Marekani yaipa sharti la kuiondolea Zimbabwe vikwazo

0
905

HARARE, ZIMBABWE

IWAPO Zimbabwe itaitii na kutekeleza kikamilifu katiba yake ya 2013, vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hilo vitaondolewa, Balozi wa Marekani nchini hapa, Brian Nichols amesema.

“Mtu wa kawaida nchini Zimbabwe ana haki ya kuishi bila hofu ya ukandamizaji na ninadhani kuongeza kuheshimu haki za binadamu ni kipaumbele kikuu cha serikali yangu,” alisema Balozi Nichols.

“Iwapo Zimbabwe, kama taifa itatekeleza kikamilifu katiba yake ya 2013, ambayo itatatua masuala ya vikwazo na serikali tayari imeonesha dhamira ya mageuzi. Ikitokea kweli, vikwazo vitaondoka.”

Nichols pia alifichua kuwa Marekani ipo tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa bunge na ngazi yoyote ya serikali katika kurekebisha sheria 27 katika Katiba.

Marekani iliiwekea Zimbabwe vikwazo mwaka 2002 na 2003 kwa kile ilichoita ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, kukwaza demokrasia na kukithiri kwa rushwa katika utawala wa Rais Robert Mugabe.

Vikwazo dhidi ya utawala huo, vijulikanavyo kama ZIDERA, vimekuwa vikifufuliwa mara kwa mara tangu hapo huku Serikali ya Chama tawala cha Zanu PF ikivilaumu kusababisha matatizo ya kiuchumi.

Mugabe aliangushwa na jeshi Novemba mwaka jana na mshirika wake aliyegeuka hasimu Emmerson Mnangagwa akawa rais akiwa na matumaini vikwazo vitaondolewa, lakini Marekani ilivifufua.

“ZIDERA ilirekevishwa mwaka 2018 na ni mwongozo wa kushawishi mageuzi, ambayo watu wengi nchini Zimbabwe wamekuwa wakiyataka,” Nichols alisema.

“Hayo ni pamoja na haki ya kutoa maoni, chaguzi za kidemokrasia, ukuaji wa sekta binafsi, uwezo wa kununua na kuuza ardhi – ni mambo ZIDERA inayozungumzia bila kusahau kuchukuliwa hatua kwa matendo ya nyuma ya haki za binadamu.”

Hata hivyo, alisema Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zimbabwe.

“Tunatarajia ushirikiano na Zimbabwe na kuisaidia kukabiliana na magumu iliyo nayo, ukuaji wa uchumi, maendeleo, afya, elimu, suala la uharibifu wa mazingira na tuna matumaini ya kuunda mazingira mazuri zaidi kidemokrasia na jamii iliyostawi,” alisema.

“Uzuri ni kwamba kuna dhamira ya Rais Emmerson Mnangagwa na upinzani wa MDC Alliance ya uwapo wa mabadiliko Zimbabwe na tumefahamishwa kuwa ahadi hizo zitatekelezwa.”

Aliongeza; “Kuchaguliwa kwa baraza jipya la mawaziri ni mwanzo mzuri. Nilifurahi kukutana na Waziri wa Ulinzi na Veterani wa Vita Oppah Muchinguri asubuhi hii (juzi) na tulikuwa na mazungumzo mazuri ya kutia moyo.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here