24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe, Matiko kula krismasi mahabusu

Krismasi mahabusu

NA PATRICIA KIMELEMETA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, watasherehekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya gerezani baada ya kufutiwa dhamana zao katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi hao na wengine saba wa chama hicho.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana, viongozi hao wawili waliwatakia wanachama wao heri ya Krismasi na mwaka mpya.

Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa madai kuwa hawana taarifa ya kinachoendelea mahakama ya juu.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi wa kesi hiyo, Faraja Mangula, alidai kuwa mawakili, Peter Kibatala na Sheck Mfinanga, wamepata dharura na kushindwa kufika mahakamani hapo na waliomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 4, mwakani.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Wankyo, alidai suala la kupanga tarehe wanaiachia mahakama hiyo kwa watakayoona inafaa.

Hakimu Mashauri alisema Januari 4, mwakani atakuwa na kazi nyingine hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 3, mwakani.

Baada ya kuelezwa hayo, Mbowe na Matiko, waliwatakia wafuasi wao heri ya Krismasi na mwaka mpya wakiamini kuwa hawawezi kutoka gerezani kwa kipindi hicho.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu. 

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16, mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles