24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaagiza Dk. Mwaka achunguzwe

3Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

SERIKALI imemwagiza Mkurugenzi wa Baraza la Tiba Asili Tanzania kumfanyia uchunguzi tabibu Dk. Juma Mwaka ndani ya wiki moja ili kujua iwapo amekidhi vigezo vya kisheria.

Agizo hilo limetolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangwala baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha Fore Plan Clinic kinachosimamiwa na Dk. Mwaka.

Alisema Dk. Mwaka amekuwa akitoa huduma ya matibabu kwa njia ambazo hutumiwa na madaktari wa kisasa na si asilia, huku akiwa hana cheti cha udaktari jambo ambalo ni kinyume na taratibu za utabibu.

“Najua alikuwa hapa muda mfupi uliopita, lakini alipogundua tunakuja yeye na wasaidizi wake akiwamo katibu na wafamasia walipitia mlango wa nyuma. Nafahamu  hana cheti cha udaktari, amekuwa akijifanya ni daktari na amekuwa akijitangaza jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utabibu.

“Mimi ni daktari, nimesomea udaktari wa tiba, tuna miiko, tena ile mikubwa, haturuhusiwi kuikiuka, ni pamoja na kujitangaza… haturuhusiwi kujitangaza, ni kinyume na maadili kujitangaza kwenye vyombo vya habari na kusema unatibu hiki au kile,” alisema.

Alisema Dk. Mwaka amekuwa akijiita daktari na akichambua mwili wa binadamu kama vile amesomea udaktari, wakati sheria ya tiba asilia na tiba mbadala hairuhusu kutumia maneno ya tiba ya kisasa.

Dk. Kigwangwala alisema baadhi ya wateja aliozungumza nao kituoni hapo, walimweleza  namna wanavyofanyiwa vipimo, na mmoja wao aliambiwa kuwa ana tatizo la homoni kwenye mirija ya uzazi (Falopian tube).

“Hivyo ninaomba kwa kutumia sheria ya tiba asilia na tiba mbadala, ufanyike uchunguzi dhidi yake ndani ya wiki moja na mniletee mezani kwangu mapendekezo ya hatua za kisheria za kuchukua pamoja na hao washirika wake.

“Nataka nijue taaluma za wote wanaotoa huduma katika kituo hiki, tiba wanazotoa na aina ya mitishamba wanayotumia ili tujue kama kweli Watanzania wanapata huduma stahiki na halali,” alisema.

Alitaka uchunguzi huo ufanyike pia kwa vituo vingine vya tiba asili kikiwamo cha Dk. Rahabu Lubago ambaye hujitangaza kutibu vidonda vya tumbo kwa dawa yake ya Fiterawa na cha Dk. Izike Ndodi.

“Wote wanajiita madaktari, wanachukua pesa nyingi za watu kwa kutumia lugha za ulaghai kupitia redio na televisheni kinyume na maadili ya taaluma za utabibu,” alisema Dk. Kigwangwala.

Dk. Mwaka, akizungumza na MTANZANIA juu ya taarifa hiyo, alisema kituo chake hakina matatizo yoyote.

“Nimepata taarifa hii, kituo changu hakina matatizo yoyote na kila kitu kinakwenda sawa sawa,” alisema Dk. Mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles