25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Amana yatoa huduma bure kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Hospitali ya Rufaa ya Amana imetoa huduma za uchunguzi na matibabu ya awali bure kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Dk. Bryceson Kiwelu, akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma za uchunguzi na matibabu katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.

Huduma hizo zilizoanza kutolewa Desemba 7 ni za magonjwa ya saratani ya matiti, njia ya uzazi, kisukari, macho, masikio, kinywa, koo, matatizo ya akili na sonona pamoja, kutoa chanjo ya Uviko 19 pamoja na kukusanya damu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hizo Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Bryceson Kiwelu, amesema wanatambua mchango wa wananchi katika hospitali hiyo ndiyo maana wamewiwa kutoa huduma bure sambamba na kupokea maoni yao kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma.

“Tuna wajibu wa kuwahudumia wananchi wetu na kuhakikisha kwamba huduma ambazo wanazipata zinakidhi viwango vya ubora uliokusudiwa,” amesema Dk. Kiwelu.

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wakisubiri kupatiwa huduma bure na Hospitali ya Rufaa ya Amana katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.

Kiwelu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa amesema wanajivunia kuwa na wataalamu kama vile madaktari wa kawaida, wauguzi wabobezi katika fani mbalimbali, madaktari bingwa wa upasuaji wa kawaida, upasuaji wa kinywa, koo na pua, macho, magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto, magonjwa ya kina mama, akili, wataalamu wa lishe na ustawi wa jamii.

Aidha amesema hivi karibuni wataanza kutoa huduma za vipimo ya Digital X Ray na ST Scan ambavyo awali vilikuwa vikipatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali.

Kwa mujibu wa Dk. Kiwelu Serikali ina mpango wa kujenga jengo la kisasa la kutolea huduma za Digital X ray na CT Scan na kujenga miundombinu ya kisasa ya kuhudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu ICU.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali hiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi Dk. Petronilla Ngiloi, ameishukuru Serikali kwa kuipa kipaumbele sekt ya afya na kutoa fedha za kutosha kuboresha huduma katika ngazi zote.

“Wananchi wajue Hospitali ya Amana iko katika kiwango cha juu na bado kuna maendeleo na ujenzi wa kuongeza miundombinu ili kuendelea kuboresha huduma. Wagonjwa ambao walikuwa wanahitaji kwenda Muhimbili sasa hivi hawaendi kwa sababu huduma nyingi zinapatikana hapa hivyo, muitumie fursa hiyo,” amesema Dk. Ngiloi.

Mmoja wa wananchi waliopatiwa huduma katika maadhimisho hayo, Judiketi Munisi (53), ameishukuru hospitali hiyo kwa kutoa huduma bora na kuwashauri Watanzania wawe na moyo wa kujitolea damu ili kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles