30 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

MATUKIO HAYA YATUPE MUDA WA KUTAFAKARI TULIPOKOSEA, TUNAPOKWENDA

FEBRUARI 21, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Dayosisi ya Karagwe, alizungumza mambo mengi juu ya amani na umuhimu wa viongozi wa dini kukemea mambo maovu yanayotokea nchini.

Pamoja na mambo mengine, Askofu Bagonza, alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kushauri na kuonya pale wanapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

Juzi pia Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Yohane, Raymond Manyanga, alipokuwa akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, aliyeuawa kwa kitu kinachodhaniwa ni risasi, alisema huu ni wakati wa kumwomba Mungu hekima, busara ili tuweze  kuvumiliana.

Aliasa watu kutochezea uhai kwa sababu hakuna mwenye uwezo wa kuurudisha. Alisema kama Watanzania tusipopatana na kukubaliana kuwa sote ni watu wa Mungu, tutamalizana.

Padri Manyanga, alisema mtu wa kutuunganisha Watanzania turudi kwenye umoja wetu ni Serikali pekee.

Ikiwa haijapita hata saa 10, mkoani Morogoro kumeripotiwa mauaji ya Godfrey Lwena, Diwani wa Chadema Kata ya Namwawala iliyopo Jimbo la Mlimba.

Lwena anadaiwa kuuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Tukitazama mauaji haya na kutafakari maneno ya watumishi wa Mungu hapo juu, tunaona ni muda sasa kama Taifa kukaa na kutafakari tunapoelekea. Lazima tutafakari ni wapi tulipokosea.

Ikumbukwe kwa sababu yoyote ile, hakuna mwanadamu mwenye haki ama mamlaka ya kutoa uhai wa mwenzake.

Kwa miaka yote, Tanzania imekuwa ikisifika kama kisiwa cha amani. Hata pale migogoro inapotokea tumekuwa na njia zetu kama Taifa za kuimaliza na kurudi kuwa ndugu.

Utamaduni wetu huo naamini bado upo, haujafa na hauwezi kufa, Utanzania wetu ni zaidi ya jambo lolote lile, ndiyo maana tumeishi zaidi ya miaka 50 tangu tupate uhuru tukiwa kama ndugu.

Ni muda mwafaka sasa kwa viongozi wa dini ambao wanatulea kiroho kuona ni nini cha kufanya ili kila mtu ajue kuwa uhai wa mwenzake una thamani sawa na wake.

Viongozi wa Serikali katika ngazi zote wajue ni nini cha kufanya ili kuliunganisha Taifa, watu wawe wamoja bila kuwa na chuki ama kinyongo cha kutamani kutoa uhai wake.

Vyama vya siasa vizungumze na wafuasi wao, kila mtu atambue umuhimu wa kumheshimu mwenzake na uhai wake.

Hizo ndizo njia pekee za kurudisha taswira njema ya Taifa letu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,409FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles