25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Kauli za Askofu Pengo mjadala

Na GRACE SHITUNDU – DAR ES SALAAM

KAULI ambazo amekuwa akizitoa Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwenye masuala makubwa yanayoigusa nchi, mara kadhaa zimeonekana kuzua mijadala mikubwa kiasi cha kuwagusa viongozi wenzake wa dini na watu wa kada tofauti katika jamii.

Kauli yake ya hivi karibuni iliyozua mjadala ni ile aliyoitoa wiki hii katika mkutano alioutisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuzungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya mkoa wake.

Katika mkutano huo, viongozi wa dini walipitisha azimio la kumpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kazi aliyoifanya kipindi cha miaka mine tangu aingie madarakani.

Akizungumza katika mkutano huo, ikiwa ni miezi mitatu tangu Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis aridhie ombi lake la kustaafu kama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Pengo mbali na kuhoji wanaomwita Rais Magufuli Dikteta, alimmwagia sifa Makonda akisema ni kiongozi wa aina yake na msadizi bora kwa Rais.

Kwa maneno yake mwenyewe, Kardinali Pengo alisema; “Kwa maana hii kwamba Rais wetu ni mtendaji, lakini hawezi akafanya yote peke yake, anahitaji watu ambao wapo pamoja naye.

“Kwa kitendo cha leo cha kutuita na mambo uliyotueleza wewe (Makonda), naweza kukuweka katikati ya watu ambao ni wasaidizi bora wa Rais Magufuli, tunapomwombea kwa Mwenyezi Mungu Rais Magufuli aendelee, tunakuombea na wewe na vijana wa aina yako muendelee.”

Aliongeza; “Tunajiuliza baada ya Magufuli atakuwepo nani? Mkiwepo kama wa aina yako (Makonda) wengi, mimi nisingekuwa na shaka kwamba tutakuwa na watu wa kuendeleza kazi.” 

Kauli hizo za Kardinali Pengo zilimwibua Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dk. Stephen Munga aliyesema kuwa viongozi hao wa dini walijipendezesha zaidi wakati wa kuongea na pia alimtaja moja kwa moja Askofu Pengo kuwa alisifu kwa kupitiliza.

Askofu Munga katika andiko lake lililosambaa katika mitandao ya kijamii, alisema Askofu Pengo alitoa kauli tata zinazoweka utukufu kwa wanadamu na si kwa Mungu na hakutegemea angetoa maneno ya aina hiyo.

“Wenzangu viongozi wa kiimani katika mkutano ulioitishwa na komredi Makonda na kupewa nafasi ya kuongea kwa kweli mlijipendezesha,” alisema Askofu Munga.

Alisema kiapo chake kinamtaka mchungaji aseme kweli hata kama amekaa mezani akila na kaisari, lakini hajui kiapo cha kiuchungaji cha upande mwingine kinasemaje.

Kuibuka kwa Askofu Munga pia kulikoleza mijadala katika kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Baadhi ya watu walionyesha kutilia ukakasi kauli ya Askofu Pengo, wakikumbuka mjadala mpana wa siku za nyuma kuhusu tuhuma za Makonda kutokuwa na vyeti vya elimu.

Wengine walikwenda mbali na kumshutumu kwa utovu wa nidhamu kwa madai kuwa aliwahi kupiga viongozi na wengine wakihoji kile walichodai kauli tata za kujikweza na kuanzisha mambo yasiyoisha.

2015: KATIBA MPYA 

Pamoja na hayo, hii si mara ya kwanza kwa kauli za Kardinali Pengo kuzua mijadala katika masuala ya kitaifa na hata kuwaibuia viongozi wenzake wa dini na watu wa kada mbalimbali.

Mwaka 2015 aliwahi kutoa kauli iliyoonyesha kupingana na waraka uliotolewa na Jukwaa la Wakristo kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya yenye maoni ya wananchi.

“Mtu akiniambia ‘priority’ (kipaumbele) ya Tanzania ni Katiba Mpya inabidi anithibitishie huo ukipaumbele, maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya Katiba Mpya. Kwangu mimi Katiba ni kitu ambacho kije baadaye, si cha haraka. 

“Wanasiasa wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya Katiba. Wasiache watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu ya Katiba,” alisisitiza Kardinali Pengo wakati huo.

Kauli hizi ziliwaibua baadhi ya maaskofu walioonekana kumpinga waziwazi akiwemo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Askofu Gwajima alionekana kukerwa na msimamo wa Askofu Pengo na hata kutoa maneno makali dhidi yake hatua iliyosababisha kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hata hivyo, Askofu Pengo hakumjibu na Askofu Gwajima aliachiwa huru baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuifuta kesi ya kutoa lugha ya matusi kwa hoja kwamba upande wa Jamhuri ulishindwa kujali kwani kwa miezi 14 walipeleka shahidi mmoja kutoa ushahidi.

2018: WARAKA WA KWARESMA 

Aidha mwaka 2018 Askofu Pengo tena alizua mjadala baada ya kutoa kauli kuhusu waraka uliotolewa na maaskofu 35 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika kuelekea mfungo wa Kwaresma mwaka huo.

Waraka huo wa TEF ulifuatiwa na ule wa maaskofu 27 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT) ambao nao uligusa na kuonya mwenendo wa masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Askofu Pengo alipokuwa akiadhimisha Jumapili ya Matawi sambamba na tamasha la vijana huko Bagamoyo mkoani Pwani mwaka huo, alisema hakuwa anajua kama kuna waraka utatolewa kuhusu Kwaresma na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, huku akisema waraka huo una mazuri mengi japo umechanganya dini na siasa.

Katika ibada hiyo, Askofu Pengo alisema maneno haya; “Barua ile ijapokuwa hata jina langu mnaliona limeandikwa pale, kwamba na mimi ni mmoja wa waandishi au watamkaji… mimi nimeipokea, baadhi yenu mmeshaipokea.

“Kwahiyo sioni namna gani mimi naweza kuwa mwandishi au mhubiri kwenu wa ile barua ambayo imetungwa labda na maaskofu… naamini na baadhi ya maaskofu, lakini mimi mwenyewe hata nilikuwa sijaiona, hata nilikuwa sijaambiwa kuna kitu cha namna hiyo kinakuja.

“Tuelewane vizuri, ninaposema hivi, sitaki kusema ile barua ni mbaya. Moja tu ni kwamba barua nzima imechanganya vitu viwili; Mwalimu angekuwepo angepiga kelele maaskofu msichanganye dini na siasa.

“Angepiga kelele sana kuhusu waraka huu katika nyakati zake. Na hilo nawaambia sina hofu, muende mkamwambie mtu yeyote nimesema hivi. Ndio wala msione aibu, najua labda hata wengine mmekunja nyuso, kunjeni tu, lakini huo ndio msimamo wangu.

“Zipo sehemu katika waraka huo zinazochanganya dini na siasa, na si kazi ya maaskofu, ni kazi yenu wanasiasa mkiwa ni wa Chadema, mkiwa ni wa CCM, lakini haiwezi kuwa kazi yangu mimi.

“Siwezi kwanza nikaanza kuchambua na ‘ku-criticize’ (kukosoa) Serikali katika mambo yaliyo yake; sikupewa mamlaka hayo. Na kwanini niwe padri mpaka nikubali kuwa askofu na huku kumbe wito wangu ni siasa?

“Itakuwa namsaliti hata yule aliyenipa wito huu. Tuchambue yale yanayohusu imani yetu katika ule waraka. Yale ambayo moja kwa moja yanahusu imani yetu Katoliki na tuyashike tuyazingatie kwa dhati kabisa.

“Lakini yale ya kuanza kusema Serikali ya awamu ya tano inagandamiza uhuru inafanya nini… wewe Askofu uhuru wa kisiasa umeujua wapi? Umeujuaje? Na mambo ya ndani ya kisiasa huyajui na bado uje kutamka… nadhani tumeelewana.

“Yapo yaliyo mema mazuri kabisa katika waraka ule, ingawaje sikujua kama yameandikwa, lakini siwezi kukataa yaliyo mema kwa sababu sikujua.

“Yanaendelea kuwa mema mpaka kesho na keshokutwa. Lakini yale ambayo yanachanganya dini na siasa hayo siwezi kuyakubali.” 

2009: VITA YA UFISADI

Wanaomfahamu Askofu Pengo, wanasema misimamo katika jambo analoliamini yeye kabla ya mtu mwingine yeyote ni ya siku zote na mfano mmojawapo ni matamko yake ya siku za nyuma.

Tamko mojawapo ni lile alilolitoa mwaka 2009 wakati wa Jubilee ya Miaka 75 ya Shirika la Masista wa Bibi Yetu Kilimanjaro iliyokwenda sambamba na harambee ya kuchangia Shule ya Sekondari Henry Gogat iliyopo wilayani Rombo. 

Wakati huo, Askofu Pengo aliibuka na kutangaza mapambano mapya dhidi ya mafisadi huku akidai nchi imeoza na kamwe kanisa halitakaa kimya na kulea hali hiyo.

“Sisi viongozi wa dini hatuwezi kunyamaza huku tukiona nchi inaendelea kuozeshwa na viongozi wasiozingatia maadili ya utawala bora. Lazima tukemee kwa nguvu zote,” alisema wakati huo vita ya ufisadi ikiwa imepamba moto. 

Aliwataka wananchi kushirikiana na viongozi wa dini kuwafichua mafisadi na kuwakemea popote pale walipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles