26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Matheo Qares amvaa Samuel Sitta

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

Na Abraham Gwandu, Babati

ALIYEWAHI kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi, Matheo Qares, amemshutumu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akisema kuwa kiongozi huyo amepwaya katika kila nafasi ya uongozi.

Qares pia amehoji uhalali wa Sitta kuendelea kukusanya maoni ya Katiba Mpya wakati kazi hiyo ilikwisha kufanywa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili   nyumbani kwake katika Kijiji cha Nkwaa nje kidogo ya mji wa Babati juzi, alisema katu haungi mkono hatua ya Sitta kuendelea   kuwa Mwenyekiti wa Bunge  akidai kuwa amepungukiwa sifa za uongozi.

Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa anajishughulisha na kilimo na ufugaji, alisema kitendo cha Sitta kuburuza vikao vya Bunge la Katiba na kuendelea kukusanya maoni kutoka makundi mbalimbali, ni ishara tosha kwamba hafai kuwa kiongozi wa wananchi kwa sababu  hafuati misingi, sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa na kiongozi.

“Ni nani alimpa Sitta kazi ya kukusanya maoni ya makundi anayodai maoni yao hayakuchukuliwa? Ameonyesha dharau kwa Tume ya Jaji Warioba iliyokusanya maoni ya wananchi, anataka kila kitu kiandikwe kwenye Katiba, malisho ya wafugaji yaandikwe, maeneo ya kunyweshea maji, masoko kweli yote yaandikwe?” alihoji na kuongeza:

“Vipi makundi mengine kama wachimbaji wa madini pale Mererani, wavuvi nao wakiendelea kupeleka mambo yao yaandikwe kwenye Katiba, nasema katika hili amevurunda na amepwaya hawezi kuwapatia wananchi Katiba wanayoitaka bali watapendekeza Katiba ya viongozi,” alisema.

Alisema kinachoendelea sasa katika Bunge Maalumu la Katiba ni vurugu ambako kila mjumbe wa Bunge hilo  anafanya anachoona kinafaa kwa masilahi yake au ya chama chake na hata kuondoa dhana ya kupatikana  Katiba ya wananchi.

Qares alipinga hatua ya Sitta kuendelea kung’ang’ania vikao vya Bunge kwa vile ana malengo yake binafsi ya siasa, huku akiamini wananchi watamwona kama shujaa wao jambo ambalo halitatokea.

“Analichukulia kwa mtizamo na kwa malengo binafsi ya siasa akidhani atakuwa hero (shujaa). Lakini ameonyesha kushindwa tangu mwanzo. Ningekubaliana naye kama haamini Rasimu ya Warioba angekataa tangu mwanzo wasingeanza kuijadili ili wananchi waamini hiki anachokisema sasa kwamba rasimu ina upungufu,” alisema.

Kuhusu madai ya baadhi ya wanasiasa kwamba mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ulivurugwa na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge la Katiba, Qares alisema Rais Kikwete hakufanya kosa ila alikuwa anatoa maelekezo kwa Tume juu ya Muungano.

“Rais hakufanya vizuri kuwaambia wajumbe wa tume wasiruhusu mawazo ya kuhoji Muungano, kwa nini wananchi wasihoji? Kitendo cha kuwakataza kiliamsha hisia za wananchi wakaanza kuhoji kwa nini wakatazwe kuhoji muungano, tangu mwanzo niliposikia hivyo nikasema Katiba haitapatikana.”

“Kama haitoshi, Warioba na tume yake walipofika kwangu nilimwambia mmeanza na mguu mbaya na nimewasilisha maoni yangu kwa maandishi, nilisema hamuwezi kufunga mkokoteni mbele ya punda mkasema uko sawa tuu.

“….  sasa ukiwaambia hawa kwa nini mawazo ya wananchi kuhusu muundo wa  Muungano hayachukuliwi, wanadai tukiwauliza watavunja Muungano, sasa si ndiyo mawazo yao? Waachiwe wayatoe,” alisema.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema mawazo na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na kundi la G 55 lililokuwa likiundwa na wabunge wa CCM mwanzoni mwa miaka ya 1990 yalikuwa bora zaidi ya kile kinachofanywa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

“Kile kilichokataliwa wakati ule ni bora zaidi kuliko hiki kinachopendekezwa sasa. G 55 ilipendekeza na kutoa mawazo mazuri sana kuhusu muundo wa Muungano, lakini sasa sielewi kinachofanyika huko Dodoma.”

Alisema   makosa mengine yaliyofanyika ni kitendo cha kuwaingiza wanasiasa kuwa wajumbe wa Bunge hilo.

Qares alisema hicho ni kiini cha mkwamo unaoendelea na kamwe hawawezi kuwaletea wananchi Katiba bora bali wanaangalia masilahi yao.

- Advertisement -

Related Articles

5 COMMENTS

  1. Naunga mkono maoni ya Kada huyu mkongwe wa CCM.Kwa kweli kama Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba haikubaliki, jambo la busara siyo kwa Bunge hilo kuibadilisha na kupokea maoni mapya. Jambo la busara lilikuwa kurudia zoezi hilo kuanzia ukusanyaji wa maoni ya Wananchi na kuandika Rasimu mpya. Au kupeleka moja kwa moja kwa Waanchi kwa maana ya kura ya maoni.

  2. Kwa kifupini kwamba Sitta pamoja na CCM wamekata tamaa ya kuongoza na kushinda uchgauzi mwaka 2015. Wanaharibu kanuni na sheria ili kuivuruga nchi, ni jukumu la wananchi bilakujali chama, dini, kabila kuikataa katiba mpya kwa kishindo na kuikataa CCM katika uchaguzi mkuu 2015. CCM ikiondoka madarakani na maovu mengi yataondoka, nchi imefikia hapa kwa sababu ya udhaifu wa serikali ya CCM. NI afadhali kujaribu wengine kuliko kuendelea na uongozi mbovu. Watanzania tujenge ujasiri wa kufanya mabadiliko, tusiogope. Hadi sasa CCM imeonyesha inatawala kwa mabavu na madharau kwa wananchi, na vitisho hii ni demokrasia gani?

  3. Mzee Saba kachoka kabisa. Hayo maoni anayokusanya ni kwa sheria ipi? iliyotungwa lini? na Bunge gani?

    Mzee huyu hajui kama document hiyo (rasimu ya tume)ni summarized ili iweze ku accomodate kila kitu

    Kweli Mungu amewapa upofu viongozi wa ccm wasiweze kuona ili waadhibiwe 2015

  4. tatizo la watanzania ni kutokua na maamuzi sahihi na hasa pale inapokua ni kwa ajili ya mstakabari wa nchi. Hivi ni kwa nn watanzania tusiikatae hii katiba wakati wa kura ya maoni? Huu ndo mda wa wananchi wa Tanzania kuzunduka na kujitambua kua viongozi tulokua nao hawana mchango wowote kwetu bali ni kwa maslahi yao ndo maana kamati zilizo nyingi zinapendekeza kuondoa sura na ibara zinazobana viongozi kuhusu uwajbikaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles