27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Hofu ya Mabadiliko makubwa Polisi

IGP Mangu*Waziri wa Mambo ya Ndani atoa tamko, IGP Mangu aguswa

NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM

HOFU ya mabadiliko makubwa imetanda ndani ya jeshi la polisi, huku ikielezwa kuwa huenda yakamgusa Mkuu wa jeshi hilo, IGP Ernest Mangu, MTANZANIA imebaini.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata Dar es Salaam kutoka kwenye vyanzo vyake zilieleza kwamba IGP Mangu ni miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu wa jeshi hilo ambao huenda wakakumbana na mabadiliko hayo.

“Mabadiliko makubwa yanakuja na mmoja waoanayeguswa ni bosi wetu, IGPMangu.

Unajua ndani ya jeshi hili kuna mambo yanaonekana hayaendi vizuri hasa matukio ya ujambazi ambayo yamekuwa yakiendelea kila kukicha katikamaeneo mbalimbali nchini.

“Hata juzi umeona IGP Mangu kafanya mabadiliko ya makamanda wa polisi wa mikoa na wakuu wa vikosi kwa nia ya kuboresha utendaji ambao unaonekana kulegalega,” kilisema chanzo chetu.

Mtoa habari huyo alisema pamoja na hatua hiyo ya IGP Mangu, bado kuna baadhi ya viongozi wa juu nchini ambao wamekuwa hawaridhishwi na matukio kadhaa ikiwamo kurejea kwa kasi matukio ya ujambazi nchini.

Kutokana na hali hiyo kwa wiki ya pili sasa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amekuwa akifanya vikao na wakuu na watendaji kadhaa wa Jeshi la Polisi pamoja na wa idara zilizoko chini ya wizara hiyo.

Suala jingine linaloelezwa ni kulegalega kwa utendaji wa Jeshi la Polisi, hali ambayo imesababisha Waziri Kitwanga aombe msaada wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kudhibiti vitendo vya uhalifu ukiwamo ujambazi.

“Ni aibu na fedheha kubwa… kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini baada ya majambazi kuvamia benki ya Access kule Mbagala, JWTZ wameombwa washiriki kukomesha vitendo hivi… ni fedheha kwa jeshi la polisi.

“JWTZ kazi yao kubwa ni kulinda mipaka ya nchi wakati wote lakini sasa hatua ya kuanza kupambana na majambazi ni wazi polisi wameshindwa kazi ambayo ndiyo jukumu lao la msingi,” kilisema chanzo chetu.

IGP Mangu aliteuliwa kushika wadhifa huo Desembav30 mwaka 2013 na Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Alichukua nafasi ya mkuu wa jeshi hilo aliyestaafu utumishi wa umma, IGP Said Mwema.

Kabla ya uteuzi huo, Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Inteligensia ya Jinai katika jeshi hilo.

KAULI YA WAZIRI

Kutokana na taaarifa za mabadiliko hayo, MTANZANIA ilimtafuta Waziri Kitwanga ambaye alisema ameshtushwa na watu wanaosambaza taarifa za kuondolewa IGP Mangu, wakati yeye mwenyewe au Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk. John Magufuli, hana taarifa hizo.

“IGP haondolewi kwenye nafasi yake, Rais Magufuli ana imani naye kutokana na

utendaji kazi wake mzuri…sijui kwa nini watu wanasambaza taarifa za uongo maana maneno haya nimeyasikia, naomba uandike haya ninayoyasema.

“Mimi waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani sina taarifa yoyote juu ya kuondolewa IGP, Rais ana imani naye, lazima angenishirikisha katika suala hili nyeti, tungejadiliana ili kuiona nini cha kufanya ila hayo ni maneno ya kusikia tu.

“Kutokana na utendaji kazi wake ndiyo maana tumekuwa tukishirikiana vizuri kuboresha jeshi letu, ndiyo sababu hata juzi mmeona tumefanya mabadiliko makubwa ya makamanda wa polisi wa mikoa na wakuu wa vikosi…sasa hili linatoka wapi?” alihoji Waziri Kitwanga.

Alisema mpaka sasa Rais Magufuli hajafikiria kufanya mabadiliko kwenye nafasi hiyo.

“Unajua Rais ana uamuzi wa mwisho.

Kama waziri au IGP ameshindwa kutekeleza wajibu wake sawasaswa atamuondoa, hata kama ni mimi nitaondolewa kwa mamlaka ya uteuzi…lakini mpaka sasa majukumu tuliyokabidhiwa yanaendelea vizuri,”alisema Waziri Kitwanga.

IGP

Juzi IGP Mangu alifanya mabadiliko kwa baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa na vikosi. Katika mabadiliko hayo alimteua Kamishina Msaidizi wa Polisi, Mihayo Msikhela kuwa Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kabla ya Msikhela kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya Godfrey Nzowa, alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam juzi na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, ilisema mabadiliko hayo ni ya kawaida kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za jeshi hilo.

Pia IGP Mangu alimhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Leonard Paul, kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles