23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mapendekezo ya CAG yasivyotekelezwa

MAREGESI PAUL -DODOMA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, ameeleza jinsi mapendekezo yake ya kikaguzi ambavyo yamekuwa yakitekelezwa na Serikali kwa miaka iliyopita.

Profesa Assad aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.

“Sura hii inawasilisha tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo yangu yaliyotolewa miaka iliyopita pamoja na hati za ukaguzi zilizotolewa kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Katika ukaguzi wangu nilifanya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya kiukaguzi yaliyotolewa miaka iliyopita na kubaini kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuyafanyia kazi.

“Tathimini ya utekelezaji wa mapendekezo hayo inaonyesha kuwa kati ya mapendekezo 350 yaliyotolewa miaka iliyopita, mapendekezo 80 ambayo ni sawa na asilimia 22.9 yametekelezwa kikamilifu.

“Mapendekezo 80 ambayo ni sawa na asilimia 35.4, utekelezaji wake bado unaendelea. Hata hivyo, mapendekezo 72 ambayo ni sawa na asilimia 20.6, utekelezaji wake haujaanza na mapendekezo 74 ambayo ni sawa na asilimia 21.1 yamepitwa na wakati.

“Kwa kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo bado uko chini, ninapendekeza Serikali iongeze jitihada katika kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti zangu,” alisema Profesa Assad.

HATI ZA UKAGUZI

Akizungumzia hati za ukaguzi zilizotolewa kwa mwaka wa fedha 2017/18, Profesa Assad alisema kuwa alitoa hati 548 za ukaguzi.

“Katika ukaguzi wa hesabu nilioufanya kwa Serikali Kuu na taasisi zake, mamlaka ya Serikali za Mitaa na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2017/18 nimetoa jumla ya hati za ukaguzi 548.

“Kati ya hizo, hati zinazoridhisha ni 531 (sawa na asilimia 97), hati zenye shaka ni 15 (sawa na asilimia 2.6) na hati mbaya ni moja (sawa na asilimia 0.2.

“Katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyokuwa inatekelezwa na taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2017/18, nilitoa jumla ya hati za ukaguzi 469.

“Katika hati hizo 469, hati zinazoridhisha ni 455 ambazo ni sawa na asilimia 97 na hati zenye shaka ni 14, sawa na asilimia tatu.

“Vile vile, katika ukaguzi wa vyama vya siasa kwa mwaka wa fedha 2017/18, nilitoa hati za ukaguzi kwa vyama 14.

“Kati ya hivyo, vyama vitatu vilipata hati zinazoridhisha, vyama vinne vilipata hati zenye shaka, vyama viwili vilipata hati zisizoridhisha na vyama vitano vilipata hati mbaya,” alisema Profesa Assad.

Alivitaja vyama hivyo vya siasa vilivyopata hati mbaya na hati zisizoridhisha na hati zake kwenye mabano ni ADA-TADEA (hati mbaya), NRA (hati mbaya), UMD (hati mbaya), AAFP (hati mbaya), SAU (hati mbaya), CHAUMMA (hati isiyoridhisha) na NLD (hati isiyoridhisha).  

DENI LA SERIKALI

Katika maelezo yake, Profesa Assad alisema hadi kufikia Juni 30, 2018, deni la Serikali lilikuwa Sh trilioni 50.92 ambapo deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 14.73 na deni la nje Sh 36.19.

UDHAIFU MALIPO YA MAFAO

Katika eneo la malipo ya mafao, Profesa Assad alisema katika mwaka wa fedha 2017/18 alikagua majalada 2,868 ambapo 2,814 yenye jumla ya Sh bilioni 165.44 yaliidhinishwa kwa ajili ya malipo na 54 yalirudishwa kwa maofisa masuuli husika kwa ajili ya masahihisho.

“Kati ya majalada 2,868 yaliyokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2017/18 mafao ya wastaafu 295 yalibainika kukokotolewa kimakosa.

“Kati ya hayo, majalada 172 yalibainika kuwa na ziada ya malipo ya Sh milioni 577.32 huku majalada 123 yakiwa na upungufu wa malipo ya Sh milioni 294.35.

“Aidha, nilibaini ucheleweshaji mkubwa wa waajiri katika maandalizi na uwajibikaji wa majalada ya wanufaika wa mafao kwa ajili ya ukaguzi.

“Ucheleweshaji huo niligundua kuwa ulitokana na waajiri kutotoa kipaumbele kwenye usimamizi wa uandaaji wa mafao, hivyo kuwanyima wastaafu haki yao ya kupata mafao kwa wakati,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles