23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Sh bilioni 65.7 za makontena gizani

Pg 1*Ni za ufisadi wa Bil. 80/- ulioibuliwa na Majaliwa

 Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

 WAKATI vita dhidi ya wakwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam ikipamba moto, umeibuka utata wa Sh bilioni 80 ambazo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema ni kodi ya makontena 329 kutoka kwa wafanyabiashara 58, walioyatoa bandarini bila kuyalipia kodi.

Akitoa ufafanuzi wa ukusanyaji wa fedha hizo, Desemba 12, Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Philip Mpango, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamekusanya Sh bilioni 10.6 kutoka kwa  wafanyabiashara 28 na kwamba wamebaki 15 wanaodaiwa Sh bilioni 3.7.

Kutokana na takwimu hizo, wafanyabiashara hao 15 nao wakilipa kodi, zitapatikana jumla ya Sh bilioni 14.3 kwa makontena yote 329, jambo linalofanya kuwe na upungufu wa Sh bilioni 65.7, tofauti na kiasi cha Sh bilioni 80 alichosema Waziri Mkuu Majaliwa.

Juzi Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alipotafutwa na gazeti hili kufafanua utata huo, alisema: “Sikiliza, usituingize kwenye ‘issue’ na waziri mkuu, ninachoweza kusema ni kwamba tumekusanya Sh bilioni 10.6 na zilizo nje bado ni Sh bilioni 3.7.”

Alipotafutwa Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Irine Bwire siku hiyohiyo, alisema waziri mkuu ameshatoka ofisini, lakini takwimu za Sh bilioni 80 hakuzitoa kichwani bali kwenye ripoti iliyotoka TRA.

“Mimi nitamuuliza vizuri kesho asubuhi (jana),” alisema Bwire.

Jana alipotafutwa tena, alisema hajafanikiwa kuzungumza na waziri mkuu kwa kuwa alikuwa na vikao vingi.

 “Labda baadaye kama atarudi ofisini kwa sababu sasa hivi amekwenda Ikulu kwenye kikao kingine,” alisema Bwire.

Rais Dk. John Magufuli, alipokutana na wafanyabiashara, alitoa siku saba kwa waliokwepa kulipa kodi kufanya hivyo na watakaokaidi watachukuliwa hatua.

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Desemba 12, Dk. Mpango alisema ni kampuni 28 tu ndizo zilizotii agizo hilo la rais na kufanikisha ukusanyaji wa Sh bilioni 10.6.

Dk. Mpango alisema kuwa muda wa kulipa kodi kwa hiari uliisha Desemba 11, hivyo wafanyabiashara 15 ambao wameshindwa kulipa kodi katika kipindi hicho “wasubiri cha moto” kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Hata hizo siku saba walizokuwa wamepatiwa tayari walikuwa wameshavunja sheria, hivyo wale waliolipa kwa wakati wamesamehewa kupelekwa mahakamani, lakini ambao hawajalipa watashtakiwa na kupigwa faini,” alisema Dk. Mpango bila kubainisha kiwango cha adhabu.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara hao walienda “kulalamika”, lakini TRA haitawasamehe kwa kuwa kodi hizo zinahitajika kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dk. Mpango alibainisha kuwa kati ya fedha zilizokusanywa katika kipindi hicho, Sh bilioni 4.16 zimetoka katika kampuni 13 ambazo zimelipa kodi yote iliyokuwa imekadiriwa, huku Sh bilioni 2.2 zikitoka katika kampuni 15 zilizotoa sehemu ya kodi wanayodaiwa.

Alisema bandari kavu (ICD) ya Azam ililipa kiasi cha Sh bilioni 4.17 kama dhamana kati ya Sh bilioni 12.6 ya kodi iliyokuwa imekwepa kulipa katika sakata hilo la upotevu wa makontena 329.

Akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na wale wa TRA katika ziara ya kushtukiza aliyofanya  Novemba 27, Waziri Mkuu Majaliwa, alimtaka aliyekuwa  Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu, Lusekelo Mwaseba, wahahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na kodi ya Sh bilioni 80 iliyokwepa ipatikane na kurudishwa serikalini.

 “Ninataka uchunguzi uanze kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. Nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yako wapi, na fedha hiyo ihakikishwe inarudi serikalini,” alisema.

Katika kikao hicho, Bade alikiri kwamba kuna upotevu wa makontena ambao huwa unafanyika kati ya bandarini na ICDs na hasa ICD ya Ubungo. Akitoa ufafanuzi, alisema kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia za wizi.

“Hata hivyo, tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia 327. Tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na Takukuru. Mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini Sh bilioni 12.6 na ameshalipa Sh bilioni 2.4,” alifafanua.

Alipoulizwa na Waziri Mkuu Majaliwa kama ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo, Bade alikiri kwamba anayo, lakini si kwa wakati huo labda ayapate kutoka kwa wasaidizi wake.

Baada ya kusema hayo, ndipo Waziri Mkuu Majaliwa alimuonyesha orodha ya makontena 349 yenye taarifa zote hadi namba za magari yaliyoyabeba, na Bade akakiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli.

 “Kwa utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akiwa bandarini hapo, Majaliwa alitangaza kusimamisha kazi maofisa watano wa TRA, na baadaye Rais Magufuli akatangaza kumsimamisha kazi, Kamishana wa TRA, Bade.

Siku chache baadaye, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Mpango, alitangaza kusimamisha kazi watumishi wengine 27 wa mamlaka hiyo kutokana na kashfa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles