24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Matokeo kidato cha nne tunahitaji mjadala wa kitaifa kunusuru vijana

WIKI iliyopita Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018 na kutaja shule 10 zilizofanya vyema katika mtihani huo kwa shule zenye watahiniwa zaidi ya 40.

Wakati shule binafsi zikifanya vyema, mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi katika mtihani huo ni wa Shule ya Serikali ya  Sekondari Ilboru ya Arusha, Hope Mwaibanje.

Akitangaza matokeo hayo Katibu Mkuu wa Necta, Dk Charles Msonde amezitaja shule zilizofanya vizuri kuwa ni St. Francis Girls (Mbeya), Kemebos (Kagera), Marian Boys, Ahmes, Marian Girls (zote Pwani), Canossa, Bright Future Girls (zote Dar es Salaam), Maua Seminari (Kilimanjaro), Precious Blood (Arusha) na Bethel Sabs Girls (Iringa).

Katika matokeo hayo, watahiniwa 252 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu na kati yao, 71 ni wa kujitegemea huku wawili kati yao wakiandika matusi.

Akizungumza na wanahabari Dk Msonde alisema Mwaibanje wa Shule ya Sekondari Ilboru ndio amekuwa kinara akifuatiwa na Avith Kibani wa Marian Boys ya mkoani Pwani.

Nina kila sababu kumpongeza Hope wa Ilboru kwa kuonesha kwamba hata shule za Serikali zinao uwezo mkubwa wa kutoa matokeo mazuri iwapo tu zikiwezeshwa ikiwa ni pamoja na kuwapa mazingira mazuri ya kusomea  wanafunzi wake.

Naamini Hope amefaulu kutokana na jitihada zake binafsi na hii inatokana na mazingira yasiyo rafiki ya kusomea yanayozikabili shule zetu za Serikali. Matatizo yanayozikabili shule za Serikali kwa kiasi kikubwa yanaeleweka na yamechangia kwa kiasi kikubwa kufanya ufaulu wa shule hizi kushuka kila mwaka.

Wakati tukitafakari ya Hope, nashauri wahusika wa elimu kuanza kuwafuatilia akina Hope wengine na kujua hatima yao ya elimu, tusiishie kuwapongeza tu, ni lazima kujua hatima yao ya elimu inafika wapi.

Ningeshauri hata hizi Scholarships kuanzia sasa zipelekwe moja kwa moja kwenye shule za Serikali zinazoibua vipaji kama kina Hope na wengine kuepuka aina fulani ya upendeleo.

Baadhi ya shule zilizofanya vibaya

Ni vyema basi tukaanza kutafuta mwarobaini wa kushuka vibaya kwa ufaulu  kwa vjana hawa, kama tatizo liko mikononi mwetu ni vyema ukawekwa mjadala wa kitaifa na wadau wakajadili namna ya kujinasua kwenye jinamizi hili.

Mmoja wa wadau wa elimu kwenye Wilaya ya Chemba alitoa mfano wa wilaya hiyo akisema matokeo ya kidato cha nne Wilaya ya Chemba yanasikitisha wazazi na walezi kwani ufaulu unazidi kuchungulia kaburi.

Ikumbukwe kuwa wilaya hii kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka jana ilifutiwa matokeo kwa udanganyifu na hata wanafunzi waliopewa nafasi ya kurudia mitihani walifanya vibaya na kuwa ya mwisho.

Tukija kwenye matokeo ya kidato cha nne kwa Wilaya ya Chemba yameonesha kwamba hakuna ufaulu wa daraja la kwanza kwa wilaya nzima, daraja la pili wamefaulu wanafunzi kumi, daraja la tatu wanafunzi 65, daraja la nne wanafunzi443 na ziro imeanguka kwa wanafunzi 253.

Nimetoa mfano wa Wilaya ya Chemba tu lakini tatizo hili liko hata kwa baadhi ya Wilaya za Zanzibar zilizotangazwa ufaulu wao ni wa kiwango cha chini na kutajwa katika ya wilaya zilizo na shule zilizofanya vibaya kitaifa.

Hili tatizo la ufaulu mbaya tukiliacha tunatengeneza bomu na kuacha watoto wakipotea na inavyoonekana hakuna anayestuka kwenye hili. Ni lazima wadau na waratibu wa elimu kukuna vichwa.

Wilaya ya Chemba na Zanzibar elimu inazidi kuzama, viongozi wa kisiasa ni lazima wastuke juu ya hili, hawa tunaowatengeneza ni Taifa la aina gani? Wapiga kura gani?

Wadau wa elimu waungane waone tatizo linaanzia wapi? Kwani kila siku elimu inazidi kushuka?

Kuna madai kwamba Shule za Serikali walimu wake wanayo malimbikizo ya mishahara, lakini inakuwaje baadhi ya sehemu walimu walio na matatizo kama hayo wanafaulisha vizuri.

Ni lazima sasa majibu maswali haya yapatiwe majibu kuhakikisha ufaulu kwenye shule zetu za Serikali unaangaliwa kwa jicho la pekee.

Kwanza, Je, miundombinu inawawezesha watoto kusoma na kufaulu? Madawati yanatosheleza idadi ya watoto? Maabara na vifaa vyake vinatosheleza wanafunzi kuweza kufanya majaribio? Umeme? Vitabu vya kiada na ziada? Lakini pia walimu wakuu na waratibu elimu wa wilaya wanafanya kazi zao ipasavyo?

Maswali haya yatajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi iwapo ukiwapo mjadala wa kitaifa juu ya kushuka ufaulu kwenye shule zetu za Serikali. Tuchukue hatua sasa haraka iwezekanavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles