24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kabila atoa matumaini Bandari Dar

Rais Dk. John Magufuli (kulia), akimshuhudia mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, akizindua jiwe la msingi la Jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (One Stop Centre) jijini Dar es salaam jana.
Rais Dk. John Magufuli (kulia), akimshuhudia mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, akizindua jiwe la msingi la Jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (One Stop Centre) jijini Dar es salaam jana.

Na Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Jospeh Kabila, ametoa matumani kwa kueleza kuwa Serikali na wafanyabishara wa nchi yake, wataendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

Mbali na hilo, ameahidi  nchi yake itatumia bomba la mafuta linalojengwa mkoani Tanga, kwa ajili ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert nchini DRC.

Uamuzi huo aliutangaza jana mbele ya mwenyeji wake, Rais Dk. John Magufuli katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Alisema wanachukua hatua hiyo,baada ya Serikali ya Tanzania kufanya maboresho bandarini.

Rais Kabila,  aliahidi kushirikiana na Tanzania katika biashara kwa kuhakikisha kuwa nchi yake inatumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yake yote, huku Serikali ya Tanzania ikimwahidi kutoa msamaha  ‘Grace Period’ wa siku 14 hadi 30 bandarini kwa mizigo hiyo.

Rais Kabila aliweka wazi kuwa awali walisitisha kupitisha mizigo katika bandari hiyo kutokana na kodi, urasimu na upotevu wa mizigo, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yameshughulikiwa na Serikali ya awamu ya tano.

Alisema nchi yake, imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kupunguza vituo vya ukaguzi wa mizigo inayotoka bandarini kwenda DRC.

“Hali ya kupunguza vituo vya ukaguzi itarahisisha wafanyabiashara kufikisha mizigo kwa wakati na kupunguza gharama za usafirishaji” alisema Rais Kabila.

Pia alimwahidi Rais Magufuli kuwa atahakikisha anafanya mabadiliko makubwa katika mamlaka ya kodi ya DRC ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wafanyabiashara wengi kuhusu urasimu na ukiritimba.

Akizungumzia kuhusu suala la amani mashariki mwa DRC,Rais Kabila  alisema hali si kama inavyoripotiwa katika vyombo vya habari vya nje, licha ya kuwapo vikundi vichache vya waasi vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao.

Aidha alilishukuru Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) chini ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kutunza amani ya nchini kwake.

Pia Rais Kabila amefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali, kwani bandari hiyo ni tegemeo kwa usafirishaji wa mizigo ya Kongo mashariki na sehemu nyingine za nchi hiyo.

Kutokana na hali hiyo aliahidi kuwahamasisha wafanyabiashara wa Kongo kuitumia Bandari ya Dar es Salaam na kwamba Serikali yake itachukua hatua za kurekebisha kasoro zinazolalamikiwa na wafanyabiashara dhidi ya maofisa wa forodha wa Kongo waliopo hapa nchini.

Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga itakuwa ni fursa nyingine kwa nchi yake kutumia bomba hilo kusafirisha mafuta yake iliyoyagundua katika Ziwa Albert upande wa Kongo na pia juhudi zinazoendelea kupata mafuta katika Ziwa Tanganyika kama njia ya kuimarisha ushirikiano muhimu.

Akizungumzia hali ya usalama nchini Kongo, Rais Kabila alisema asilimia 97 nchi hiyo ina usalama na kwamba ni maeneo machache tu ya mashariki mwa Kongo ndiko kuna vikundi vinavyoendesha vurugu.

“Mheshimiwa Rais Magufuli hivi karibuni tutaanza mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu nchini Kongo, na lengo letu ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba,” alisema

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kabila aliweka jiwe la msingi la jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) lililopo kando ya Bandari ya Dar es Salaam na jioni ya jana alishiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Dk. Magufuli.

Awali akizungumza  katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli alimhakikishia Rais Kabila kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa za kuimarisha huduma katika Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza vizuizi vya barabarani hadi kubaki vitatu ili nchi ya Kongo na nchi nyingine za kusini na magharibi mwa Tanzania ziitumie bandari hiyo bila vikwazo.

Alisema Tanzania imeweka malengo ya kuhakikisha uchumi wake unakua kwa asilimia 7.2 na kutokana na hali hiyo anawakaribisha wafanyabiashara wa Kongo kuja kuwekeza Tanzania na wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kuwekeza nchini Kongo.

“Mheshimiwa Rais Joseph Kabila, takwimu zinaonyesha nchi zetu zinafanya biashara kubwa, mwaka 2009 tulifanya biashara iliyofikia Sh bilioni 23.1 na imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka na hivi sasa tunafanya biashara yenye thamani ya Sh bilioni 393.6 kwa mwaka.

“Mimi ningependa kuona sisi ndugu na majirani tunafanya biashara zaidi, wafanyabiashara wa Kongo waje Tanzania kuwekeza na Serikali yangu itawaunga mkono,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia mikakati ya kuimarisha mawasiliano ya barabara na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa ‘Standard Gauge’, Rais Magufuli alisema Serikali imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi huo na kwamba hatua hiyo itarahisisha zaidi usafirishaji wa mizigo ya kwenda na kutoka Kongo kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga,Rais Magufuli  alisema matarajio ya Kongo ambayo pia imegundua mafuta Ziwa Albert, itatumia bomba hilo kama ambavyo Tanzania pia inatarajia kulitumia kutokana na tafiti kuonesha uwepo wa mafuta katika maeneo ya ziwa Eyasi na Ziwa Tanganyika.

Rais Kabila yupo nchini kwa ziara ya siku tatu ambayo inamalizika leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles