25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

KISA CHA ASHA NA UMUHIMU WA KUMSAMEHE MZAZI

Mama na Mwanawe
Na Christian Bwaya,

TUMEKUWA tukijadili namna uhusiano wetu na wazazi unavyoathiri aina ya malezi tunayowapa watoto wetu. Tumeona kuwa tabia walizokuwa nazo wazazi wetu zimechangia kutufinyanga kuwa hivi tulivyo.

Ndani yako yanaishi maisha ya utoto usiyoyagundua lakini yapo.  Unaweza usitambue hili lakini ndio hali halisi. Maisha yako yamezungukwa na sauti ulizozisikia tangu ukiwa mtoto. Inapotokea kuwa sauti hizo unazozisikia ndani yako ni hasi, inahitajika kazi ya ziada kuzinyamazisha.

Namna moja wapo ya kushughulika na majeraha haya ya utotoni ni kuwasamehe wazazi wako kwa makosa yao. Hakuna kosa lisilo na msamaha. Hata kama mama yako alikutupa na ukalelewa kwenye kituo cha yatima, bado unahitaji kufanya uamuzi wa kumsamehe.

Unapomsamehe, humsaidii yeye. Huenda hana habari na maumivu aliyokusaidia. Kumsamehe kunakusaidia wewe kuwalea wanao bila kuathiriwa na majeraha ya kukataliwa na kuonewa utotoni. Unamsamehe mzazi wako kwa faida ya wanao. Hili ni la muhimu mno.

Kisa cha mama mmoja kinaweza kutusaidia kuelewa umuhimu wa msamaha kwa wazazi. Asha alizaliwa nje ya ndoa. Baba yake aliyekuwa na ndoa nyingine, alikataa kuutambua ujauzito aliokuwa amempa Mwajuma ambaye ni mama yake Asha.

Unaweza kuelewa visa anavyokutana navyo msichana anayepata ujauzito akiwa shuleni. Mwanamume aliyempa ujauzito anamkataa. Wazazi wake nao kwa hasira ya kuaibishwa wanaweza wakamfukuza nyumbani. Shule nayo inamfukuza kwa kosa la kupata ujauzito akiwa mwanafunzi.

Kama vile haitoshi waumini nao wanamtenga kwa dhambi ya uasherati. Mwanamke huyu anajikuta katika mazingira ya upweke usio kifani. Unaweza usielewe kiwango cha uchungu na majuto anachoweza kuwa nacho mwanamke anayejikuta katika hali hii.

Katika mazingira hayo, anazaliwa Asha aliyekataliwa tangu akiwa tumboni. Wakati mwingine, hata wajomba zake, shangazi zake hawamtambui. Kila mmoja anamwona Asha kama mtoto ‘haramu’ asiyestahili heshima yoyote.

Anapopata akili, Asha anajikuta hana mtu mwingine zaidi ya Mwajuma mama yake anayemlea katika mazingira hayo ya uchungu wa kukataliwa na kila mtu. Faraja pekee ya mama huyu ni Asha mwanawe.

Kwa kuwa mama anahitaji mtu anayeweza kumwelewa bila kumhukumu, itakuwa rahisi kwake kumsimulia Asha mambo mazito aliyokutana nayo. Lengo ni kupunguza maumivu ambayo, kwa hakika, hawezi kumwambia mtu mwingine yeyote. Masimulizi hayo ya nia njema, yanapanda chuki na visasi kwa Asha dhidi ya baba yake, babu na bibi, ndugu na kila aliyehusika kumnyanyasa mama yake enzi za usichana wake.

Asha anakuwa mtu mzima. Moyoni mwake hana imani na watu. Anaamini watu ni waovu kama alivyokuwa baba yake. Haamini wanaume wanaweza kuwa na moyo wa kujali. Hata hivyo, hatimaye Asha anakutana na Mahamudu. Wanafunga ndoa.

Ndani ya Asha, unaishi uchungu ambao kwa haraka hawezi kukubali kuwa anao. Asha ni mwepesi wa kukasirika, Mahamudu anapofanya kosa. Wakati mwingine, anashindwa kudhibiti hasira yake mbele ya watoto. Asha, bila kujua, anaishi na kisasi dhidi ya baba yake. Kisasi hiki, si tu kinaathiri namna anavyoishi na mume wake, pia kinaharibu namna anavyowalea watoto wake.

Suluhu iliyo kwenye uwezo wa Asha ni kumsamehe baba yake. Kufanya hivyo ni hatua ya kwanza kwa Asha kuponya majeraha aliyonayo. Msamaha utaokoa kizazi cha Asha.

Itaendelea

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles