24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mapya corona

 MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM

WAKATI wagonjwa wa corona nchini wakifikia 94, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, amekabidhi vifaa mbalimbali vikiwamo vitakasa mikoni na barakoa ili kusaidia mapambano dhidi ya corona jijini Dar es Salaam.

Rostam alikabidhi msaada huo jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ikiwa ni sehemu ya ahadi yake kwa Waziri Mkuu wiki iliyopita ya kutoa Sh bilioni moja ya vitakasa mikono kwaajili ya daladala za jiji la Dar es Salaam na Zanzibar.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Rostam alisema pamoja na vitakasa mikono hivyo na barakoa alizotoa, ameongeza mchango wake kwa kutoa barakoa 70,000 kwa hospitali mbalimbali kwa wauguzi, madaktari na manesi ambao ndiyo wako hatarini kuliko mtu yeyote.

Vitu vingine alivyotoa ni pamoja na galoni 6,000 za lita tano za vitakasa mikono na mashine maalumu za kupuliza dawa ya kupambana na maambukizi ya virusi hivyo, huku akiwaasa Watanzania kuchukua tahadhari ya virusi hivyo sasa kuliko wakati mwingine. 

“Janga hili halipo Tanzania tu, lipo sehemu zote duniani na kama sote tunavyofahamu, ugonjwa huu hauna tiba na tiba pekee ni kujihami ili usiupate, namshukuru pia Makonda kwa kutoa tahadhari ya namna ya kujihami.

“Machi 22 mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli katika ‘speech’ (hotuba) yake kwa taifa kuhusu maradhi haya, alitupa tahadhari kwamba pamoja na kuendelea kuchapa kazi, lazima tuchukue tahadhari ya kunawa mikono mara kwa mara, kuangalia wakati wa kushika vitasa unatakiwa kunawa.

“Ni wazi kwamba tahadhari hizo tuzingatie kuliko wakati wowote wa kipindi cha wiki moja au wiki mbili zilizopita,’’alisema Rostam.

Akizungumza namna barakoa inavyofanya kazi, Rostam alisema inaweza kukuepusha na maradhi mengi, na kwamba jambo hilo linaweza kufanyika kwa kila mtu ambapo unaweza kuchukua nguo yako iliyochakaa ukatengeneza.

Alisema amezungumza na madktari wakamwambia ni vema kuvaa barakoa wakati unakwenda kwenye msongamano wa watu lakini pia watu wanaweza kutengeneza wenyewe si lazima kununua madukani.

“Leo hii kwa mara ya kwanza nimevaa hii kitu inaitwa barakoa na hii nimetengenezewa na mama yangu, hivyo hakuna haja ya kwenda kununua dukani.

“Unachotakiwa kufanya unachukua shuka au foronya unakata kitambaa unakunja mara mbili, unaitengenezea kamba, tayari unakuwa umetengeneza barakoa.

 “Barakoa inapunguza maambukizi mengi, kuvaa barakoa ni muhimu, hasa wakati unakwenda kwenye msongamano wa watu.

“Pamoja na hizi ‘sanitizer’ ambazo nimetoa, hii nimeongeza mchango wangu kwa mahospitali na wauguzi wake, najitolea barakoa 70,000 ambazo tayari ziko hapa mbele yetu ili wahudumu na madaktari na manesi ambao ndio wanahatarisha maisha yao kuliko mtu mwingine yeyote wawe wamejikinga na maradhi haya,” alisema Rostam.

Vilevile aliwaomba wafanyabiashara wenzake kuisaidia Serikali kwa kutoa michango yao ili kupambana na ugonjwa wa corona.

“Kama kawaida yangu ningependa kuwaomba wafanyabiashara wenzangu hili si jukumu la serikali pekee, wafanyabiashara wengi duniani wameishaidia serikali, tumeona Amazon wamejitolea.

“Si lazima uwe mfanyabiashara mkubwa, hata mfanyabiashara wa duka unaweza kuweka ndoo ya maji dukani na ukaweka vitakasa mikono kwa wafanyakazi unaweza kuokoa maisha ya watu.

 “Natoa wito kwa wafanyabisahrawa wakubwa na wadogo kwa kikasi tunachoweza tusaidiane kuisaidia serikali mzigo huu mzito ili wananchi wengi zaidi wasipate maambukizi haya,” amesema Rostam.

MAKONDA

Kwa upande wake, Makonda alisema vifaa hivyo ambavyo ni mashine 25 kubwa za kupulizia dawa mwili mzima, vitakasa mikono na barakoa vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 600, vitasambazwa kwenye daladala ili abiria waweze kujitakasa kabla ya kupanda ndani ya usafiri huo.

“Tunamshukuru Rostam kwa kuamua kuwagusa wananchi katika kipindi hiki kigumu, kazi hii si rahisi hasa kwa sekta ya taifa kwa sababu watu wengi wameingiwa na hofu.

“Madaktari wetu kwa kweli wanafanya kazi ngumu na wanastahili kutiwa moyo, tuwaombee madaktari wafanye kazi hii bila woga, naomba sana tuendelee kuwatia moyo na kuwaombea madaktari.

“Kaka yangu Rostam anastahili kuombewa yeye na watu wa moyo wa aina yake ili kuendelea kuwagusa Watanzania walio wengi zaidi, utoaji si utajiri ila ni moyo, na hapa mmesikia ametoa yeye kama yeye, Taifa Gas imetumika kama platform kufikisha huo mzigo, lakini yeye binafsi ameguswa.

“Vifaa hivi vina zaidi ya Sh milioni 600… kwa niaba wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tunakushukuru maana moyo wa namna hii si wa kawaida,” alisema Makonda. 

Aliwataka abiria wanapoingia kwenye vyombo vya usafiri ni lazima wapake vitakasa mikono na pale mtu anapokaidi kondakta amkabidhi askari wa usalama barabarani.

“Abiria mnapoingia kwenye vyombo vya usafiri, unapoambiwa paka ‘sanitizer’ ni lazima na ukiwa hutaki tutakukamata na makondakta waripoti wale ambao wanakaidi.

“Ukiona mtu kama Rostam anatoa zaidi ya bilioni moja si kwamba ana hela sana, ni kwa sababu anatamani kuona Watanzania wasife kwa janga la corona, lakini wewe unayesaidiwa hutaki kujilinda,” alisema Makonda.

TAIFA GAS 

Mkurugenzi wa Taifa Gas, Hamisi Ramadhani alisema mchango huo umetolewa na Rostam kama yeye binafsi, lakini peke yake asingeweza kufanya ugawaji, hivyo Taifa Gas imetumika kufanya kazi hiyo.

 “Taifa Gas tumehusika hapa kwa sababu sisi tuna watu na uongozi, hivyo tunasaidiana pamoja naye kuhakikisha kwamba mchango wake huu unawafikia wahusika… hivyo sisi ni watendaji tu kuhakikisha vifaa hivi vinafika inapotakiwa, lakini katoa yeye binafsi,” alisema Ramadhani.

WAGONJWA 94

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, jana alitoa taarifa ya kuongezeka kwa wagonjwa wapya sita wa corona na kufanya nchi nzima sasa kuwa na watu 94 waliothibitika kuwa na virusi hivyo.

Juzi pia Hamad Rashid alitoa taarifa ya wagonjwa wapya sita visiwani humo na kufanya waliokuwa na virusi hivyo kufika 18 hadi juzi, huku aliowatangaza jana wakipandisha idadi hiyo hadi 24.

Katika taarifa yake ya jana, Hamad Rashid alisema wagonjwa hao ni wanaume wakazi wa Zanzibar.

Alisema wa kwanza ni mwanaume mwenye miaka 30 mkazi wa Kibweni, mwanaume (27) mkazi wa Magogoni, mwanaume (28) mkazi wa Kwarara, mwanaume (58) mkazi wa Kilimahewa Juu, mwanaume (23) mkazi wa Amani na mwanaume (55) mkazi wa Kidoti. 

Hamad Rashid alisema pia wagonjwa wote hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za karibuni na wamelazwa kwenye vituo vya kuhudumia wagonjwa wa corona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles