23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

MAZOEZI YANAVYOWEZA KUKUPA FURAHA, NGUVU

Wanawake wakifurahia mazoezi
Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.

MOJA ya faida muhimu za mazoezi ni kutupatia furaha na uwezo wa kufanya kazi kwa nguvu na ufasaha. Tafiti zinaonyesha kwamba watu wanaofanya mazoezi mara kwa mara huwa na furaha na kuwa na uwezo wa kufanya kazi zao kwa haraka na ufasaha. Ni kutokana na sababu hii mazoezi  huweza kutumika kutibu tatizo la sonono na hata lile la msongo wa mawazo.

Ni nini basi kinacho fanya mazoezi kuweza kutupatia faida hizi zote, ambazo ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Leo tutajadili sababu tano za kisayansi na kijamii zinazoelezea uwezo wa mazoezi katika kuleta furaha na nguvu za kufanya kazi katika miili yetu.

Mazoezi huongeza kiwango cha vichocheo vya furaha mwilini

Tafiti zinaonyesha kwamba, mojawapo ya vitu vinavyowafanya watu wenye tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara kuwa wenye furaha ni kutokana na ukweli kwamba mazoezi huongeza kiwango cha vichocheo (hormones) vya furaha mwilini. Vichocheo hivi maarufu kama endorphins huifanya miili yetu kujisikia furaha kitu ambacho ni muhimu kwa utendaji kazi na afya.

Ili kufaidika na hili, hakikisha unafanya mazoezi wakati wa asubuhi ili uwe na furaha siku nzima na uweze kufanya shughuli zako kwa ufasaha.

Mazoezi huongeza kiwango cha homoni ya testosterone mwilini

Homoni ya testosterone maarufu homoni ya kiume, inahusika zaidi katika kuupa mwili nguvu na uwezo wa kufanya kazi na matendo mbalimbali. Ikumbukwe kwamba licha ya homoni hii kujulikana kama homoni ya kiume, wanawake pia hutengeneza homoni hii. Kwa maana hiyo, kazi ya kuupa mwili nguvu inayofanywa na testosterone ni kitu kinachotokea kwa wanaume na wanawake pia. Mazoezi hususani yale ya kusukuma na kunyanyua uzito huweza kuongeza kiasi cha homoni hii mwilini. Kuongezeka kwa kiwango cha homoni hii hutusababisha kuwa wenye nguvu na kutupa uwezo wa kumaliza kazi zetu kwa wakati.

Hakikisha unafanya mazoezi ya kusukuma, kunyanyua au kuvuta uzito (resistance exercise) angalau mara mbili kwa wiki. Kumbuka si lazima kutumia uzito mkubwa na hakikisha unaifanyisha kazi misuli yote mikubwa kama ile ya mapaja, kifua na mikono.

Mazoezi huimarisha nguvu ya mifupa na misuli

Ili mwili uweze kufanya kazi ipasavyo, misuli na mifupa yenye nguvu ni muhimu. Kwa kufanya mazoezi mara kwa mara mifupa na misuli yetu huwa yenye nguvu kitu ambacho hutuwezesha kufanya kazi ipasavyo. Mazoezi yanayoimarisha mifupa na misuli ni pamoja na yale ya kunyanyua na kusukuma uzito.

Mazoezi hutupa fursa ya kujumuika

Kujumuika na ndugu na marafiki ni mojawapo ya njia ya kupata furaha. Kwa mfano, tunaposhiriki katika michezo ambayo ni sehemu ya mazoezi tunapata fursa ya kukutana na ndugu na marafiki. Mikutano hii huongeza furaha kitu ambacho ni muhimu kwa afya zetu.

Hakikisha unajiunga na vilabu vya michezo au mchaka mchaka (jogging clubs) mtaani kwako. Waweza pia kufanya mazoezi kama vile kukimbia au kutembea pamoja na mwenzi wako.

Mazoezi hushusha kiwango cha vichocheo vya msongo wa mawazo (stress hormones)

Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kushusha kiwango cha vichocheo vya msongo wa mawazo au stress hormones. Kiwango cha juu cha vichocheo vya msongo wa mawazo ni muhimu kwa muda mfupi maana hutusaidia kuweza kutilia mkazo shughuli fulani, hivyo kuimaliza katika muda unaotakiwa. Lakini kiwango cha vichocheo hivi endapo kitakuwa juu katika mwili kwa muda mrefu huweza kusababisha tatizo la msongo wa mawazo. Tafiti zinaonyesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara huweza kushusha kiwango cha vichocheo hivi vya msongo wa mawazo hivyo kuzuia viwango hivyo kuwa juu kwa muda mrefu.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa namba 0752255949, barua pepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles