30.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

MBELGIJI KUJIBU MASWALI MATATU YA MASHABIKI SIMBA

NA MASYENENE DAMIAN- MWANZA


KOCHA wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems, leo atafanya mtihani rasmi wa kwanza tangu alipojiunga na timu hiyo itakapoumana na Mtibwa Sugar katika pambano la Ngao ya Jamii litakalopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Aussems ambaye ni raia wa Ubelgiji, alitua Msimbazi kuchukua nafasi ya Pierre Lechantre ambaye aliachana na timu hiyo baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kumalizika.

Aussems tangu alipojiunga na Simba, ameiongoza kucheza michezo minne ya kirafiki, kati ya hiyo akishinda miwili na kutoka sare mbili.

Simba ilicheza michezo mitatu ya kirafiki ilipopiga kambi ya wiki mbili  nchini Uturuki, ikianza kwa kuvuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Mouloudia Oujda ya  Morocco kabla ya kuicharaza mabao 2-1, timu ya Ksaifa ya Palestina.

Baada ya kurejea nchini, ilishuka dimbani Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuumana na Asante Kotoko ya Ghana na kutoka sare ya bao 1-1, huo ulikuwa mchezo wa  siku maalumu ya klabu hiyo ‘Simba day’, ikalazimishwa suluhu na Namungo FC ya mkoani Lindi kabla ya kucheza mchezo mwingine dhidi ya Arusha United na kushinda mabao 2-1.

Aussem licha ya kwamba hajapoteza mchezo wowote zaidi ya sare miongoni mwa mechi nne za kirafiki, lakini ukweli ni kwamba mashabiki wa klabu hiyo wataanza kumfanyia tathmini leo atakapoikabili Mtibwa Sugar leo, ukiwa  ni mchezo wa kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania  Bara.

Mashabiki wa Simba wana sababu tatu  za kuusubiri kwa hamu mchezo wa leo wa Ngao ya Jamii.

Sababu ya kwanza ni kutaka kuona matunda ya usajili wa wachezaji nyota kutoka ndani na nje ya Tanzania, mabadiliko ya benchi la ufundi na kambi ya wiki mbili nchini Uturuki.

Ikumbukwe kuwa uongozi wa Simba  ulijinasibu kuwa unafanya usajili wa wachezaji unaoamini wataisaidia timu yao kutetea ubingwa, lakini kubwa ni kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, ambapo timu hiyo  itaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ndio wakasajili wachezaji bora akiwemo Adam Salamba, aliyefanya vizuri msimu uliopita akiwa na Lipuli ya Iringa pamoja na wageni, mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere kutoka Gor  Mahia ya  Kenya, kiungo raia wa Zambia, Clatous Chama, aliyekuwa anakipiga Ittihad ya Misri na beki Muivory Coast, Pascal Wawa.

Pia ifahamike, Lechantre aliondoka Simba akiiwezesha kutwaa ubingwa, hivyo mashabiki wa klabu hiyo wanataka kuona kitu cha ziada kutoka kwa Aussems.

Kambi ya Uturuki ilionekana kusifiwa na uongozi pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo, ingawa kiwango  kilichoonyeshwa na timu hiyo katika michezo mitatu  ya kirafiki ya nyumbani hakikuwaridhisha baadhi ya mashabiki.

Kwa upande mwingine, Mtibwa Sugar inataka kuonyesha kuwa maandalizi yake ya wiki mbili jijini Dar es Salaam, sambamba na kushiriki michuano ya Reha hayakuwa ya kupoteza muda zaidi ya kutaka matokeo mazuri.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Aussems, alisema anaamini maandalizi yao ya mwezi mmoja   yataanza kutoa matunda staili leo watakapoikabili Mtibwa Sugar.

“Tumefanya maandalizi ya mwezi mmoja, kikosi chetu kiko sawa hatujapoteza mchezo wa maandalizi, nyota wote wa Simba watakuwepo isipokuwa Kapombe (Shomari) na Bocco (John) ambao bado wanaendelea na matibabu, kuwatumia kesho (leo) tutakuwa tumeharakisha.

“Nadhani watakuwa tayari Jumatano ligi itakapoanza, waliosalia wako fiti kucheza mchezo wa kesho,” alisema Aussems.

Naye Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila, alisema kikosi chake kinashuka dimbani leo kikiwa kinajiamini kiasi cha kutosha, kikikusudia kuandika historia mpya ya kutwaa kikosi hicho.

Mgeni rasmi katika mchezo huo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Simba ilipata fursa ya kucheza mchezo   huo baada ya kuibuka mabingwa wa msimu uliopita wa Ligi Kuu, wakati Mtibwa Sugar ilitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho maarufu Azam Cup

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,507FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles