22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mapambano dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia na utoro shuleni yalivyoleta matokeo chanya

Na Clara Matimo, Mtanzania Digital

Matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Kilimanjaro yametajwa kupungua kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita kutokana na jitihada mbalimbali za utoaji elimu uliofanywa na mashirika yaliyojikita kutetea haki za binadamu na msaada wa kisheria.

Hayo yalielezwa wakati wa ziara ya kutathmini mwaka mmoja  wa mradi wa Mwanamke Imara unaoratibiwa na Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wenye thamani ya Sh bilioni 9 katika mikoa hiyo.

Akieleza mafanikio katika Wilaya ya Rombo, Mkuu wa Upepelezi Makosa ya jinai Vicent Msami alisema matukio ya ubakaji yamepungua kutoka 85 hadi 59, kulawiti 13 hadi 6, shambulio la aibu 31 hadi 28, kujaribu kubaka matano hadi sifuri na mimba kwa wanafunzi kutoka kesi 28 hadi tisa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2020-2021.

Kaimu Mkurugenzi wa halmasahuri ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Gilbert Ngailo, akiwaeleza waandishi wa habari pamoja na wadau wanaotekeleza mradi wa Mwanamke Imara wenye lengo la kutokomeza aina zote za ukatili wa kijinsia mafanikio waliyoyapata, walipokuwa kwenye ziara ya kutathmini mwaka mmoja tangu uanze kutekelezwa, mradi huo unaratibiwa na Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Alisema mwaka huu zimefunguliwa kesi 27 wakati mwaka jana zilifunguliwa 51 huku akisifu juhudi za wadau mbalimbali kuwezesha jeshi hilo kutoa elimu shuleni, boda boda na makundi mbalimbali ya kijamii na kusaidia kupunguza matukio ya vipigo na kujeruhi, ambapo alilipongeza Shirika la WILDAF lililotoa msaada mkubwa katika usuluishaji wa migogoro ya aina tofautitofauti.

Kaimu Mkurugenzi wa halmasahuri ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Gilbert Ngailo alieleza kabla ya mradi kamati za ugawaji ardhi vijijini zenye wajumbe nane nyingi wanaume walikuwa sita hadi saba, lakini kupitia mafunzo ambayo kamati hizo zimepewa wameanza kubadilika.

Alifafanua kwamba haki za mwanamke upande wa sheria wanawake wameanza kuelewa haki zao hasa kwenye maeneo ya umiliki wa ardhi pamoja na mali nyingine ambazo wametafuta na wenzi wao tofauti na hali ilivyokuwa awali.

 “Mfano katika kata za Lugarawa, Lubonde, Mundindi na Mavanga unakotekelezwa mradi wa Mwanamke imara wameanza kubadilika wanaleta hadi mapendekezo wenyewe namna ya kuunda kamati yao ya ugawaji ardhi na kuomba idadi ya wanawake iongezeke, hii inaonyesha kuna mwamko wamefahamu umuhimu wa mgawanyo wa majukumu,” alisema Ngailo.

Mwakilishi wa dawati la jinsia na watoto kituo cha polisi Igurusi wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya, Mariam Ramadhani, alisema kupitia shule salama klabu ambazo zimeanzishwa na shirika la WILDAF ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mradi imesaidia kupunguza idadi ya malalamiko ya wanafunzi kupewa mimba yaliyokuwa yakiwafikia.

Alieleza kuwa kabla ya kuanzishwa klabu hizo kwa mwezi mmoja walikuwa wanapokea malalamiko 20 lakini baada ya kuanza kwa mradi Septemba mwaka jana wanapokea malalamiko 10 hadi 15 kila baada ya miezi mitatu ambapo klabu hizo zimeleta tija na kusaidia kupunguza utoro shuleni hasa shule za msingi.

Mwalimu Shukuru Joshua mlezi wa shule salama katika shule ya msingi Itamboleo iliyopo Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na Mary Mrosso, mlezi katika shule ya msingi Rima wilayani Rombo mkoa wa Kilimanjaro, walisema uanzishwaji wa klabu hizo umesaidia kupunguza utoro kwani wanafunzi wanafurahia elimu wanayopewa inawasaidia kujua haki zao pia wameondoa uoga kwa walimu na kuwaona ni marafiki zao.

Baadhi ya wanafunzi walionufaika na klabu hizo Masanja Maganga na Nesta Konga wa shule ya sekondari Itambolea walisema mambo yanayofundishwa kwenye klabu hizo walikuwa hawajawahi kufundishwa popote kwani inawasaidia hata wazazi wao na walimu kutambua haki za watoto hivyo sasa wanahudhuria shuleni wakiwa na amani kwani walimu wamekuwa marafiki.

Mratibu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini  kutoka TAWLA, Wakili  Barnabas Kaniki, alisema wameanzisha shule salama club kila wilaya kwa lengo la kuwakutanisha walimu, wazazi na wanafunzi ili kujadili chagamoto ambazo wanafunzi wanakutana nazo lengo ni  kuendelea kutengeneza mazingira salama kwa mtoto akiwa shuleni na nyumbani.

“Klabu hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa mwanamke imara eneo la ukatili wa kijinsia lengo ni kuimarisha mifumo rasmi na isiyo rasmi ili kutoa uelewa kwenye jamii kuhusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia, tunafanya mafunzo na makundi mbalimbali yakiwemo badoboda, walimu na wanafunzi,”alisema Kaniki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles