23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mawakili 6 wa Kubenea kumkabili Makonda

Pg 3Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

JOPO la mawakili sita wamejitokeza kumtetea Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa shtaka moja la kutoa lugha chafu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Mawakili hao, wakiongozwa na Peter Kibatala, walijitokeza katika mahakama hiyo jana na kudai dhamana baada ya kusomewa mashtaka hayo kwa madai kuwa shtaka la mteja wao linadhaminika.

Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya hakimu, Thomas Simba, Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis, alidai mahakamani hapo kuwa Desemba 14, mwaka huu katika Kiwanda cha TOOK Garment Com Ltd kilichopo Mabibo External wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, mtuhumiwa alimtolea lugha chafu Makonda hali ambayo ingeweza kuashiria uvunjifu wa amani na utulivu.

Alidai maneno hayo ni “wewe kibaka, mpumbavu, mjinga na cheo chenyewe cha kupewa tu”.
Kubenea alikana shtaka hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29, mwaka huu  kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, baada ya upelelezi kukamilika.

Mawakili wengine wa upande wa utetezi katika kesi hiyo, ni Rwegamalila Nshara, Nyaronyo Kicheere, Frederick Kihwelo, Jeremiah Ntobesya na Omary Msemo.
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemjia juu Makonda na kusema kinatambua mipaka yake.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana  na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene, ilisema Makonda anatumia vibaya madaraka yake kwa kukandamiza watu.

“Mkuu wa wilaya hana mamlaka ya kisheria, wala ya kisiasa kuhalalisha amri aliyoitoa ya kumkamata mbunge aliyekuwa anatekeleza wajibu wake. Tunatoa wito kwa mamlaka zilizomteua kumwangalia kwa makini kama bado anazo sifa za kuwa kiongozi wa ngazi hiyo,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo, imelitaka Jeshi la Polisi liwarudishie waandishi wa habari vifaa vyao vya kazi vikiwa katika hali salama na bila athari yoyote, baada ya kuwapora juzi ili wasiandike au kutangaza taarifa za Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles