23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAOMBI RUFAA YA LEMA KUSIKILIZWA DES 14

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)

NA JANETH MUSHI-ARUSHA

MAOMBI ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha nia ya kukata rufaa kuomba dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), yamepangwa kusikilizwa Desemba 14.

Maombi hayo namba 69 ya mwaka huu yaliwasilishwa juzi mahakamani hapo na Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga, ambaye pia anaiomba Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iweze kusikiliza rufaa ya mbunge huyo ambaye yuko katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Upande wa Jamhuri katika maombi hayo ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Matenus Marandu. Maombi ya Lema yanasikilizwa na Jaji Dk. Modesta Opiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama hiyo, Wakili Mfinanga alisema kuwa maombi hayo aliyawasilisha Desemba 7, mwaka huu chini ya hati ya dharura.

Alisema kuwa maombi hayo yalipangwa kusikilizwa jana, lakini ilishindikana baada ya Wakili Marandu kuiomba mahakama iwape muda wa siku 14 ili waandae hati  kinzani.

“Kutokana na maombi ya Wakili wa Serikali kuomba muda wa kupitia maombi hayo na kuwasilisha hati kinzani baada ya siku 14, baada ya kusikiliza pande zote mbili, mahakama ilitumia busara zake na ikatoa amri Desemba 13 wawasilishe hati kinzani ili Desemba 14 saa sita mchana maombi hayo yasikilizwe,” alisema Mfinanga.

Kwa upande wake, Wakili Marandu alisema kuwa upande wowote ukishapeleka maombi mahakamani, upande wa pili una haki ya kupewa muda wa kujibu kwa maandishi.

“Kule ndani miongoni mwa mabishano tuliyokuwa nayo ni pamoja na ulazima wa hati ya dharura katika maombi haya, kwani linapokuja suala la dharura mahakama yenyewe ndiyo inaangalia na kukubaliana na suala husika kama ni la dharura na kuchukua hatua inayostahili,” alisema Marandu.

Miongoni mwa viongozi waliokuwapo mahakamani hapo, ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, wabunge wa viti maalumu wa Chadema Wilaya ya Karatu, Secilia Paresso na Joyce Mukya (Arusha Mjini), Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa na viongozi wengine wakiwamo madiwani wa Chadema wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumza na wafuasi, Dk. Mashinji aliwaeleza kuwa ametoka gerezani Kisongo na kuwa Lema amemtuma salamu zake kwao, na wao kama chama wana imani na mahakama ingawa bado inasuasua.

“Naomba niwape salamu za Lema, nimetoka kumtembelea gerezani, anasema yupo imara na ataendelea kudai haki ya watu wa Arusha,” alisema.

Kwa upande wake, Golugwa aliliomba Jeshi la Polisi mkoani hapa kuacha tabia ya kuzuia wafuasi wa chama hicho kuingia mahakamani hapo.

Desemba 2, mwaka huu, mahakama hiyo ilifuta rufaa ya Lema kutokana na kukatwa nje ya muda na pia alitakiwa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10, tangu maamuzi ya maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya chini kutupwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sekela Moshi, Novemba 11, mwaka huu.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles