Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, amewasili mkoani Arusha ambako pamoja na mambo mengine, ataongoza mkutano wa 17 wa wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo utafanyika kesho kutwa mjini hapa.
Dk. Magufuli aliwasili mjini Arusha jana ambako katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alilakiwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali.
Rais Magufuli kwa sasa ndiye Mwenyekiti Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kabla ya kuongoza kikao hicho, Rais Magufuli anatarajiwa kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wakuu wa EAC.
Machi 3 mwaka huu, yeye pamoja na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili – Taveta – Voi inayoziunganisha Tanzania na Kenya.
Barabara hiyo ni sehemu ya miradi ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekelezwa na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.