26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jenerali Musuguri: Nilitamani kumchinja Idd Amin

mtanzania 010914
mtanzania 010914

Na Kulwa Karedia, Butiama

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi mstaafu, Brigedia Jenerali David Musuguri, amesema aliumizwa sana na ukatili alioufanya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin Dada na kuapa iwapo angemkamata akiwa hai angemchinja.

Jenerali Musuguri aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi  kati ya mwaka 1980 hadi 88 wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Hayati Mwalimu Nyerere, alisema hayo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kitongoji cha Kitanga, Wilaya ya Butiama hivi karibuni.

Jenerali Musuguri alikuwa akizungumzia jinsi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilivyopigana kuukomboa Mkoa wa Kagera wakati Iddi Amin alipovamia Novemba 1978.

Katika uvamizi huo, Idd Amin alishusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupandisha bendera ya Uganda huku Watanzania wasio na hatia wakiwamo watoto waliuawa  na wengine kupata vilema vya kudumu.

Akizungumzia kilichojiri wakati huo wa vita, Jenerali Musuguri alisema katika uwanja wa vita majeshi ya Amin yalipigwa na majeshi ya Tanzania na kusababisha Idd Amin kukimbilia Libya kuomba hifadhi.

Aliwataja makamanda walioshirikiana bega kwa bega katika vita ya Uganda kuwa ni Meja Jenerali Tumaniel Kiwelu, Meja Jenerali Silas Mayunga ‘Mti Mkavu’, Meja Jenerali Martin Mwakalinde na Meja Jenerali John Walden.

“Nakumbuka tulikwenda hadi kwenye mipaka ya nchi za Sudan na Msumbiji, tulipigana vita usiku na mchana bila kuchoka…Amin pamoja na kusaidiwa na Libya alikumbana na upinzani mkali.

“Kwa kweli kama siku ile mwaka 1979 asingekimbia na kupanda ndege kukimbilia Libya, ningemkamata pale Nakasongola. Nilitamani nimkamate lakini sikufanikiwa mpaka nasikia amefia Saudi Arabia.

“Unajua mtu yule hakuwa wa kawaida, kuna watu wetu walikufa, dada zetu walibakwa ovyo, mali za Watanzania ziliporwa huku wenzetu wa Kagera wakiuawa pasipo na hatia yoyote, sasa mtu kama huyo utaendelea kumvumilia kwa kipi?

“Kama ningemkamata dikteta Idd Amin Dada, ningemchinjachinja kama mbuzi wa kafara,” alisema Jenerali Musuguri.

Kwa mujibu wa Jenerali Musuguri, Amin aliivamia Tanzania Oktoba 30, 1978 na kuamuru majeshi yake kuvuka mpaka na kulivamia eneo la Tanzania huku Watanzania zaidi ya 10,000 wasiokuwa na hatia waliangamizwa na eneo la kilomita za mraba 1,850 zilichukuliwa na majeshi ya Uganda.

Alisema majeshi ya Amin yalilikalia eneo la Mto Kagera sehemu ya Kyaka na kufanya vitendo vya kinyama kwa kuua wananchi wa Mkoa wa Ziwa Magharibi (hivi sasa Kagera), kuchoma nyumba, viwanda, kupora mali na kuzipeleka Uganda.

“Kibaya zaidi aliwachukua akina mama wajawazito na kuamuru wafungwe kamba kisha wanamwagiwa petroli na kuwashwa moto. Huu ni unyama mbaya ambao sijawahi kuuona maishani,” alisema.

Soma mahojiano maalumu kati ya gazeti hili na Jenerali Musuguri katika ukurasa wa 13.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles