NEW YORK, Marekani
SERIKALI ya China na Marekani zimeafikiana kutowekeana ushuru mpya wakati nchi hizo zikifanya majadiliano kufikia makubaliano ndani ya siku 90.
Makubaliano hayo yalifikiwa jana mjini hapa kati ya Marais Donald Trump na Xi Jinping.
Ikulu ilieleza kuwa katika makubaliano hayo, Rais Trump alikubali kutopandisha ushuru kwa hadi asilimia 25 kwa bidhaa za China zenye thamani ya dola bilioni 200 ifikapo Januari mosi kama ilivyokuwa imetangazwa awali, baada ya China kukubali kununua kiwango kisichotajwa lakini muhimu, cha bidhaa za kilimo, nishati, viwandani na nyingine.
Mapatano hayo yaliyofikiwa baada ya chakula cha usiku kilichodumu kwa zaidi ya saa mbili, yanatoa muda kwa mataifa hayo mawili kushughulikia tafauti zao katika mzozo unaohusu kampeni ya ushari ya China kuchukua nafasi ya udhibiti wa Marekani wa nyanja ya teknolojia.
“Ni makubaliano ya kushangaza,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye ndege ya Air Force One.
“Tutakachofanya ni kusimamisha mpango wa kupandisha ushuru. China itazungumza, China itaondokana na ushuru. China itakuwa inanunua bidhaa nyingi kutoka kwetu,” aliongeza Rais Trump.
Ikulu ilisema pia kwamba China imeacha milango wazi kuweza kuidhinisha makubaliano ambayo awali hayakuidhinishwa ikiwa yatalazimika kuwasilishwa tena.
Julai, Qualcomm ambaye ndiye mtengenezaji mkubwa duniani wa vifaa vya kuhifadhi kumbukumbu katika simu za kisasa, iliachana na mpango wa dola bilioni 44 wa kununua vipitishi vya umeme kutoka NXP, baada ya kushindwa kupata idhini ya mamlaka ya udhibiti ya China, na kuwa mwathirika wa ngazi ya juu wa mgogoro wa biashara kati ya China na Marekani.
Ilisema ikiwa makubaliano kuhusu masuala ya biashara, ikiwemo uhamishaji wa teknolojia, vikwazo visivyo vya kodi, wizi wa mtandaoni na kilimo, hayajafikiwa na China katika siku 90, kwamba pande zote mbili zinakubaliana ushuru wa asilimia 10 utapandishwa hadi asilimia 25.
Awali, Rais Trump aliweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za thamani ya dola bilioni 200 kutoka China Septemba mwaka huu na China ilijibu kwa kuweka ushuru wake.
Trump pia ametishia kuongeza ushuru kwa bidhaa nyingine za China zenye thamani ya dola bilioni 267.