31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Mapya kijiji cha mauaji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa

Na RAMADHAN HASSAN,CHAMWINO

SIKU chache baada ya wakazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kuwaua watafiti watatu wa Kituo cha Udongo na Maendeleo cha Selian Arusha, mapya yameibuka.

Taarifa zaidi zilizopatikana kijijini hapo na kijiji jirani zinasema wananchi wa kijiji hicho waliwaua watafiti hao baada ya kuwahusisha na mmoja wa wafanyabiashara maarufu kijijini hapo (jina tunalo) ambaye amekuwa akihusishwa na vifo vya baadhi ya wakazi wa kijiji hicho.

Katika tukio hilo lililotokea Oktoba mosi mwaka huu, wakazi wa kijiji hicho waliwaua Watafiti,  Theresia  Ngume, Jafari Mafuru na dereva wao, Nikas Magazine kwa kuwahisi kuwa ni majambazi.

Awali ilielezwa kuwa watafiti hao waliuawa wakihisiwa kuwa ni wanyonya damu.

Lakini akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mvumi Mission, Kenneth Chiute, alisema mauaji hayo yanaweza kuwa yamechangiwa na uzembe wa polisi kutomchukulia hatua mfanyabiashara huyo anayedaiwa kuhusika na vifo vya baadhi ya wakazi wa vijiji vya Iringa Mvumi na Mvumi Mission.

Katika mazungumzo hayo, Chiute alikuwa na mjumbe wa Serikali ya kijiji hicho, Hamisi Chibago.

“Vimetokea vifo vya watu wanane katika vijiji hivi viwili. Wa kwanza kuuawa alikuwa ni Nguha Msilee ambaye alikuwa mchungaji.

“Huyu aliokotwa akiwa amekatwa mapanga mabegani na alipofikishwa katika Hospitali ya Mvumi Mission alifariki dunia.

“Tukio jingine ni la Fredrick Mlowezi ambaye ni rafiki wa mfanyabiashara huyo muuaji. Mlowezi alikamatwa na wananchi akimpiga Sarah Mbogoni na kumuua kwenye kisima cha maji katika Kijiji cha Mvumi.

“Mlowezi alipokamatwa na kupigwa, alimtaja mfanyabiashara huyo  kwamba ndiye aliyemtuma kufanya mauaji hayo.

“Baada ya matukio hayo ambako mfanyabiahara huyo hakuchukuliwa hatua, wakazi wa Mvumi Misheni walichoma moto nyumba zaidi ya sita za mfanyabiahara huyo.

“Baadaye, Serikali ya kijiji ilimfukuza mfanyabiashara huyo kutokana na matukio hayo, lakini baada ya siku chache, alirudi akiwa na barua kutoka kwa mmoja wa vigogo wa Wilaya ya Chamwino (jina tunalo) akimtambulisha kuwa yeye ni mkazi halali wa kijiji hicho.

“Jambo hilo liliwakera wananchi kwa vile  matukio ya kuuawa watu yaliongezeka kijijini hapo,” alisema Chiute.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Serikali ya Kijiji cha Mvumi Mission, watu walianza kuuawa katika vijiji hivyo   mwaka 2012, lakini hatua hazichukuliwi.

Aliwataja wengine waliofariki dunia na mfanyabiashara huyo kuhusishwa kuwa ni Sifuni Chiume, aliyeuawa mwaka 2015 katika shamba la Shule ya Msingi Mvumi, Tatu Mapepele mkazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi aliyeuawa akitokea Mnadani, Julai mwaka huu.

Wengine ni Hassan Allan mwenye umri wa miaka sita ambaye alifariki dunia wiki moja iliyopita wakati akichota maji katika Kijiji cha Mvumi Mission.

“Nilikwenda kuiona maiti ya mtoto huyo akiwa mochwari (chumba cha maiti)nikakuta ina michubuko kidevuni na kifuani.

“Wengine waliouawa katika vijiji vyetu ni Joseph Mabwaya aliyefariki dunia mwaka 2014 na Richard Mzungu ambaye alikatwakatwa vipande.

“Kwa hiyo, ulifika wakati wananchi wanawaogopa wageni na inawezekana waliouawa ni kutokana na hofu iliyotanda,” alisema mwenyekiti huyo.

Michael Joel, mkazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi, aliungana na Chiute na kusema watafiti hao waliuawa baada ya kuhusishwa na mfanyabiashara huyo.

“Watu wote hapa kijijini wanajua mhusika wa matukio ya ujambazi ni huyo mfanyabiashara na walikuwa wamempania kweli kweli.

“Sasa wakati mchungaji anatoa tangazo kuwa kuna majambazi, watu wote wakajua ni huyo jamaa na walipokwenda eneo la tukio, walijua ni washirika wa mfanyabiashara huyo ndiyo maana hawakutaka hata kusikiliza lolote kutoka kwao,” alisema Joel.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alipozungumza na MTANZANIA juu ya mfanyabiashara huyo, alisema hana taarifa zake ingawa aliahidi kufuatilia taarifa hizo.

“Ndiyo kwanza unanitajia jina lake. Ila nasikia watu wengi wamekimbia makazi yao lakini waambie popote watakapoenda, lazima tutawakamata kwa sababu  hakuna aliye juu ya sheria,” alisema Kamanda Mambosasa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza waliohusika na mauaji hayo wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana alipozungumza na waandishi wa habari   mjini Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles