiwani wa Mkoa wa Arusha kukihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amesema yeyote anaweza kuondoka ila chama kama taasisi kitabaki imara.

Mbowe alisema hayo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA wiki iliyopita, alipoulizwa kuhusu msimamo wa chama chake juu ya kuhama kwa madiwani hao na kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, aliyoitoa hivi karibuni kuwa mtu mzito kutoka Chadema atajiunga na chama chao.

Wakati Mbowe akisema hayo, jana madiwani watatu kutoka katika jimbo lake la Hai, walitangaza kuondoka Chadema na kujiunga CCM.

Madiwani hao ni Goodluck Kimaro wa Kata ya Machame Mashariki, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Hai, Abdala Chiwili (Kata ya Weruweru) na Erneti Kimati (Kata ya Mnadani).

Wamesema wamehama chama hicho baada ya kuridhishwa na utendaji wa Rais Dk. John Magufuli na kukerwa na kile walichodai kuwa uongozi wa Chadema ngazi ya taifa unaendekeza majungu na kudhalilisha baadhi ya viongozi.

KAULI YA MBOWE

“Kwanza sitaki kuzungumzia propaganda za Polepole, ambaye najua anajifunza siasa, wapo wazito zaidi waliohama ama kufukuzwa, lakini niseme tu chama hiki kina misingi yake, mtu awe mdogo ama mkubwa ni tafsiri tu, ingawa wapo wenye mchango mkubwa.

“Mtu yeyote anaweza kuondoka, lakini Chadema kama taasisi ikabaki imara, mimi kama mwenyekiti ninajua tumejenga taasisi imara ambayo haiwezi kutetereka kwa mwanachama au kiongozi wa ngazi yoyote kuondoka.

“Kimsingi hakuna aliye bora kuliko chama, chama ni kikubwa kuliko mtu yeyote,” alisema Mbowe.

Januari 2014, Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na mshauri wa chama hicho, Dk. Kitila Mkumbo, walifukuzwa uanachama kwa kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013.

Zitto Kabwe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, alifukuzwa uanachama Machi 2015, baada ya kushindwa kesi aliyofungua kuzuia uanachama wake usijadiliwe baada ya kusimamishwa awali na wenzake Mwigamba na Dk. Mkumbo.

Julai 2015, Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho na mgombea urais mwaka 2010, alijiuzulu kwa kile alichosema ni kupinga Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015.

 

MADIWANI KUJIUZULU

Akizungumzia mwenendo wa madiwani wa kata mbalimbali za Mkoa wa Arusha kujizulu, Mbowe alisema hata kabla ya wao kuchukua hatua hiyo, kama chama walishapata taarifa zao juu ya usaliti wao na mipango yao ya kuhama, wakaamua kuwaacha waondoke wenyewe badala ya kuwafukuza.

Hadi sasa takribani madiwani 11 kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambayo ineonekana kuwa ngome ya Chadema, wamejiuzulu nyadhifa zao wakidai kuridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli na kuamua kumuunga mkono.

Mbowe alisema katika mazingira ambayo wabunge, viongozi wakuu wa chama, madiwani na hata wenyeviti wa vijiji wanakamatwa ovyo, si jambo la kushangaza kwa mtu asiye na msimamo kuondoka.

“Kujenga chama cha upinzani ndani ya hali tuliyonayo si kazi rahisi, inahitaji ujasiri, uvumilivu, utayari na kuteseka.

“Lakini ninachoweza kusema ni kwamba madiwani ni wepesi sana kutoka au kufukuzwa katika chama, hii si mara ya kwanza kuhama au kufukuzwa kwa aidha mwanachama au kiongozi, lakini hilo halikuzuia Chadema kukua na kuimarika kama taasisi imara ambayo inawanyima usingizi watawala.

“Kwa kifupi hao madiwani tulikuwa na taarifa zao, tukasubiri wajifukuze wenyewe, tunajua wameahidiwa kulipwa mafao yao ya udiwani, vyeo, wamelipiwa mikopo na mambo mengine mengi.

“Hivi hamshangai wote wanaoondoka hoja yao ni moja, hata hao wanaowafundisha si wawakaririshe neno lingine. Wengine wangesema wanaunga mkono, wengine waseme labda ndani ya Chadema kuna kitu fulani, lakini wote wanakaririshwa kitu kimoja.

“Kwetu sisi tunaona hii ni fursa nyingine kwa wanachama wengine kuchukua nafasi hizo na kuonyesha uwezo wao,” alisema Mbowe.

 LOWASSA NA URAIS

Akizungumzia kauli za baadhi ya watu waliokuwa wakihoji kauli ya Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, kutangaza nia ya kuwania tena urais 2020, alipokuwa nchini Kenya hivi karibuni, Mbowe alisema chama chao kina uhuru na mtu kusema matamanio yake si kosa.

“Hata wewe (mwandishi) kama ni mwanachama wa Chadema na unataka kugombea uenyekiti si dhambi mtu kusema matamanio yake, ili mradi tu apite kwenye taratibu zinazokubalika na baadaye vikao vya chama vitaamua,” alisema Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles