Maswali ndege mpya kukamatwa

0
919

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MIEZI michache baada ya Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini kuzuia ndege ya Air Tanzania kabla ya kuiachia baadaye, nyingine mpya aina ya Bombardier Q400 imekamatwa nchini Canada.

Ndege aina ya Airbus A220-300 iliyoshikiliwa Afrika Kusini Agosti 24 mwaka huu, ilitokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na raia wa nchi hiyo, Hermanus Steyn ambaye alidai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.  

Kesi hiyo ilisababisha Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kuizuia ndege hiyo kuondoka nchini humo, lakini baadaye Serikali ya Tanzania ilishinda kesi bila kutoa fedha yoyote. 

KUKAMATWA BOMBARDIER Q400 

Taarifa za kukamatwa ndege mpya aina ya Bombardier Q400 zilielezwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi wakati Rais Dk. John Magufuli akiwaapisha mabalozi watano Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Profesa Kabudi alisema aliyesababisha ndege hiyo ya Bombardier Q400 kukamatwa ni Steyn, mkulima ambaye alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini akidai fidia ya dola milioni 33.

Alisema kuendelea kwa vitendo hivyo ni hujuma za mabeberu wasiofurahishwa na maendeleo ya Tanzania.

“Tulikwenda mahakamani (Afrika Kusini) tukamshinda, akakata rufaa na wiki iliyopita tukamshinda tena, huyo huyo sasa amekimbilia Canada amekamata ndege ya Bombardier Q400 ambayo ilikuwa ifike nchini.

“Jambo linalosikitisha ndege zilizokuwa zinatoka Marekani aina ya Dreamliner mbili hazikukamatwa, zimefika, lakini kila ndege inapotakiwa kuondoka Canada tunashangaa hao matapeli wanajuaje na ndege zinakamatwa,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema Balozi wa Tanzania nchini Canada aliitwa na kuelezwa jinsi nchi isivyofurahishwa na kukamatwa kwa ndege zake kila zinapokaribia kuondoka huko.

“Nimemwambia si tu kwamba tunasikitika, bali tunakasirishwa na tunafikiri mheshimiwa Rais kukushauri kama Canada inaendelea kuruhusu vitu kama hivyo, si wao peke yao wanaotengeneza ndege, hatukufanya makosa kununua ndege Canada, hata Brazil wanatengeneza ndege,” alisema Profesa Kabudi.

Kutokana na hilo, Profesa Kabudi alisema tayari wameandaliwa wanasheria kwenda nchini Canada kuipigania ndege hiyo.

MKULIMA ALIVYOIKAMATA NDEGE YA KWANZA

Septemba 4, mwaka huu mkulima huyo baada ya kushindwa kesi ya ndege aina ya Airbus A220-300 aliyokuwa ameikamata Uwanja wa Ndege wa OR Tambo, nchini Afrika Kusini iliachiwa na Mahakama Kuu ya Jimbo la Gauteng na kurejea Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Damas Ndumbaro ambaye pia ni wakili, akiwa pamoja na jopo la mawakili wengine wa Tanzania na wale wa Afrika Kusini, alieleza jinsi Tanzania ilivyoridhishwa na uamuzi wa mahakama.

Mkulima Steyn ambaye alipeleka shauri hilo mahakamani na kupata kibali cha kushikiliwa ndege hiyo, hakuridhishwa na hukumu ya awali na kukata rufaa, ambayo pia ilitupiliwa mbali na mahakama.

Wakati huo Dk. Ndumbaro alikaririwa akisema kama Steyn bado ana madai yoyote, inafaa arudi kwenye mahakama za Tanzania na kusikilizwa.

Dk. Ndumbaro pia alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania imeshamlipa Steyn dola milioni 20, kwamba wapo tayari kumalizia bakaa ya deni, lakini mkulima huyo anatakiwa kurudi katika mahakama za Tanzania, na aache kuihusisha Afrika Kusini.

Baada ya kushindwa kwa kesi ya awali na hatimaye rufaa, wakili wa Steyn  alikaririwa akisema uamuzi wa mahakama ni kushindwa moja kwa moja kwa haki, na mteja wake anaona kuwa ameonewa.

Jaji aliyesikiliza rufaa, alisisitiza kuwa Afrika Kusini haina mamlaka ya kisheria (jurisdiction) ya kuliamulia jambo hilo.

MKULIMA HUYO NI NANI?

Steyn alikuwa anamiliki ardhi, mifugo na mali nyingi ambazo zilitaifishwa na Serikali ya Tanzania miaka ya 1980.

Ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, kwa ujumla wake dola milioni 33 na tayari ameshalipwa dola milioni 20 kati ya hizo.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, Serikali ya Tanzania, kwa mujibu wa mkulima huyo imeacha kulipa deni hilo, na hatua ya kukamata ndege ilikuwa moja ya harakati zake za kutaka kumaliziwa deni.

NDEGE YA KWANZA KUKAMATWA

Mwaka 2017 ndege nyingine ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-8 ilizuiwa nchini Canada kutokana na madai ya Sh bilioni 87.3 zilizokuwa zikidaiwa na kampuni ya kikandarasi. 

Aliyefichua kuhusu kukamatwa kwa ndege hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu na baadaye Serikali ilijitokeza na kukiri jambo hilo.

Kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa  Lissu wakati huo, ndege hiyo ilikamatwa kwa amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, baada Kampuni ya Stirling Civil  Engineers Ltd kuidai Serikali Dola za Marekani milioni 38.7 (Sh bilioni 87) kutokana na hatua yake ya kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka  Wazo Hill hadi Bagamoyo mwaka 2009.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa ndege hiyo kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alikiri kuwepo kwa mgogoro katika ununuzi wa ndege hiyo ambao alisema umechangiwa na kesi iliyopo mahakamani iliyosababisha kuzuiwa.

“Mgogoro huo upo, lakini kimsingi umetengenezwa na Watanzania wenzetu baada ya kuweka mbele masilahi ya kisiasa badala ya kuweka mbele ya taifa,” alisema Kawawa.

Alisema kutokana na mgogoro huo, kampuni husika ambayo hakuitaja kwa jina, imepeleka kesi mahakamani na kuweka zuio lililoelekeza ndege hiyo isiondolewe hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa.

RAIS MAGUFULI

Akizungumza baada ya kuwaapisha mabalozi jana, ambao ni Meja Jenerali Anselm Shigongo Bahati (Misri), Mohamed Abdallah Mtonga (Abu Dhabi), Jestas Abouk Nyamanga (Ubelgiji), Ali Jabir Mwadini (Saudi Arabia) na Dk. Jilly Elibariki (Burundi), Rais Magufuli  hakuzungumzia suala la ndege hiyo mpya kukamatwa, badala yake aliwatakia heri katika majukumu yao ya kuiwakilisha Tanzania katika nchi walizopangiwa.

Zaidi aliwataka kuripoti katika vituo vyao kwa kipindi kisichozidi wiki moja kukamilisha taratibu za kuaga na kuondoka nchini kwenda kwenye vituo walivyopangiwa.

“Samahani kidogo kwa mabalozi walioteuliwa, kumekuwa na tabia mkishateuliwa mnakaa miezi mnakwenda kuaga kwenye maofisi, leo (jana) ni juma ngapi?

“Leo (jana) ni Jumamosi, ninawapa wiki moja tu muwe mmeshaondoka Tanzania kwenda kwenye sehemu zenu.

“Nataka niwaeleze wazi kwa sababu mmeshateuliwa muende mkafanye kazi, imekuwa ni tabia leo niko kwenye ofisi ya waziri nani, nakwenda wapi, hapana. Tumeshamaliza maagizo, hakuna kwenda kuaga kazini. Mungu awajalie,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka mabalozi hao pamoja na wengine wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali, kusimamia vizuri fedha na mali zilizopo katika balozi hizo.

Mbali na hilo, pia aliwataka mabalozi hao kusimamia vizuri utekelezaji wa kidiplomasia ya uchumi ili Tanzania inufaike na uhusiano mzuri uliopo kati yake na nchi wanazoziwakilisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here