CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, kimefanya uchaguzi wa kuziba nafasi za uongozi wa chama hicho mkoani humo.
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa zamani wa Longido, Michael Laizer, amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa CCM wa mkoa kwa kura 515.
Mkutano huo pia umemchagua Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe kuwa katibu mwenezi.
Uchaguzi huo mdogo ulifanyika kutokana na kuhama chama kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa, Onesmo ole Nangole ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Longido kwa tiketi ya Chadema.
Mwingine aliyehama ni aliyekuwa Katibu wa Itikadi na uenezi, Isack Joseph ambaye hivi sasa ni Diwani wa Kata ya Monduli Mjini na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli kwa tiketi ya Chadema.
Mdoe alishinda kwa kura 36 huku mpinzani wake Veraikunda Urio, akipata kura 12 katika kura zilizorudiwa awamu ya pili.
Katika awamu ya kwanza, ingawa Mdoe aliongoza lakini hakufikisha nusu ya kura zilizotakiwa.
Akimtangaza Laizer, Msimamizi wa Uchaguzi huo Steven Wasira, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema alipata kura 515 kati ya kura 861 zilizopigwa, akifuatiwa na Emanuel Makongoro aliyepata kura 338 huku kura nane zikiharibika.
Nafasi hiyo ilikuwa na wagombea watatu akiwamo John Pallangyo aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambaye alipata kura 154, Laizer kura 409 na Makongoro kura 330 kati ya kura 903 zilizopigwa