29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Mkataba mpya wa urafiki baina ya Ujerumani na Ufaransa

OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI

KATIKA historia ya karibuni Ufaransa na Ujerumani zilikuwa nchi hasimu wa jadi na katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia uadui baina yao ulipindukia mipaka kwa Ujerumani kuivamia Ufaransa na maelfu kwa maelfu ya watu wa mataifa hayo mawili wakapoteza roho zao kwa kupigana.

Baada ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, ilianza enzi mpya ya urafiki pamoja na masikilizano na mapatano baina ya majirani hao wawili. Mwaka 1963, viongozi wa nchi hizo mbili baada ya vita, Charles de Gaulle wa Ufaransa na Konrad Adenauer wa Ujerumani, walitiliana saini katika Kasri la Elysee, katika Mji Mkuu wa Ufaransa, Paris, mkataba wa urafiki baina ya nchi zao, hivyo kuzibadilisha nchi hizo zilizokuwa maadui kuwa marafiki na washirika wakubwa barani Ulaya.

Kwa hakika, nchi hizo zikawa waasisi na injini ya Umoja wa Ulaya, zikishirikiana katika siasa za Ulaya, ulinzi, mambo ya kigeni, siasa za maendeleo, uchumi, ulinzi wa mazingira na utamaduni.

Miaka 56 ni kipindi kirefu na mambo mengi yamegeuka duniani tangu wakati huo. Kwa hivyo, wiki iliyopita nchi mbili hizo zilihisi inafaa kuudurusu urafiki wao na kuupa msukumo mpya.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walikutana katika mji wa mpakani wa Ujerumani, Aachen na wakatia saini mkataba mpya baina ya nchi zao mbili.

Kuchaguliwa Aachen kama mahala pa kutia saini kulikuwa na umuhimu kwa vile mji huo unachukuliwa kuwa ni kitovu cha Ulaya. Katika mji huo aliishi Mfalme Karl (768-814), Wafaransa wakimuita Charlemagne, ambaye alitawala maeneo ya sasa ya Ufaransa na Ujerumani.

Kwa hakika mwanafalsafa Michel Serres miaka kadhaa iliyopita alipendekeza kwamba mafungamano hayo ya zamani baina ya nchi mbili hizi yarejeshwe. Hata hivyo, mahusiano hayo hivi sasa yamefikia mbali.

Kutokana na mkataba huu mpya, Ufaransa na Ujerumani zitaarifiana na kupatana kuhusu siasa zao za kigeni, zile zinazohusu Bara la Ulaya na ulinzi pamoja na kubadilishana ziara za vijana wa nchi zao mbili. Mikoa iliyoko katika mpaka wa pamoja wa nchi hizo mbili itazidi kushirikiana na vijana wa Ufaransa na Ujerumani watatiwa moyo wasome lugha ya nchi ya pili.

Katika mktataba huo imetajwa pia kwamba Ujerumani na Ufaransa zinataka kuwa na kanuni za aina moja katika kusafirisha nje silaha zao. Itakumbukwa kwamba hivi karibuni Ujerumani iliiwekea Ufalme wa Saudi Arabia vikwazo vya kuiuzia silaha, wakati Ufaransa ikiendelea kuipatia silaha nchi hiyo ya Kiarabu. Pia mkataba huo unataka kila nchi kati ya hizo mbili ijiweke tayari kumsaidia mwenzake, hata ikiwa kijeshi, pale nchi hiyo inaposhambuliwa kutoka nje.

Hiyo ni ishara kutokana na kutotegemewa Marekani hivi sasa kutoa msaada kwa washirika wake. Mara kadhaa Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akizisimanga baadhi ya nchi shirika za Ulaya katika Umoja wa Kujihami wa NATO kwamba zinategemea ulinzi wa Marekani, lakini bila ya kuchangia vya kutosha gharama za ulinzi huo.

Kutakuwapo eneo la kiuchumi la nchi hizo mbili. Hii inatokana na lawama zinazotolewa na wafanyabiashara wa Kijerumani kuhusu vizingiti vya kirasimu vilivyoko Ufaransa.

Katika maeneo ya mipakani baina ya nchi mbili hizo kutakuwapo Eneo la Ulaya. Kutakuwapo shule za chekechea za Kijerumani na Kifaransa. Pia itarahisishwa katika maeneo hayo kusambaza maji na umeme wa pamoja, na kutakuwapo usafiri wa treni za barabarani kwa pamoja, mfano ukichukuliwa usafiri wa treni za barabarani kati ya mji wa Strassburg (Ufaransa) ambao karibu miaka miwili sasa zinapita treni za barabarani juu ya Mto Rhein hadi mji wa Kehl (Ujerumani).

Kansela Merkel katika hotuba yake kwenye sherehe hiyo ya kutia saini alisema mkataba huo mpya ni jibu la pamoja la nchi hizo mbili kukabiliana na kupata nguvu hisia za uzalendo wa kinazi na siasa nyepesi na rahisi za kujitafutia umaarufu.

Alisema mtu sasa anaishi katika wakati maalumu unaohitaji majibu yenye msingi na yanayojielekeza katika mustakbali. Pia watu wengi wanangojea ishara ya ushirikiano baina ya Ujerumani na Ufaransa zikitembea mkono kwa mkono kuzishinda changamoto zilizoko mbele.

Naye Rais Macron wa Ufaransa alisema kitisho cha sasa kinakuja si tu kutoka nje, lakini kutoka ndani ya jamii pia na kwamba Ulaya haiwezi kuendelea kuishi bila ya watu wake kusikilizana. Ulaya ya sasa si ndoto ya kuwa na Dola Kubwa la kutawala watu wengine, lakini Ulaya ya sasa ni mradi wa kujenga demokrasia. Kuipenda na kuiunganisha Ulaya si mambo yanayopingana. Alisema: Tunazipenda nchi zetu, lakini tunaipenda pia Ulaya.

Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, alizitaka Ufaransa na Ujerumani zitumie mafungamano yao kwa ajili ya Ulaya na si kwa ajili ya mfumo ulio mbadala na Ulaya. Naye Rais wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, aliuona urafiki baina ya Berlin na Paris kuwa ni injini ya Ulaya na alipoulizwa kama yeye anaufurahia mkataba huo mpya, alijibu: Bila shaka! Mkataba huu ni zaidi ya maneno ya kisheria, lakini ni masuala ya kutoka moyoni.

Kuna lawama miongoni mwa vyama vya mrengo wa kushoto kwamba mafungamano haya baina ya Ujerumani na Ufaransa yatazidisha mataifa hayo mawili kujilundikizia silaha na kupunguzwa misaada ya kijamii kwa watu wasiojiweza.

Vyama vya mrengo wa kulia, kama vile AfD hapa Ujerumani, vinahofia kuchomoza Umoja Mkubwa wa Ulaya ukisimamiwa na Ujerumani pamoja na Ufaransa, hivyo dola za kitaifa zinaweza zikadhoofika.

Wafaransa wenye siasa za mrengo wa kulia kabisa wanadai kwamba mkataba huo utasababisha maeneo ya Elass-Lothringen kujitenga kutoka Ufaransa na kujiunga na Ujerumani, jambo ambalo linakanushwa kabisa na Serikali za Ujerumani na pia Ufaransa na kuitwa kuwa ni uzushi.

Ilivyokuwa Ufaransa, kiuchumi haifanyi vizuri kama Ujerumani, bila shaka, kutakuwapo kuoneana kijicho.  Pendekezo la Chama cha Social Democratic (SPD) cha Ujerumani kwamba kuwapoi bima ya Ulaya ya ukosefu wa ajira haichangamkiwi na washirika wa Kiconservative katika Serikali ya Mseto ya Berlin. Hivyo hivyo kuhusu suala la Bajeti ya pamoja ya Ulaya.

Ujerumani na Ufaransa hazijawahi maisha kuwa marafiki wa chanda na pete kama ilivyo sasa. majeshi ya Kifaransa ya Napoleon yaliikalia Ujerumani mwanzoni mwa Karne ya 19, lakini sasa nchi hizi mbili zinaafikiana vizuri na kila mara zina fikara za aina moja.

Kuna watu wasiofurahia sana mafungamano haya makubwa: Mambo yakiwa mengi sana, inakuwa tena mengi mno. Lakini pindi Wajerumani na Wafaransa watatofautiana mara moja, basi ni wahakiki hao hao watakaozuka na lawama.

Mkataba wa Aachen, kwa hivyo, ni mkusanyiko wa mambo madogo yanayoweza kutendeka na pia ni jumla ya mambo yanayotamaniwa kupatikana. Pia hati hiyo mpya inakanusha yale madai kwamba Berlin maisha inaweka breki linapokuja suala la kuliendeleza eneo la sarafu ya Ulaya, Euro.

Umoja wa Mabenki ndani ya Ulaya bado linabaki kuwa suala la mabishano. Ujerumani inapinga matakwa ya mabenki ya Ufaransa kwa vile inahofia kwamba walipaji kodi wa Kijerumani itawabidi baadaye walipie gharama za hasara za mabenki ya nchi nyingine za Ulaya pindi biashara za mabenki hayo zikienda kombo.

Bila shaka, kutakuwapo matatizo katika suala la kutuma majeshi ya nchi mbili hizo katika nchi za ng’ambo. Rais katika Ufaransa ana madaraka makubwa na anaweza kulituma jeshi la nchi yake hadi mahala kokote duniani. Lakini Ujerumani hujizuwia kidogo katika suala hilo.

Pia Ufaransa imeahidi itaisaidia Ujerumani ipate kiti (uwanachama) wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hili ni takwa tu, ikijulikana kwamba hivi sasa kuna wanachama watano wa kudumu katika Baraza hilo walio na kura za turufu na kwa hivyo maisha atatokea mmoja kati yao ambaye atazuwia Ujerumani isipate nafasi hiyo.

Ulaya ina mapafu mawili ya kuvutia pumzi, Ujerumani na Ufaransa. Ilimradi mapafu hayo mawili yote yanavuta pumzi kwa pamoja na kwa utulivu, basi hakuna shaka yoyote mwili mzima unaoitwa Ulaya utakuwa salama salimini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles